Best Blogger TipsSoon

Freitag, 9. September 2011

TZMPAKAAU

Mbowe,Slaa wapuliza kipyenga Igunga,Ben naye atamba
Kutoka kulia ni Katibu ndg Wilbord Slaa,katikati mtu mrefu kuliko wote ni mgombea ubunge wa jimbo hilo Joseph Kashindye na Mwenyekiti wa CHADEMA taifa A. Freeman Mbowe

Umati mkubwa wa wakazi wa Jimbo la Igunga, mkoani Tabora, jana ulijitokeza katika mkutano wa uzinduzi wa kampeni za Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kwa ajili ya uchaguzi mdogo wa ubunge huku chama hicho kikimshambulia Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa, kikimtaka awalipe wananchi kodi ya pango kwa kufanya biashara akiwa Ikulu.
Kombora hilo lilirushwa na Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk.  Willibrod Slaa, aliyezindua kampeni hizo na kuwataka wananchi wa Igunga wamdai Mkapa kodi yao ya pango kesho wakati atakapohutubia mkutano wa uzinduzi wa kampeni za Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Katibu mkuu wa CHADEMA ndg Wilbord Slaa
   
Dk. Slaa alisema kuwa  Rais huyo mstaafu alisajili kampuni ya ANBEM wakati akiwa Ikulu.
Alisema wakati nchi ikiwa katika wimbi la mgawo wa umeme, sehemu mojawapo ya lawama hizo inakwenda kwa Mkapa.
“Akija hapa muulizeni kwamba Mheshimiwa Mkapa ulifanya biashara katika jengo letu la Ikulu wakati ukiwa rais, ukaandika katika anwani yako katika kampuni uliyoanzisha wewe na mkeo Anna… ukaandika awani ya Ikulu,” alisema na kuongeza:
“Mwambieni awalipe leo ada ya pango la kufanya biashara Ikulu kwa sababu wana Igunga mtu akifanya biashara anakulipa pango la nyumba, atulipe Watanzania pango la Ikulu yetu.”
Aidha, alisema iwapo viongozi wakuu wangekuwa wanawajali wananchi wa Igunga, alitegemea kuwa fedha ambazo zinachangishwa kwa ajili ya maadhimisho ya miaka 50 ya uhuru zingeelekezwa katika kutatua kero za wananchi na si vinginevyo.
Dk. Slaa alisema ni kilio cha nchi nzima kuwa fedha zinazochangwa na Watanzania kwa ajili ya maadhimisho hayo zisiende katika sherehe ya siku moja, badala yake ziende katika kutatua kero.
MBOWE AISHAMBULIA SERIKALI

Mwenyekiti wa CHADEMA taifa ndg A. Freeman Mbowe
Akimnadi mgombea wa Chadema, Joseph Kashindye, Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, alisema serikali ya CCM ni serikali ya omba omba na ni ya anasa.
“Tulimwambia Waziri Mkuu Pinda simamia uuzaji wa mashangingi, okoa fedha,” alisema na kuongeza kuwa baaada ya hapo watu wakamwambia mbona na yeye (Mbowe) anatembelea shangingi, akaamua kulirudisha.
Aidha, Mbowe ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Hai, alisema kuwa wananchi wamekuwa wakizidi kukabiliwa na hali ngumu ya uchumi na kuwataka  wasikichague tena CCM.
KASHINDYE: NICHAGUE NIWAWAKILISHE
    
