Best Blogger TipsSoon

Montag, 9. Mai 2011

TZMPAKAAU

  Upinzani waitahadharisha serikali ya umoja wa kitaifa




Vyama vya upinzani vimesema Zanzibar inaelekea kubaya kiuchumi na vimeitaka Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Zanzibar (GNU), kuchukua hatua za haraka kuondoa kodi katika bidhaa za vyakula ili kuwapunguzia wananchi makali ya mfumuko wa bei.


Viongozi wa vyama hivyo, wamesema hali ya uchumi imezidi kuzorota tangu kuundwa kwa serikali hiyo na kusababisha kiwango cha mfumuko wa bei kuathiri sehemu kubwa ya wananchi, hasa wa kipato cha chini.
Tamko hilo lilitolewa na viongozi wa vyama vya Tanzania Democratic Alliance (Tadea), NCCR-Mageuzi na Chama cha Wakulima (AFP), walipokuwa wakitoa tathimini ya Serikali ya umoja wa kitaifa katika mkutano na waandishi wa habari kwenye ukumbi wa Idara ya Habari (Maelezo) mjini hapa.

Mwenyekiti wa AFP, Said Soud Said alisema hivi sasa kilio kikubwa cha wananchi ni kupanda kwa bei za bidhaa, hasa vyakula katika soko la ndani la Zanzibar. Alisema kabla ya kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa wananchi walijenga matarajio makubwa kwamba ingeleta unafuu wa maisha tofauti na hali ilivyokuwa kabla ya kuundwa kwa serikali hiyo.

Alisema licha ya mfumuko wa bei za vyakula, huduma za afya pia zinazidi kuzorota kutokana ukosefu wa dawa hospitalini ambako huduma pekee inayopatikana ni wagonjwa kuonana na daktari na kuandikiwa dawa ambazo hazipatikani karibu katika vituo vyote vya afya vya serikali.
Soud alisema Serikali ya Umoja wa Kitaifa isione haya kuwaondoa madarakani mawaziri wanaoshindwa kuleta mabadiliko yanayotarajiwa na wananchi kutoka Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
Katibu Mkuu wa Tadea, Juma Ali Khatibu, alisema ingawa Serikali ya Umoja wa Kitaifa imefanikiwa kujenga umoja, lakini iimekwama katika suala la kuiondoa Zanzibar katika hali ngumu ya uchumi.
Alisema kupanda kinyemela kwa bei za mafuta, kumechochea kasi ya mfumuko wa bei za vyakula, kama vile mchele, unga wa ngano na sukari na kwamba hatua pekee ya kuondokana na tatizo hilo ni kuondoa kwa kodi katika bidhaa za vyakula.
Viwango vya bei katika soko la Zanzibar

Chanzo:TZMPAKAAU,IPPMEDIA

Keine Kommentare:

Kommentar veröffentlichen