Best Blogger TipsSoon

Mittwoch, 25. Mai 2011

TZMPAKAAU

      TARIME HAPAKALIKI
  • Maiti za waliouwawa zatelekezwa barabarani
  • Tundu Lisu na waitara waswekwa rumande
  • Mbunge Matiko na waandishi wanne wa habari nao wakamatwa


                   Wananchi wa Tarime leo asubuhi, walipomkuta marehemu wao katikati ya barabara


Jeshi la polisi limewafikisha mahakamani watu wanane akiwemo mbunge wa jimbo la Singida Mashariki ambaye pia ni mwanasheria wa chama cha Chadema, Tundu Lissu.
Wengine ambao walifikishwa mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Tarime, Yusto Ruboroga, ni pamoja na wasaidizi wa mbunge huyo na Mkurugenzi wa Sera na Utafiti wa chama hicho, Mwita Waitara kufuatia sakata la mauaji ya raia Tarime mkoani Mara.


Mbunge wa Singida Mashariki kwa tiketi ya CHADEMA Tundu Lissu


Polisi wa kikosi cha kutuliza ghasia FFU wakiimarisha ulinzi



Watuhumiwa hao walifikishwa mahakamani hapo saa 7:00 mchana chini ya ulinzi mkali wa Polisi wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) waliokuwa na silaha mbalimbali yakiwemo mabomu ya kutoa machozi kisha kufunga njia zote za kuingia na kutoka mahakamani hapo ambapo Lissu na Waitara, walionekana kuchechemea wakati wakishuka katika magari huku nguo zao zikiwa zimelowa damu.
Hatua hiyo ilileta kizaa zaa kwa ndugu waliokuwa eneo hilo kwa ajili ya kutoa dhamana kwa ndugu zao ambao waliamuliwa kukaa mita mia 200 kutoka eneo la mahakama huku baadhi ya maofisa wa mahakama waliokuwa nje wakati huo pia wakizuiwa kusogelea eneo hilo.


Viongozi wa Chadema wakiongozwa na mbunge wa Nyamagana, Ezekiel Wenye na Mstahiki Meya wa Manispaa ya Musoma ni miongoni mwa viongozi waliokuwa wakishughulikia dhamana hiyo, ambayo hata hivyo hawakufanikiwa. Akizungumza wakati watuhumiwa hao wakipandishwa katika magari kupelekwa rumande katika gereza la wilaya ya Tarime, Wenje alisema kitendo kinachofanywa na polisi katika wilaya ya Tarime kinaweza kusababisha chuki zenye madhara makubwa katika siku za usoni.



WAANDISHI, MBUNGE WAKAMATWA

Katika hatua nyingine, polisi imewashikilia waandishi wa habari wanne pamoja na mbunge wa viti maalumu kupitia Chadema (Viti Maalum), Esther Matiko na kada wa chama hicho John Heche, kwa muda wa zaidi ya saa sita, kisha kuamuru kila mtu kujidhamini na endapo atapatikana na hatia jeshi hilo litamkamata na kuendelea kumhoji.

Kushoto ni  Mbunge wa CHADEMA
viti maalum  Esther Matiko



Waandishi hao walikamatwa katika kijiji cha Nyakunguru wakiwa njiani kuelekea kijiji cha Kewanja kwa lengo la kupata uhakika wa miili ya watu wanne kati ya watano waliouawa na polisi katika eneo la Nyamongo kudaiwa kutupwa barabarani na jeshi la polisi juzi usiku baada ya kuichukua miili hiyo chumba cha maiti cha hospitali ya wilaya Tarime.

Waandishi waliokuwa wamekamatwa ni Berdina Nyakeke (The CITIZEN), Anthony Mayunga (MWANANCHI), Mabere Makubi (Channel Ten) pamoja na Anna Mrosso (NIPASHE).


Hata hivyo, waandishi hao walipofika katika eneo la kijiji cha Nyakunguru walikuta mwili wa marehemu Emmanuel Magige ukiwa katikati ya barabara ukiwa umejaa ukungu juu ya jeneza.
NIPASHE ilipozungumza na baadhi ya wanakijiji walisema kuwa waliamka majira ya alfajiri saa 11:00 na kuona jeneza likiwa barabarani.


“Watu waliposogea tulifungua kuangalia ndani tukakuta mwili wa marehemu hali iliyozidi kutuchanganya, kwa kuwa ndugu zetu waliokuwa na mwili wa marehemu hatukuwaona, baadaye tuliwapigia simu wakatueleza kuwa mwili huo uliibiwa usiku na polisi,” alisema Janesi Ghati kaka wa marehemu.
Kwa upande wake, Matiko alisema kuwa juzi saa 4:00 usiku, walipata taarifa kutoka kwa wanachama wao kuwa wamewaona polisi wakinunua majeneza manne, ambapo yaliwapa wasiwasi kuwa huenda walikuwa na njama za kuiba miili hiyo usiku.


Kufuatia hali hiyo, Matiko alisema ilikwenda katika eneo la chumba cha kuhifadhi maiti ili kuchunga polisi hao wasichukue miili hiyo na ndipo vurugu zilipoanza na watu hao kukamatwa.
Alisema baada ya watu hao kukamatwa, polisi waliingia katika chumba cha maiti na kuchukua miili hiyo na kuanza safari ya kusafirisha miili hiyo bila idhini ya wafiwa huku Chadema tukibaki na majeneza matupu.
Alisema miili hiyo iliwekwa katika majeneza bila kuvikwa nguo za aina yoyote wala sanda hali ambayo alisema ni ya udhalilishaji wa hali ya juu wa maiti za binadamu. Alisema baada ya miili hiyo kufikishwa katika kila kijiji, wanakijiji walizikataa na kuwataka polisi kuzika wenyewe, hivyo kuitelekeza barabarani na iliendelea kubaki hapo hapo barabarani.


