Best Blogger TipsSoon

Sonntag, 11. September 2011

TZMPAKAAU

   MV SPICE ISLANDERS ILIVYOPOTEA NA WENZETU!!

  • 190 wafa manji
  • Uzembe umechangia
  • Majeruhi wasimulia walivyookoka
  • Siku 3 za maombolezo zatangazwa
Taifa limepatwa na msiba mkubwa baada ya watu 190 kufa kwa maji baada ya meli ya MV Spice Islander kuzama katika mkondo wa bahari ya Nungwi, Zanzibar.
Meli hiyo ilikuwa ikitokea Unguja kwenda Kisiwani Pemba ikiwa imebeba abiria na mizigo, iliondokea katika bandari ya Malindi mjini Zanzibar.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais, Mohammed Aboud Mohammed, amesema tukio hilo limetokea majira ya saa 7:00 usiku na watu 521 wameokolewa.
Waziri Aboud alisema kwamba orodha ya abiria waliosafiri na meli hiyo inaonyesha walikuwa 610.
Hata hivyo, inaonekana watu hao wameokolewa na Kikosi Maalumu cha Kuzuia Magendo (KMKM), ambao walikuwa wakiwatoa kutoka baharini na kuwapakia katika boti za Sea Express, Seabus, meli ya Jitihada na boti ya bandari inayoitwa Rubani.
Wakizungumza na NIPASHE majeruhi waliosalimika katika ajali hiyo wamesema meli hiyo ilipinduka na kuzama kutokana na mzigo mkubwa uliokuwa imebeba yakiwemo magunia ya mchele, sukari na unga wa ngano.
Mwinyi Bakari (70), mkazi wa Kombeni Pemba alisema kwamba meli hiyo ilianza kuegemea upande mmoja kutokana na mzigo kuwa mkubwa baada tu ya kuondoka katika bandari ya Malindi Zanzibar.
“Mizigo ilikuwa mingi na ilipakiwa vibaya chombo chetu kiliondoka kikiwa kinaegemea upande mmoja na mnamo saa 7:00 usiku meli ilianza kuzama,” alisema Bakari.
Watalii wakitoa msaada kwa walionusurika


Alisema kwamba baada ya meli kupinduka abiria walianza kujitosa baharini na wengine wakikumbatia magunia ya mchele na unga wa ngano ambayo yalikuwa yakielea baharini pamoja na magodoro.“Magunia ya mchele na unga wa ngano yamesaidia sana watu kujiokoa nikiwemo mie mwenyewe,” alisema Bakari.
Said Saleh (25), mkazi wa Mpendae alisema kwamba kutokana na meli kubeba mzigo kupita kiwango ilionekana ikiegemea upande mmoja kabla ya kupinduka na watu kuanza kutokea madirishani. “Siamini kama nimepona, siamini kama nipo salama, kwa sababu tumekumbana na mazingira magumu mawimbi makubwa ya maji yalitupiga hadi tulipookolewa majira ya saa 2:00 za asubuhi,” alisema Said.
Nao wanafunzi waliokolewa katika ajali hiyo walisema walikumbatia magodoro na magunia ya mchele ndio yaliyowasaidia baada ya kuyakumbatia kuanzia saa 7:00 usiku hadi walipookolewa saa 2:00 asubuhi. Watoto wengi waliookolewa na majokofu (friji) yaliyokuwa yakikitupwa majini kupunguza uzito wa meli hiyo.
Mwanafunzi wa shule ya Msingi Kiyuyu Kipangani Mohammed Suleiman Nassor alisema kwamba Keptein wa meli hiyo alitoa tangazo kuwataka abiria waondoke upande wa kulia wahamie upande wa kushoto baada ya meli kuanza kuegemea upande mmoja.
Alisema kwamba wakati hali hiyo inajitokeza kapteni hakuchukua tahadhari yoyote ya kuwataka abiria wavae vifaa vya kujiokoa (life jacket), isipokuwa aliwataka wawe watulivu. “Hatukupewa vifa vya kujiokoa nakumbuka kapteni alisema ondokeni kulia mwende kushoto,” alisema mwanafunzi huyo.
Alisema yeye mwenyewe aliogolea kwa masaa matatu na maji ya bahari yalikuwa yakimvuta kutokana na mkondo mkubwa wa maji katika eneo hilo kabla ya kukiona kifaa maalumu cha kujiokolea kilichokuwa kikielea na mtu mmoja aliyekuwa akishikilia.
“Kama meli za kuokoa abiria zingefika mapema watu wengi wangeokolewa kwa sababu wengine walikuwa juu ya meli kabla ya kuzama yote majira ya saa 12:00 alfajiri,” alisema Ali Suleiman.
Mwanafunzi wa shule ya Kiyuyu Kipangani, Safia Said Salum na Ibrahim Hamad Sheha ambao ni wanafunzi wa darasa la nne walisema kwamba wamefanikiwa kujiokoa baada ya kupitia dirishani kabla ya kujitosa baharini na kuwahi magodoro yaliyokuwa yakielea katika maji. “Meli ilipopinduka nilipanda juu baadae nikajitosa kwenye maji nikabahatika kukutana na godoro ndio limenisaidia hadi nilipookolewa saa 2:00 asubuhi,” alisema Ibrahim Hamad Sheha.
Makamu wa Rais wa Jamhuri yA Muungano wa Tanzania DK, Bilal akiwa na makamu wa Pili wa Rais Wa Zanzibar balozi Seif wakimfariji mmoja kati ya wahanga wa MV Spice Mussa Hemed anayetokea mji wa Wete aliyelazwa katika Hospital kuu ya Mnazi Mmoja

