Best Blogger TipsSoon

Donnerstag, 8. September 2011

TZMPAKAAU

Mwanasheria na Mwanaharakati machachari sasa awekwa kiti moto!!
  
Mwanasheria na Mwanaharakati machachari nchini, Kainerugaba Msemakweli, jana alianza kuhojiwa rasmi na kikosi kazi kinachoundwa na timu ya maofisa kutoka vyombo vitatu vya dola nchini.
Msemakweli, ambaye mwaka jana aliwataja baadhi ya mawaziri na wabunge kuwa ni mafisadi wa elimu kutokana na kudanganya elimu zao, anahojiwa na kikosi kazi hicho kuhusu ushahidi alioibuka nao wa kuipeleka mahakamani Kampuni ya Kagoda Agriculture Limited.

Kagoda inatuhumiwa kukwapua Sh. bilioni 40 kati ya Sh. bilioni 133 zilizoibwa na kampuni nyingine 22 katika Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (Epa) ndani ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Kikosi kazi hicho kinaundwa na maofisa waandamizi kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (Takukuru), Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) na Jeshi la Polisi.

Mahojiano hayo yalianza rasmi jana, zikiwa zimepita siku sita, baada ya kikosi kazi hicho kufanya mahojiano ya utangulizi na Msemakweli kuhusu ushahidi huo, Septemba 3, mwaka huu. 

Kwa mujibu wa Msemakweli, jambo kubwa aliloliandika katika mahojiano hayo ya awali yaliyofanywa na kikosi kazi hicho siku hiyo, lilihusu kwamba analijua suala la Kagoda kwa kina na anao ushahidi wa kuipeleka mahakamani na kwamba, yuko tayari kuupeleka mbele yao (kikosi kazi).

Hatua hiyo ilichukuliwa na vyombo hivyo, siku chache, baada ya Msemakweli, kuwasilisha ushahidi huo kwa Ofisi ya DPP.
 
Director of Public Prescution (DPP) bw. Eliezer Feleshi
Mahojiano yalifanyika saa chache, baada ya Msemakweli kukutana na DPP, Eliezer Feleshi na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Kamishna Robert Manumba, ofisini kwa DPP siku hiyo.

Kwa mujibu wa Msemakweli, alikwenda siku hiyo kwa DPP baada ya kuitwa na Felesh kwa ajili ya mazungumzo kuhusu ushahidi aliouwasilisha ofisini kwake.
Advera Senso Msemaji wa jeshi la polisi kama anavyoonekana kushoto

Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, Mrakibu Msaidizi (ASP) Advera Senso, jana alithibitisha kufanyika kwa mahojiano hayo na kwamba uchunguzi kuhusu ushahidi alioibuka nao Msemakweli unaendelea.

Habari zilizolifikia NIPASHE jana zinaeleza kuwa mahojiano kati ya Msemakweli na kikosi kazi hicho yalifanyika kwa zaidi ya saa nne.

Haikuweza kufahamika mara moja mambo aliyohojiwa Mwanaharakati huyo na kikosi kazi hicho jana.

Kwa mujibu wa habari hizo, mahojiano hayo yanafanyika katika Ofisi za Kikosi Kazi (TFO) zilizoko Mikocheni, jijini Dar es Salaam. Yanatarajiwa kuendelea tena keshokutwa.

Msemakweli alipoulizwa na NIPASHE jana, hakuwa tayari kueleza kwa undani kuhusu mahojiano hayo ya jana.
Hata hivyo, alithibitisha kuwa yalifanyika kwa muda huo.

“Nisingependa kueleza kwa siku ya leo mambo waliyonihoji,” alisema Msemakweli.

Alipotakiwa kueleza sababu za kutokuwa tayari kueleza alichohojiwa jana, Msemakweli alisema: “Nitavuruga upelelezi. Napenda wafanye kazi yao kwa uhuru na amani.”

ASP Senso alipoulizwa na NIPASHE jana kuhusiana na mahojiano hayo, alisema yanaendelea.

“Uchunguzi kuhusu mambo ya Msemakweli unaendelea. Taarifa zikikamilika ni haki yetu kuiarifu jamii. Hivyo tutawaita na kuwaambia,” alisema ASP Senso.

Kikosi kazi baada ya kumhoji Msemakweli Ijumaa iliyopita kilitarajia kuendelea kumhoji Jumatatu wiki hii, lakini mahojiano hayo hayakufanyika.

Msemakweli alisema mahojiano hayo yalisitishwa baada ya (Msemakweli) kuugua ghafla malaria na homa ya matumbo.
Hata hivyo, Takukuru, Polisi na ofisi ya DPP hawakuwa tayari kueleza sababu zilizosababisha kuahirishwa kwa mahojiano hayo Jumatatu.

Septemba 2, mwaka huu, Msemakweli alikutana na waandishi wa habari na kuwaeleza kuwa amefanya uchunguzi na kupata ushahidi unaoweza kuipeleka Kagoda mahakamani kujibu tuhuma za ufisadi zinazoikabili.

Msemakweli alisema ushahidi huo aliuwasilisha kwa DPP.

Alisema katika ushahidi wake kwa DPP, amewataja wamiliki saba halali wa kampuni hiyo, wakiwamo wafanyabiashara Yusufu Manji na aliyekuwa Mbunge wa Igunga, Rostam Aziz.
 
Mbunge wa Igunga aliyejiuzuru bw. Rostam Aziz


Bw.Yusuf Manji

Msemakweli alisema pia aliwasilisha kwa DPP baadhi ya vielelezo vinavyoonyesha kwamba wahusika hao saba waliratibu na kuiba dola za Marekani milioni 30.7 kutoka Epa.

Alidai amefanikiwa kukusanya na kufahamu ushahidi unaowaunganisha moja kwa moja Rostam, Manji, Gulam Chakaar, Bahram Chakaar, John Kato, Barati Goda na Tabu Omary, kuwa ni wahusika wakuu katika wizi huo.

Vyanzo:Ippmedia,TZMPAKAAU,fikra pevu,Global Publishers

Keine Kommentare:

Kommentar veröffentlichen