Kwa upande wake, Kamanda wa Kanda Maalum ya Polisi Tarime/Rorya, Costantine Massawe, alipoulizwa kuhusu polisi kupora maiti hizo bila idhini ya wafiwa tena usiku, alisema kuwa walichukua miili hiyo baada ya wafiwa hao kuwaomba msaada wa kuwapelekea miili hiyo katika vijiji vyao.
Hadi jana jioni miili hiyo ilikuwa bado imetelekezwa barabarani, huku ndugu wa marehemu wakiwa mjini Tarime wakitaka polisi kurejesha miili hiyo ili ichukuliwe na kuzikwa kwa heshima zote na mila za Kikurya.
“Mimi nimefiwa na mtoto wangu Emmanuel Magige, jana tuliambiwa asubuhi ndio tutachukua miili ya watu wetu tukazike sasa tumeamka tunaambiwa eti polisi walichukua marehemu wamekwenda kuwatupa porini na sisi tuko hapa Tarime. Hatujui hii ni serikali kweli?” Alihoji mzee Magige Ghati, baba wa marehemu.

Marando Azungumza

Jijini Dar es Salaam Mwanasheria Mwandamizi wa chama hicho, Mabere Marando, alizungumza na waandishi wa habari akiwaelezea kuhusu mkasa huo



Bw:Mabere Marando Kulia akizungumza na vyombo vya habari

Marando aliwataja waliokamatwa kuwa wabunge Lissu na Matiko, waandishi Mroso, Mayunga, Nyakeke na Makubi pamoja na wananchi na viongozi wa ngazi mbalimbali wa chama hicho wapatao 14.
Alisema polisi waliendesha kamata kamata ya watu hao kwa nia ya kuzuia wananchi wa mji wa Tarime kushiriki kwenye shughuli ya kuaga miili ya wenzao waliouawa na polisi, kitendo ambacho kilikuwa kinyume cha makubaliano waliyokuwa wameyafikia.


“Tundu Lissu na mimi, tulitumwa na chama chetu kwenda kufuatilia suala la mauaji wa Watanzania hao ambao ni wanachama wetu ili kupata usahihi wa namna yalivyofanyika na hasa baada ya kusoma kwenye magazeti kwamba waliouawa ni majambazi. Ukweli ulivyo ni kwamba waliouawa si majambazi bali ni wananchi wa kawaida,” alisema.

Alisema baada ya kupata uhakika kuwa waliouawa si majambazi kama ilivyoripotiwa, alienda chumba cha maiti hospitali ya wilaya ya Tarime kuona hali halisi ya maiti ilivyo, alihakikishiwa na mhudumu mmoja kwamba zilikuwa katika hali nzuri kwa kuwa zilikuwa zimeshatibiwa.





Mkuu wa operesheni wa jeshi la polisi ndugu Paul Chagonja


Alisema Jumapili asubuhi alikutana na Kamishina wa Polisi wa Operesheni, Paul Chagonja, Kamanda Massawe, viongozi wa Chadema wa wilaya na kukubaliana kufanya uchunguzi wa maiti na namna mazishi hayo yatakavyofanyika kwa kuwa Chadema ilikuwa imejitolea kugharimia mazishi hayo. Alisema zoezi la uchunguzi wa maiti lilienda vizuri na lilifanywa na daktari wa kujitegemea kutoka Mwanza na kushuhudiwa na ndugu wa marehemu na Chadema kwa kuwa marehemu walikuwa wanachama wao.
Marando alisema walikubaliana kwamba jana ingekuwa ni siku ya kuwaaga marehemu katika uwanja wa Sabasaba Tarime kwa heshima zote za kichama na kwamba marehemu wangechukuliwa kutoka chumba cha maiti kwa magari.


Alisema walikubaliana kuwa baada ya kuagwa, kila marehemu angepelekwa kuzikwa kwao.
Alisema juzi jioni walipata habari za siri kutoka ndani ya Polisi kuwa wanajiandaa kwenda kuzichukua maiti hizo na kuzisafirisha makwao kwa mazishi kinyume cha makubaliano waliokuwa wameyafanya.
Alisema kitendo hicho kiliwafanya wananchi waelezane na kwenda kuzilinda maiti pale hospitali ili zisichukuliwe.
Alisema ilipofika saa 12 jioni, umeme katika mji huo ulizimwa na ndipo magari ya polisi yalipomwagwa na kuanza kupiga na kukamata kila waliyemkuta njiani, huku wakitangaza kwamba hairuhusiwi kutoka nje. Katika kipindi hicho, polisi ilizichukua zile maiti na kuzisafirisha kwenda makwao.
Alisema marehemu wawili walipelekwa Serengeti, mmoja katika kijiji cha Nyakangwa na mwingine katika kijiji cha Marinda.


Alisema polisi walipoondoka wananchi walipigiana simu ambapo maiti zilipofika makwao zilikataliwa.
Marando alifafanua kwamba katika kijiji cha Nyakangwa maiti ya Emmanuel Magiga ilitupwa barabarani na polisi, baada ya kukataliwa kupokelewa na wazazi wa marehemu ambapo polisi waliondoka na kuiacha hapo.

Alisema baada ya waandishi wa habari kupata taarifa waliondoka kwenda kushuhudia kulichokuwa kikiendelea, ambao walikamatwa njiani na kuwekwa ndani.

Vyanzo :NIPASHE,TZMPAKAAU,MICHUZI

Keine Kommentare:

Kommentar veröffentlichen