Mwanafunzi Ashura Mselem (14) wa Shule ya Msingi Uwondwe Pemba alisema mwanzo alikumbatia ndoo ya plastiki baada ya meli hiyo kupinduka lakini baadae aliiacha ndoo na kuwahi gunia la unga wa ngano baada ya kuona ndoo imeanza kuingiza maji.
“Mwanzo nilishika ndoo huku miguu ikiwa katika maji baadae nikakumbatia gunia la ngano miguu ikiwa katika maji hadi nilipookolewa asubuhi,” alisema.
Rashid Bakari Hamadi (16), mwanafunzi wa shule ya Mkunjwi alisema kwamba wakati ajali inatokea kwa bahati aliweza kutoka licha ya msongamano na kubahatika kujiokoa kwa kutumia godoro.
Majeruhi hao baada ya kufikishwa katika bandari ya Malindi walikimbizwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mnazimmoja kwa kutumia magari yenye namba za usajili SMZ 5945, KZU 232, na SMZ 7185, Z 703 AE, Z 744 AU, DFP 1379, na SLS 1062.
Hata hivyo, baadhi ya majeruhi walionekana wakisaidiwa kupumua kwa kutumia mitungi ya gesi katika kituo cha huduma ya kwanza kilichoanzishwa ghafla katika bandari ya Malindi Zanzibar kabla ya kuhamishiwa Hospitali ya Rufaa ya Mnazimmoja Zanzibar.
Hata hivyo, wagonjwa waliokuwa mahatuti walikuwa na wakati mgumu kutokana na mashine maalumu za kusaidia mgonjwa mahatuti kuwa zimekufa zaidi ya mwaka mmoja katika Hospitali ya Rufaa ya Mnazi mmoja Zanzibar.
Maiti baada ya kushushwa katika bandari ya Malindi zilianza kupakiwa katika magari yakiwemo ya vikosi vya SMZ na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ). Magari yaliyotumika kuchukua maiti hizo ni 512 JWTZ 07 aina ya IVECO, Z 140 AP Toyota, SMZ 7160 aina ya Hino na SMZ 5720.
Kamishna wa Jeshi la Polisi Zanzibar, Mussa Ali Mussa, alisema Serikali imeamua kuweka kituo katika uwanja wa Maisara kitakachotumika kuwatambua maiti hao.
Alisema kwamba Serikali imeamua kugharamia maiti zote ikiwemo ukoshaji, sanda kabla ya kukabidhi wahusika na kituo hicho kitafanya kazi saa 24 kuanzia jana.
Hata hivyo, alisema maiti ambazo hazitatambuliwa na wahusika zitazikwa na Serikali na kuwataka watu wote ambao ndugu zao walisafiri juzi na chombo hicho wafike katika kituo hicho.
“Chanzo cha kuzama meli bado hatujakifahamu tunaendelea na uchunguzi lakini suala la ukaguzi wa abiria na mizigo ni jukumu la maafisa wa forodha na bandari,” alisema Kamishna huyo.
Wakizungumza na NIPASHE wananchi katika Manispaa ya Zanzibar wamesema ajali hiyo imechangiwa na uzembe wa vyombo dhamana vya kusimamia sekta ya usafiri baharini na uchukuzi.
Said Khalfan, mkazi wa Michenzani alisema kwamba haiwezekani mizigo na abiria ipakiwe kupita kiwango wakati wakaguzi wa meli na mizigo wapo katika bandari hiyo.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akisikiliza maelezo kutoka kwa Dkt. Ally Amour wakati alipofika kumjulia hali mtoto Said Gerald (6) aliyenusurika katika ajali ya Meli eneo la Nungwi usiku wa kuamkia leo, akiwa amelazwa katika Hospitali ya Mnazi Mmoja mjini Zanzibar. Aliyempakata ni mama yake mzazi, Mariam Hemed.
“Waziri na wasaidizi wake akiwemo Mkurugenzi wa Bandari na Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usafirishaji baharini wajiuzulu, huu ni uzembe,” alisema Khalfan.
Alisema kwamba mwaka 2009 meli ya MV Fatihi ilizama Serikali ikaunda tume ya uchunguzi na kueleza kwamba chanzo cha kuzama meli hiyo ni uzembe kwa vile ilikuwa inakabiliwa na uchakavu lakini iliendelea kuchukua abiria.


