Best Blogger TipsSoon

Mittwoch, 1. August 2012

TZMPAKAAU

KIKWETE:MADAI YA WALIMU HAYATEKELEZEKI

Kushoto ni mwenyekiti wa chama cha walimu bwana Gratian Mkoba
Wakati mgomo wa walimu ukiendelea, Rais Jakaya Kikwete, amesema kuwa madai yao wanayoidai Serikali hayalipiki.

Akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari Ikulu, Dar es Salaam jana, Rais Kikwete alisema kuwa madai hayo kwa sasa hayatekelezeki na kuwaomba walimu kukaa katika mazungumzo na serikali ili kufikia mwafaka.

Alisema kuwa madai ya nyongeza ya mshahara kwa asilimia 100, posho ya kufundisha kwa walimu wa sayansi ya asilimia 55, asilimia 50 walimu wa sanaa na posho ya mazingira magumu ya asilimia 30 ya mshahara itafikisha fungu la mshahara kwa watumishi wa umma kuwa Sh. trilioni 6.874 kati ya mapato yote ya ndani ya serikali ya Sh trilioni 8.

"Si haki kulipa watumishi wa umma 500,000 kulipwa fedha hizo zote na kubakia na trlioni mbili tu. Hii inaweza kuleta mgogoro wa wananchi. Kuna watu milioni 43, nao watahoji," alisema Rais Kikwete.

Alisema hata kama wakilipwa mishahara hiyo hawatakuwa na kazi ya kufanya kwa sababu hakutakuwa na fedha za kugharimia mambo mengine.

“Madai haya ni magumu kuyatekeleza... sioni uwezekano huo,” alisisitiza Rais Kikwete.
Hata hivyo, alisema serikali inatambua mchango wa walimu pamoja na mawazo yao katika kuwalea na kuwafundisha watoto, hivyo aliwaomba wakae katika mazungumzo na serikali kutatua mgogoro huo.

CWT YAJA JUU

Wakati Rais Kikwete akitoa msimamo huo, Chama Cha Walimu Tanzania (CWT) kimelaani kitendo cha kukamatwa kwa baadhi ya walimu na viongozi wa chama hicho na serikali kuingilia uhuru wa Mahakama kwa kudai kuwa mgomo wao unaoendelea kote nchini ni batili.

Akizungumza na Waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Rais wa CWT, Gratian Mukoba, alisema chama hicho kimepokea kwa masikitiko kukamatwa kwa baadhi ya walimu na viongozi wake katika wilaya za Tarime, Rungwe, Kyela, Babati na mikoa ya Pwani, Morogoro na Ruvuma.

Alisema katika Mkoa wa Dar es Salaam, Mkuu wa Mkoa, Mecki Sadiki amewatishia wanachama na viongozi wao kwa kuamuru wakamatwe na kuidanganya jumuiya ya Watanzania kwa kuwaambia kuwa kiongozi wa CWT amewatangazia walimu wagome wakati yeye alikwenda kusaini kazini kwake na kuondoka.
Alisema kitendo alichokifanya mkuu huyo wa mkoa ni kitu cha  uzushi.

Aidha, Mkoba alisema mgomo wa walimu ni halali tofauti na serikali ilivyodai kupitia Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi,  Dk. Shukuru Kawambwa, aliyedai kuwa ni batili na kuitaka serikali kuacha kuingilia uhuru wa Mahakama.

Ametoa wito kwa walimu waendelea kubakia majumbani badala ya kwenda shuleni kwa kuwa wanasingiziwa kuwa wanawashinikiza wanafunzi kuandamana na kuitaka serikali kuwaachia huru walimu na viongozi wao waliokamatwa na kuwataka wakuu wa mikoa na wilaya kuacha kutumia madaraka yao kuwatisha.

Alisema serikali ikiwa sikivu chama hicho kiko tayari kukaa nayo meza moja ikiwa itakuwa na mapendekezo yenye tija badala ya kutoa vitisho kwa kutumia vyombo vya dola.
Vyanzo:TZMPAKAAU,Ippmedia na Dewjiblog


Keine Kommentare:

Kommentar veröffentlichen