Naye mgombea ubunge jimbo hilo la Igunga kwa tiketi ya CHADEMA bw Joseph Kashindye hakuwa nyuma
Kwa upande wake, Kashindye aliwataka wananchi wa jimbo hilo kumchagua ili aweze kwenda kutatua kero zinazowakabili.
“Ukiona mwalimu anaenda kusimama katika jukwaa la kisiasa hali ni mbaya….tumeambiwa kuwa kuna mabilioni ya fedha yanayoletwa kwa ajili ya maendeleo, lakini wanaosimamia ni viongozi wa CCM ambao hawana uchungu na jimbo hili,” alisema.
Alisema yeye alikuwa akiingia katika vikao vya Halmashauri ya Igunga na kwamba hakuna aliye na uchungu na mali za Watanazania
Alisema kuwa CCM imekuwa ikifikiri kuwa watumishi wote wa serikali ni mali yao, jambo ambalo sio la kweli na ndio maana yeye aliamua kujiunga na Chadema ili kuleta ukombozi wa kweli.
Mkutano huo uliwashirikisha wabunge mbalimbali akiwemo Slvester Kasulumbayi, (Maswa-Mashariki); Joseph Mbilinyi (Mbeya Mjini); Meshack Upurukwa (Meatu); wabunge wa viti maalum Suzan Kiwanga, Joyce Nkya, Paulina Gekuli, Rose Kamili na wajumbe wa Kamati Kuu,
MAPOKEZI KWA MAANDAMANO
Basi mapokezi ya CHADEMA yalikuwa hivyo

Kabla ya mkutano huo, wafuasi wa chama hicho walikwenda kuwapokea viongozi wa ngazi za juu kwa maandamano umbali wa kilometa tatu kutoka mjini Igunga.
Maandamano hayo yalipambwa na shamshamra nyingi ikiwemo nyimbo za Chadema, mabango yenye ujumbe mbalimbali huku baiskeli na bajaji zikiwa zimefungwa bendera za chama hicho.
Mbali na hilo umati wa watu ulijazana katika uwanja wa Sokoine, hali ambayo iliwafanya baadhi yao kupanda juu ya miti ili waweze kushudia kinachoendelea wakati wa mkutano wa kampeni.
MBUNGE SUGU ATUMBUIZA

 Mbunge wa mbeya mjini Joseph mbilinyi a.k.a Sugu akiwatumbuiza mashabiki wa CHADEMA Igunga

Kabla ya kufungwa mkutano huo, Mbunge wa Mbeya Mjini Joseph Mbilinyi, alipewa nafasi ya kutumbuiza umati wa watu waliojazana katika viwanja hivyo ambavyo vipo mkabala na ofisi za makao makuu ya CCM Wilaya ya Igunga.
MKAPA ATUA NA KUTAMBA
Basi kulia ni rais wa awamu ya tatu Benjamin Mkapa,Katikati ni katibu wa fedha NEC Mwingulu Nchemba na kushoto akisalimiana na Ben ni Mgombea Ubunge jimbo hilo Dalaly P.Kafumu

Wakati Dk. Slaa akimrushia Mkapa kombora hilo, Rais huyo mstaafu aliwasili Igunga jana kwa ajili ya kufungua kampeni za CCM kesho. Aliwasili jioni huku akiwaeleza wakazi wa Igunga kuwa CCM kitapata ushindi.
Akitoa kauli hiyo wakati akipokelewa katika Kijiji cha Makomero umbali wa kilomita chache kutoka mjini Igunga.
Viongozi waandamizi wa CCM walihudhuria mapokezi hayo wakiwe Mratibu wa Kampeni za chama hicho na Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) wa Uchumi na Fedha, Mwigulu Nchemba; Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tabora, Hassan Wakasuvi na Katibu wa NEC wa Oganaizesheni, Asha Abdallah Juma.
Mapokezi ya Mkapa yalipambwa na vijana waliokuwa wakiendesha baiskeli na pikipiki.
Mkapa aliwataka wananchi wa Igunga kujitokeza kwa wingi siku ya uchaguzi huo Oktoba 2, mwaka huu kupiga kura mgombea wa CCM Dk. Peter Kafumu.
Aliwaambia wananchi hao na wapenzi wa CCM kuwa atazungumza mambo mengi kesho wakati wa uzinduzi wa kampeni za mgombea wao.

Vyanzo:Ippmdeia,TZMPAKAAU na FULL SHANGWE

Keine Kommentare:

Kommentar veröffentlichen