moja ya boti zilizosaidia shughuli za uokoaji wakisaidiana chupa za maji kwa kurushiana kama inavyoonekana hapa

Hata hivyo, alisema pamoja na ripoti kupendekeza watu kadhaa washitakiwe hakuna hata mmoja aliyefikishwa mahakamani, licha ya ajali hiyo kupoteza watu saba na wengine kadhaa kusalimika.
Time Juma, mkazi wa Mkunazini alisema kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar lazima ianzishe kitengo cha uokozi baharini kwa sababu Zanzibar inategemea sekta ya bahari kwa wananchi wake. “Kama kungekuwa na boti maalumu za uokozi watu wangeokolewa tangu usiku lakini wameanza kuokolewa saa 2:00 asubuhi huu ni ushahidi bado tunaudhaifu wa majanga kama hayo,” alisema Time.
Hata hivyo, alisema kwamba Serikali lazima iwawajibishe viongozi dhamana katika sekta hiyo iwapo watagoma kujiuzulu kwa hiyari yao.
Mkurugenzi Mipango na Sera wa Chama cha Wakulima Tanzania (AFP), Rashid Mchenga amesema kwamba viongozi dhamana lazima wawajibike kwa kushindwa kusimamia sheria ya usafirishaji na uchukuzi Zanzibar.
Alisema kwamba chama chake kitatayarisha maandamano iwapo viongozi hawatokubali kujiuzulu kwa hiyari kwa kuzingatia uzito wa tukio hilo.
“Waziri na wasaidizi wake lazima wajiuzulu hatuoni sababu ya watu kuendelea kupoteza maisha kwa uzembe wa usimamizi wa sheria,” alisema.
DK. SHEIN ASEMA SERIKALI KUWAHUDUMIA WALIOPATA MAAFA
Dk Ali mohamed Shein akimfariji mmoja kati ya wahanga wa ajali ya meli ya MV Spice Islanders
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein amesema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imejiandaa kuwahudumia wale wote waliopatwa na maafa wakiwemo waliokufa na walio hai kutokana na ajali ya kuzama kwa meli ya Spice Islander.

Dk. Shein ambaye alifuatana na mama Mwanamwema Shein, walifika Nungwi mapema asubuhi ambapo pia, viongozi mbali mbali walihudhuria akiwemo Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, Mke wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Asha Balozi, viongozi wa vyama na serikali pamoja na wananchi kutoka maeneo mbali mbali.

