Best Blogger TipsSoon

Donnerstag, 14. April 2011

TZMPAKAAU

Lowasa Chenge na Rostam sasa hali ni mbaya


Mwenyekiti wa CCM Jakaya Mrisho akiwa na mjumbe wa kamati kuu ya ccm NEC Edward Lowasa


Rais Jakaya Kikwete alipokuwa akimnadi Rostam Aziz kipindi cha uchaguzi uliopita



Mbunge wa bariadi Andrew Chenge

UNAWEZA kusema kwamba huu ni mwisho wa zama kwa Edward Lowassa, Rostam Aziz na Andrew Chenge ambao, juzi Jumatatu, chama chao kiliwatosa kwa kuwapa siku 90 kujiondoa katika nafasi walizonazo kwa vile wamekuwa wakichafua  haiba ya chama hicho.

Taarifa ya Chama cha Mapinduzi (CCM), iliyotolewa juzi usiku kwa vyombo vya habari, mjini Dodoma, imeeleza kwamba vikao vya juu vya chama hicho vinataka wanasiasa hao watatu wajiuzulu nafasi zao zote za uongozi katika Chama.

Chenge, Rostam, Lowassa wapime wenyewe
“Kama mlivyomsikia Mwenyekiti (Jakaya Kkwete) wale wote ambao wamekuwa wakituhumiwa kukichafua Chama, NEC imeamua watupishe.

“Uamuzi ni kwamba katika miezi mitatu wapime wenyewe, wajiondoe katika nafasi zao. Kama watakuwa hawajafanya hivyo katika miezi mitatu ijayo, hadi tutakapokutana hapa, basi chama kitawaondoa,” alisema John Chiligati, Katibu wa uenezi katika sekretariati iliyopita ambaye mabadiliko yaliyotangazwa juzi yamempa nafasi ya Naibu Katibu Mkuu wa CCM (Bara).

Chiligati, Malecela wapigilia msumari


Mzee John Malecela

Ni kana kwamba moto aliokuwa ameuwasha Jaji Werema jana yake ulirejewa na Chiligati ambaye akiwasilisha ripoti ya Sekretariati kuhusu tathmini ya hali ya siasa nchini na uchaguzi uliopita kwa Kamati Kuu, aliendeleza mwanzo wa mwisho wa safari ya Lowassa, Rostam na Chenge.
Akizungumza katika kikao cha Kamati Kuu cha kuandaa ajenda za NEC, Chiligati alieleza kwamba haiba ya chama hicho ilikuwa imechafuliwa kwa kiasi kikubwa na viongozi waliokuwa wakitajwa katika tuhuma za ufisadi.

Bila kutaja majina, Chiligati alisema kwamba tuhuma za kampuni ya kufua umeme ya Richmond ambayo baadaye ilizaa kampuni nyingine tata ya Dowans na kashfa ya ununuzi wa rada, wizi katika Benki Kuu wa kampuni hewa ya Kagoda ni kati ya mambo yaliyochangia sana katika kukinyima kura chama chao katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka jana na hivyo Sekretariati inapendekeza wahusika na tuhuma hizo wawajibike.

Taarifa zinasema wajumbe kadhaa walichangia katika ripoti hiyo. Waziri Mkuu wa zamani John Malecela akisema kwa maoni yake isingekuwa muafaka watoswe Lowassa, Rostam na Chenge tu huku ikijulikana kuwa Sekretariti, na hasa Katibu Mkuu, Yusuf Makamba, akiwa anahusika kwa matendo na kauli zake kukinyima chama kura.

Mwingine ambaye alipigilia msumari katika ‘jeneza’ la wanasiasa hao, ni Zakhia Meghji ambaye aliwahi kuwa Waziri wa Fedha na  yeye alimrushia makombora waziwazi Rostam akimtaja kuwa ni mhusika wa kampuni ya Kagoda na kwamba amekuwa akimchafua katika vyombo vya habari; huku akijua kufanya hivyo anaichafua CCM.

Meghji, ambaye ameingia tena katika Kamati Kuu, anaelezwa kueleza wazi kwamba Rostam anastahili kuchukuliwa hatua bila kuchelewa.

Makongoro Nyerere mwiba mkali

Mwenyekiti wa CCM Mara Makongoro nyerere a.k.a Mzee wa site

Lakini la kuvunda halina ubani, juzi ikiwa tayari Sekretariati na Kamati Kuu za zamani zikiwa zimejiuzulu, akichangia katika tathmini na mapendekezo ya Kamati Kuu ya kutaka Lowassa, Rostam na Chenge wawajibike, Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa Mara, Makongoro  Nyerere, alizungumza kwa hisia za mguso mkubwa akisema isingewezekana Lowassa, Rostam na Chenge kuendelea kuwa na nafasi za uongozi ndani ya chama.

Anasema mtoa habari wetu: “Kwanza alianza kwa kumwambia Mwenyekiti kwamba japo yeye ni Mwenyekiti wa Taifa, yeye (Makongoro)  naye ni Mwenyekiti wa Mara na kwamba NEC ndio waajiri wa Mwenyekiti Taifa.

