Best Blogger TipsSoon

Donnerstag, 23. Juni 2011

TZMPAKAAU

Oscar Kambona :Upande wa pili wa shilingi

Na Maggid Mjengwa                                                                                  


”KAMBONA, ah, ah! Kambona, ameolewa, Wapi? Huko Ulaya! Wivu, wamkereketa!”



Oscar Salathieli Kambona




siku zote, wanadamu tunapaswa kufanya jitihada ya kuitafuta kweli. Tufanye hivyo ili tuyapate maarifa mapya. Wimbo huo hapo juu ni wa mchakamchaka. Uliimbwa na kaka na dada zetu mashuleni. Kuna wengi tuliousikia. Tukaamini, lakini kuna tuliojengewa kiu ya kutaka kujua ukweli wa jambo zima.

Naam. Mwaka huu tunaadhimisha miaka 50 ya Uhuru wetu. Na kwa mwanadamu, ili uweze kuyaelewa yanayotokea leo, na uweze kubashiri yatakayotokea kesho, basi, ni vema na ni busara ukajitahidi kuyajua yaliyotokea jana.


Kizazi cha sasa cha Watanzania kitapata maarifa mapya na hata kusaidiwa kuyaelewa yanayotokea leo kwa kukumbushwa na kusaidiwa kuyajua yaliyotokea jana. Maana; kuna waliojenga msingi wa nchi hii.
Mapungufu mengine tunayayaona leo yanatokana na makosa ya jana yaliyofanywa na waliojenga msingi wa nchi hii. Ni makosa ya kibinadamu.Ni mwanadamu gani asiyekosea?




Mwalimu Julius Nyerere mbele,nyuma ni Oscar Kambona

Tutafanya makosa kuadhimisha miaka hamsini ya uhuru wetu bila, japo kwa uchache, kujadili kilichowatokea marafiki hawa watatu na athari zake kwa Tanzania yetu ya leo.

Utabaki kuwa ni ukweli kuwa, kama Taifa, ya Kambarage, Kambona na Kawawa ni sehemu ya historia yetu . Maana; sio tu historia ya harakati za kudai uhuru wa Tanganyika na hata kuanzishwa kwa TANU, bali historia ya nchi yetu haiwezi kukamilika bila, mathalan, kutajwa kwa jina hili: Oscar Kambona.

Lakini, kwa miaka hamsini sasa, ukweli juu ya nini kilichotokea mpaka Oscar Kambona akaikimbia nchi yake aliyozaliwa haujawekwa hadharani umma ukaelewa. Kwa Watanzania wengi, Oscar Kambona na kukimbia kwake nchi inabaki kuwa simulizi ya upande mmoja.
Na kwa vile shilingi ina pande mbili, hata ukichukia pande moja ya shilingi, si busara ukakaa na kuubondabonda upande unaouchukia. Bado ni shilingi yako.

Utotoni nimesikia simulizi za Oscar Kambona. Shuleni hatukusoma habari za Oscar Kambona na mchango wake katika kuanzishwa kwa TANU na ujenzi wa chama hicho na hata ushiriki wake katika harakati za kudai uhuru wa Tanganyika.


Tuliosikia simulizi za Oscar Kambona tuliaminishwa kuwa, Kambona alikuwa msaliti kwa nchi yake. Kambona alikuwa bepari na alichukia Ujamaa. Kambona alikuwa mhaini na hata huko Ulaya alikokimbilia, alipanga njama za kumpindua rafiki yake wa zamani, Julius Nyerere. Naam, kulikukwa na simulizi nyingi mbaya juu ya Oscar Kambona.
Na katika dunia hii kuna wanaodhani wanajua, na kuna wale ambao wanajitahidi kujua. Nimechagua kuwa katika kundi hilo la pili; wanaojitahidi kujua.

Kazi hii ya kuutafuta ukweli hasa wa nini kilitokea miaka hamsini iliyopita, ni moja ya jitihada tunazopaswa kuzifanya wakati tukiwa hai; kujitahidi kujua.