Dk.Shein Katikati Malim Seif makamu wa rais wa kwanza wa Zanzibar na kulia ni Mama Mwanamwema Shein, wote wakiwa katika hali ya majonzi kufuatia msiba mkubwa ulioletwa na MV Spice.
Dk. Shein akizungumza  na wananchi ufukwe wa Nungwi ambako baadhi ya maiti na majeruhi walikuwa wakiokolewa, alieleza kuwa tukio hilo kubwa ni la kwanza kutokea Zanzibar na kueleza kuwa tukio hilo pia, limeathiri familia pamoja maendeleo ya nchi.
Alisema kuwa tayari taratibu zimeandaliwa kwa ajili ya kuweka mahali maalum kwa majeruhi pamoja na eneo maalum kwa ajili ya wale waliokufa.
Alisema kuwa kwa wale waliookolewa wakiwa hai wengine wanapelekwa katika hospitali ya Kivunge iliyoko Mkoa wa Kaskazini Unguja kwa ajili ya kuangaliwa afya zao na kwa wale ambao afya zao si nzuri sana watapelekwa katika hospitali Kuu ya Mnazi mmoja.
Dk. Shein aliwaomba wananchi wote kuwa watulivu na kuwapa nafasi madaktari ili waweze kutoa huduma za afya kwa wananchi waliopata matatizo.
Alieleza kuwa wananchi hao wanahitaji huduma muhimu ikiwa ni pamoja na kupata hewa na matibabu mengine.
Alisisitiza kuwa serikali itakuwa inaendelea kutoa taarifa rasmi kwa wananchi kila mara ili wananchi waweze kufahamu hali inavyoendelea na kuwataka waandishi wa habari wanaotoa taarifa juu ya tukio hilo kushirikiana na Idara ya Habari Maelezo kwa ajili ya kupata taarifa sahihi. Alisema jitihada za serikali zinaendelea kuchukuliwa kwa ushirikiano na vikosi vyote vya ulinzi na usalama vikiwemo vya SMZ na vile vya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Aidha, alisema madaktari kutoka taasisi mbali mbali na mashirikika ya maafa yakiwemo Shirika la Msalaba Mwekundu wanaendelea kutoa ushirikiano wao katika kuwahudumia majeruhi. Alisema kikao maalum cha serikali kitakaa, Ikulu mjini Zanzibar kuzungumzia tukio hilo.
Akiwa Nungwi Dk. Shein alipata nafasi ya kuwaangalia na kuwapa pole wale waliookolewa wakiwemo watoto, vijana na wazee wa kike na kiume.
Pia, Dk. Shein alifika katika hospitali ya Kivunge ambako alipata nafasi ya kuwapa pole wagonjwa wa tukio hilo ambao wamelazwa katika hospitali hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari kabla ya kuondoka katika eneo hilo, Dk. Shein alisema kuwa serikali imeajiandaa vizuri na ndio maana imeunda kamati maalum ya maafa ili kuweza kukabiliana na hali kama hiyo.
Aidha, alisema kuwa kutokana na Zanzibar kuwa ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ndio maana imeona kuna haja ya kupata nguvu za ziada kutoka Jeshi la Wananchi wa Tanzania na Jeshi la Polisi ili kusaidia juhudi za uokozi.
Wakati huo huo, SMZ imetangaza siku tatu za maombolezo, sherehe, burudani zimesittishwa na bendera kupepea nusu mlingoti.
Chama cha Kampuni ya Utalii (ZATI) kimeandaa wa harambee kucgangia walioathirika na ajali hiyo.
Mapema akitoa taarifa kwa Dk. Shein Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, Pembe Juma Khamis, alisema kuwa mapema asubuhi waliokolewa baadhi ya watu na wamepelekwa katika hospitali ya Kivunge.
Mkuu wa Mkoa huo pia, alieleza kuwa vyombo mbali mbali vya majini vimeweza kufika katika eneo la tukio na kusaidia kuokoa ikiwemo boti ya Sea Express ambayo iliokoa majeruhi 259 wakiwa hai na maiti 49 ambapo baada ya hapo boti hiyo ilielekea katika Bandari ya Malindi kutokana na kutoweza kufunga gati katika eneo la Nungwi.
Hadi Mhe. Rais anaondoka katika eneo la Nungwi bado juhudi za uokozi zilikuwa zinaendelea na majeruhi mbali mbali walikuwa wakiendelea kushushwa kutoka baharini na kupelekwa katika eneo hilo lililotengwa kwa ajili ya kupata huduma za afya.
Vyanzo:Mbeya yetu,IPPMEDIA,TZMPAKAAU

 

Keine Kommentare:

Kommentar veröffentlichen