“Akasema anapokaa Mwenyekiti wa Taifa ni mahala patakatifu, na kwa ajili hiyo pasingeweza kusogelewa na shetani, hata kama siku moja Mungu alipata kukutana na shetani barabarani.
“Akasema kule site (kwenye eneo la ujenzi ambako yeye ndiko anakoshinda akichanganya zege na kupiga bati) wanasema na wanataka watuhumiwa wote wa ufisadi watoke kwenye nafasi zao.
“Lowassa ni ndugu yangu. Sina matatizo naye. Najua ananipenda, nami nampenda. Lakini kule site wanasema hapana. Atoke. Tena nawe Mweyekiti ulipokwenda Monduli, ukainua mkono wake juu, ukasema hujapata kuona kama yeye (Lowassa), kule site wakauliza, sasa hii  ndiyo nini?

“Rostam simfahamu vizuri. Ninakotembelea yeye hawezi kuja na  mimi siwezi kwenda anakotembelea. Sina ugomvi naye. Lakini kule site wanasema naye hapana. Ulipokwenda Igunga ukamuamsha mkono ukasema ni kama timu ya mpira iliyokamilika watu kwenye site wakauliza sasa hii ndiyo nini?

“Nasikia Chenge wanamwita Mzee wa Vijisenti. Ni ndugu yangu. Sina hakika kama anavyo vijisenti kiasi hicho. Lakini kwenye site, si mimi, watu wanasema naye hapana.

“Ulikwenda pia Rombo, ukamuamsha mkono Mramba, kule kwenye site watu wakatuuliza hii  ni nini?, “ alikaririwa akisema Makongoro.

Mifano aliyoitaja Makongoro kwa kumhusisha Kikwete ilijitokeza wakati akiwa katika kampeni za Uchaguzi Mkuu wa 2010, katika majimbo ya Igunga alikokuwa akigombea ubunge Rostam, Rombo alikokuwa akigombea ubunge  Basili Mramba na Monduli alikogombea ubunge Lowassa.
Akiwa katika majimbo hayo, Kikwete aliwanadi viongozi hao waliokuwa wamepitishwa na chama chake kuwania ubunge, licha ya tuhuma za ufisadi zilizokuwa zikielekezwa kwao.

Sofia Simba awatetea, Kikwete amkejeli

Mwenyekiti wa UWT Sophia Simba


Na kama kawaida, Lowassa, Rostam na Chenge safari hii pia hawakukosa watetezi. Alisimama Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT) Sophia Simba ambaye akiungwa mkono na mjumbe mmoja kutoka Zanzibar, walitaka uletwe ushahidi wa tuhuma hizo, vinginevyo hayo yalikuwa ni maneno ambayo yasingeweza kufanyiwa kazi.

Hatua hiyo ya kina Sophia Simba kwa namna ilikejeliwa na Mwenyekiti Kikwete aliyechomekea ya kuwa ushahidi ulikuwa ni ushindi wake wa asilimia 61 mwaka 2010 badala ya asilimia 82 za mwaka 2005.
Msekwa, Kinana waongeza nguvu hoja


Mwenyekiti wa kampeni zilizopita za CCM bw.Abdurahman Kinana

Hatua hiyo ya Mwenyekiti Kikwete ilimsimamisha Makamu Mwenyekiti Pius Msekwa, ambaye pamoja na Abdulrahman Kinana walishiriki katika tume ya usuluhishi wa wabunge na viongozi wa CCM mwaka jana ambao kwa kiasi kikubwa ulikuwa umechangiwa na tuhuma za vigogo katika masuala kama Richmond, Dowans, Kagoda na ununuzi wa rada.

Bila kutafuna maneno, Msekwa alisema katika maoni yote waliyokusanya wakati wa usuluhishi, majina matatu yalikuwa yakipata maksi za juu. Na hayo ni ya Lowassa, Rostam na Chenge.
Wakati akitaja majina hayo, Chenge na Rostam ambao walikuwa wajumbe wa Kamati Kuu, walikuwa katika kikao hicho na walionekana kuduwaa.
Msekwa akasema hapakuhitajika ushahidi wa kipolisi kubaini kwamba watatu hao sasa walikuwa ni  mzigo kwa chama na hoja za kila mara kwa Upinzani na wakosoaji wa CCM, na kwa ajili hiyo wakitakiwa kuwajibika.

Taarifa zinasema kwamba huku upepo ukivuma vibaya kwa Lowassa, Rostam, Chenge na  Makamba ndani ya Kamati Kuu, alisimama Kinana.
Akasema kwamba matendo yote yaliyokuwa yakihusishwa na tuhuma za ufisadi yalifanyika mbele ya macho ya wajumbe wa Kamati Kuu.

Naye, kama Msekwa, akasema hakukuwa na haja ya kutafuta ushahidi kwa vile tayari nguvu ya umma ilikuwa inataka CCM ichukue hatua dhidi ya ufisadi na watuhumiwa wa ufisadi.
Akasema, kwa  maoni yake, Mwenyekiti wa CCM ambaye pia ni Rais wa Jamhuri, ana vyombo vikuu vya kumshauri viwili, Baraza la Mawaziri na Kamati Kuu.
Taarifa zinasema ni Kinana aliyependekeza Kamati Kuu ijiuzulu kwa kushindwa kumshauri vyema Mwenyekiti, uamuzi ambao kwa muda, ulionekana kuwa ulikuwa unawapunguzia joto na kuwalindia heshima Rostam na Chenge, lakini ambao ungewasilishwa kwenye NEC kupata baraka.

Kwa habari zaidi tembelea:www.raiamwema.co.tz
Vyanzo:TZMPAKAAU,Raia Mwema

Keine Kommentare:

Kommentar veröffentlichen