Nimesikia simulizi za utotoni juu ya Oscar Kambona. Katika utu uzima wangu huu nimejitahidi kuyatafuta maandiko yenye kumhusu Kambona na wenzake wa enzi za Tanganyika.





Na hakika, kisa cha marafiki watatu; Kambarage, Kambona na Kawawa kinatoa somo muhimu kwa Watanzania wengi wa kizazi cha sasa.


[nyirenda-4.jpg]


Sio mbaya mtu ukijua mashujaa mbalimbali wa Tanzania. Pichani ni Hayati Baba wa taifa Mwl Nyerere akiwa na hayati  Major Alex Gweba Nyirenda  huyu ndiye shujaa aliyepandisha mwenge wa uhuru mlima kilimanjaro desemba tar 9,1961.


Nimejiridhisha kuwa Oscar Kambona alikuwa Mtanzania mzalendo wa nchi hii. Alitofautiana kimisimamo na rafiki yake Julius Nyerere juu ya namna ya kuendesha mambo katika Tanganyika huru, akaamua kuondoka yeye na familia yake.

Kilichofuata, ndani ya propaganda na uvumi ule dhidi ya Kambona kwa jinsi alivyoondoka, kulikuwa na ’ kimya kizito’. Ni kimya kilichodumu kwa nusu karne sasa. Ni kimya kwa vile hakukuwa na nafasi ya kusikia kutoka kwa Oscar kambona mwenyewe, jibu la swali hili muhimu; Kwanini Kambona aliondoka?

Na kulitafuta jibu la swali hilo kutatusaidia kuyaona makosa yaliyofanyika nyuma ili kuepuka kuyarudia tena. Maana, kimya kile cha miaka hamsini kwa namna moja au nyingine, kimesababisha kuyarudia baadhi ya makosa yaliyofanywa na waliojenga msingi wa taifa hili.

Tunajua leo, kuwa Kambona alitofautiana na Nyerere juu ya utekelezaji wa Azimio la Arusha. Alikuwa na mtazamo tofauti; hivyo basi, hakukuwa na dhambi ya kufikiri tofauti.

Kambona alihoji mantiki ya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya chama kimoja bila upinzani wa kisiasa. Hakukuwa na dhambi ya kufikiri hivyo.

Tunaona sasa, msingi huo huo uliojengwa wa kuamini kuwa upinzani wa kisiasa ni uadui, ni dhambi, ndio kwa kiasi kikubwa umelifikisha taifa letu hapa lilipo.

Kwa nusu karne sasa, chini ya chama kimoja tawala, imejengeka misingi ya viongozi kulindana. Na fursa ilipopatikana, baadhi ya viongozi wetu wamekuwa matajiri wakubwa kwa njia haramu.

Tujiulize; Kambona alifanya dhambi gani kubwa kiasi cha kupata adhabu ile kubwa ya kukaa uhamishoni kwa miaka 25? Mandela alimzidi Kambona kwa mwaka mmoja katika ‘kutupwa gerezani’.

Na katika hili la Kambona na Nyerere kuna mengi ya kujiuliza: Hivi inawezekanaje marafiki wawili walioshibana wakafikia kufarakana kwa kiasi tulichokishuhudia? Ikukumbukwe, Nyerere na Kambona walikuwa marafiki kiasi cha Kambona kumfanya Nyerere kuwa ‘Mpambe wa Bwana Harusi’ kwenye harusi ya Kambona iliyofanyika London, Uingereza.








Ukiona hili jiwe la msingi linaloonekana kusahauliwa ujue umefika Tabora Boys a.k.a Kambini hii shule imefyatua viongozi wazuri sana kama huamini waulize wenzake Mwl Nyerere


Labda utajiuliza; urafiki wao ulianzaje? Nyerere alikutana na Oscar Kambona wakati Kambona alipokuwa shuleni Tabora mwishoni mwa miaka ya 40. Inasemwa kuwa Nyerere alimtangulia kiumri Oscar kwa kupishana miaka mitatu tu.
Kule Tabora Nyerere alikutana pia na Rashid Kawawa; naye alimzidi kiumri kwa miaka mitatu hivi. Hivyo basi, twaweza kusema kuwa urafiki wa Julius, Oscar na Rashid ulianzia Tabora, na harakati zao za pamoja za mapambano ya kisiasa zilianzia huko huko Tabora.
Julius Nyerere alikuwa Mkatoliki na hodari sana shuleni, akafika mpaka Uingereza kimasomo. Aliporudi akafanya kazi ya ualimu pale Pugu.

Alipoambiwa achague kati ya ualimu na siasa, Julius akachagua siasa.


Oscar naye alikuwa mwumini wa kanisa la Anglican na hodari sana shuleni. Naye akafika mpaka Uingereza kusomea sheria. Hakumaliza masomo yake, Nyerere alimshawishi akatishe masomo yake, arudi nyumbani kuimarisha TANU kwenye uchaguzi uliokuwa mbele yao.
Rashid Kawawa alikuwa Mwislamu. Alisoma mpaka Tabora, hakufika Uingereza, lakini akawa kiongozi mahiri wa vyama vya wafanyakazi . Katika TANU alikuwa ni mpiganaji wa kuaminika. Rashid alikuwa maarufu mjini. Alipata hata kucheza filamu maarufu ya ’ Mhogo Mchungu’.





Hayati Rahid Kawaka akiwa bado kijana



Rashid Kawawa hakuwa maarufu kama waziri mkuu tu lakini enzi za ujana wake alikuwa maarufu mji mzima


Rashid Kawawa kama mgeni rasmi miss Tanzania

Watatu hawa walikuwa marafiki, hilo halina shaka. Na baada ya Uhuru wa Tanganyika, Julius na Oscar walijenga nyumba zao pale kijijini Msasani kwenye pwani ya bahari. Naam. Walikuwa karibu sana kikazi na walichagua kuishi pamoja kama majirani.

Inasimuliwa kuwa nyakati za jioni, Oscar na Julius walipenda sana kutembea pamoja ufukweni pale Msasani wakijadiliana mambo mbalimbali. Bila shaka wake zao - Maria na Flora walitembeleana na hata ‘kuombana chumvi’.



Hayati mwalimu Kambarage Nyerere na mke wake Maria Nyerere

Lakini ilifika wakati Oscar na Julius hawakuonekana tena wakitembea pamoja ufukweni. Na pengine Maria na Flora hawakutembeleana na kuombana chumvi. Ikafika wakati pia Oscar na familia yake wakafungasha mizigo yao na kuondoka nchini kupitia Namanga. Nyumba yao ikaja kupata mpangaji mpya; Milton Obote, rafiki mwingine wa Julius Nyerere.

Oscar Kambona

Na mjini Dar es Salaam ukatawala uvumi zaidi kuliko ukweli wa kilichotokea. Ikasemwa kuwa Kambona ametoroka akiwa na sanduku limejaa pesa. Na pesa yetu wakati ule ilikuwa na thamani sana. Fikiri sasa kama sanduku la Kambona lilijaa manoti!


Na utotoni pale Ilala, nilipata kusikia uvumi kuwa huko Ulaya, Kambona amekuwa tajiri mkubwa. Wengine wakasema alishinda bahati nasibu. Wengine wakasema ni fedha alizotoroka nazo.

Na kuna wakati ukaenea uvumi kuwa kuna meli bandarini imezuiliwa kushusha shehena ya vitanda. Ni vitanda ambavyo Kambona alivituma Tanzania ili vitumike mahospitalini.

Kwa vile ukweli hasa kuhusu ugomvi wa Kambarage na Kambona haukupata kusemwa, basi, uvumi ukaendelea kusambazwa. Hivyo basi ’kimya kikuu’.
Makala haya ni jaribio la kuvunja ukimya wa juu ya nini kilitokea miaka hamsini iliyopita, na nini cha kujifunza.



Itaendelea.

Keine Kommentare:

Kommentar veröffentlichen