Ingawa vyama vinane vimesimamisha wagombea, hadi sasa Chadema na CCM ndiwo wanaonekana kuchuana katika harakati za kunyakua jimbo hilo lililoachwa wazi na Jeremiah Sumari (CCM) aliyefariki Januari mwaka huu.
Vyama vingine vinavyoonekana kama wasindikizaji ni pamoja na TLP, Sau, AFP, UPDP, DP na NRA, huku vingine vikishindwa kufanya mikutano ya kampeni.
Miongoni na vijembe vilivyotawala jana ni pamoja na kauli ya Mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema), Joseph Mbilinyi
maarufu kama Mr. Sugu dhidi ya ombi la makada wa CCM la kutaka mgombea wao, Sioi Sumari, apewe ubunge ili kumfuta machozi kutokana na kufiwa na baba yake, Jeremiah Sumari ambaye alikuwa mbunge wa jimbo la Arumeru Mashariki.
maarufu kama Mr. Sugu dhidi ya ombi la makada wa CCM la kutaka mgombea wao, Sioi Sumari, apewe ubunge ili kumfuta machozi kutokana na kufiwa na baba yake, Jeremiah Sumari ambaye alikuwa mbunge wa jimbo la Arumeru Mashariki.
Akihutubia mkutano wa hadhara katika kijiji cha Nshapu Kata ya Nkoaranga, Sugu alikejeli ombi hilo na kusema kuwa ubunge hauwezi kumfuta mtu machozi.
Alisema: “Kama ingekuwa hivyo basi, Rais wa Tanzania leo angekuwa Madaraka Nyerere au Makongoro, maana nao ni wafiwa, tena baba yao tunamheshimu kwa kuwa alikuwa Baba wa Taifa.”
Sugu alirusha kijembe hicho kwa lengo la kumjibu Mbunge wa Mtera (CCM), Livingstone Lusinde, ambaye amekuwa akimwombea kura Sioi kwa kuwataka wananchi wamchague ili wamfute machozi kwa sababu amefiwa na baba yake.
Sugu alisema ameshangaa kusikia kuwa mgombea wa Chadema, Joshua Nassari, hivi sasa anasomesha watoto kadhaa ambao ni yatima ilhali yeye (Sugu), ameanza kuwasaidia watoto wa namna hiyo baada ya kuwa mbunge.
MBOWE: CHADEMA TULIENI, USHINDI WETU
Mwenyekiti wa CHADEMA taifa bw.Freeman Mbowe.
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, aliwataka wafuasi wa chama hicho kutulia na kutofanya fujo wala kuwazomea wafuasi wa CCM kwa kuwa anaamini kwamba Chadema imekwisha kushinda kwenye uchaguzi huo.Badala yake, aliwataka wananchi hao waombee uchaguzi huo pamoja na Nassari ili ushindi wa Chadema uwe ni wa haki ambao hauhitaji kumwaga damu.
Alisema wananchi wa jimbo hilo wanapaswa kutumia mikutano ya chama hicho kutafakari changamoto zinazowakabili, badala ya kuichukulia kama burudani kwa kuwa inalenga kuamua mustakabali wa maisha yao.
NASSARI AJIFANANISHA NA PAKA
Kushoto ni mgombea ubunge jimbo la Arumeru Mashariki Joshua Nassari.
Mgombea wa Chadema, Nassari, amejifananisha na paka kwa kuwataka wananchi wa jimbo hilo wamchague ili akatawanye panya ambao wapo kwenye Halmashauri ya Meru.
Akihutubia jana kwenye mikutano yake ya kampeni katika Kata za Leguruki, Nkoaranga, Akheri, Nkoarisambu, Songoro na Mbuguni, Nassari alisema Halmashauri ya Meru imekuwa ikitengewa mabilioni ya fedha za maendeleo kila mwaka, lakini hazijulikani zinakoelekea kwa kuwa huduma nyingi muhimu bado ni mbovu.
Alitoa mfano kwamba katika mwaka wa fedha wa 2011/12, halmashauri hiyo imetengewa Sh. bilioni 3.9 za miradi ya maendeleo, lakini hadi sasa mwaka unaelekea mwishoni na hakuna kilichofanyika.
“Bado mama zetu wanajifungulia sakafuni, hakuna maji, hakuna barabara, shule zetu hazina madawati na hampati taarifa za matumizi ya fedha...nitumeni mimi kama panya katika halmashauri ili nikalie ‘nyau’ hawa panya wanaotafuna fedha zetu watawanyike,” alisema.
Nassari huku akishangiliwa na umati wa watu waliokuwa wanamsikiliza, alisema imekuwa kawaida kwa wananchi wa Meru kutopewa hesabu za mapato na matumizi ya fedha zao, huku wakilazimishwa kuchangia miradi mbalimbali ambayo hata hivyo haikamiliki.
“Kila mwaka wadogo zangu wanapojiunga kidato cha kwanza wanaambiwa waende na madawati, mimi najiuliza kwani waliomaliza kidato cha nne wanaondoka na madawati yao?” alihoji na kuongeza “Wananchi wenzangu miradi mingi wala siyo ya kwenda kuidai Dar es Salaam, ni suala tu la kuingia Halmashauri na kuamua vipaumbele kwa sababu fedha zipo.”
Wakati huo huo, viongozi kadhaa wa CCM wamehamia Chadema akiwemo Mwenyekiti wa Mahakama wa Ardhi Kata ya Nkoaranga, Richard Mungure, pamoja na mabalozi kadhaa.
NCHEMBA: WAPINZANI NI WAROHO
Kulia ni Mwingulu Nchemba katibu uenezi wa CCM na kushoto ni mgombea ubunge kwa tiketi ya CCM bw. Sioi Sumari.
Meneja wa Kampeni wa CCM, Mwigulu Nchemba, amedai kuwa viongozi wengi wa vyama vya upinzani wana uchu wa madaraka.Alitoa kauli hiyo wakati akiwapokea wanachama waliodai kujitoa upinzani na kujiunga na CCM.
Aliwaambia wananchi waliohudhuria mkutano wa kampeni kuwa wanachama hao wamefanya jambo jema kujiunga na CCM.
Baadhi ya waliodai kujiunga na CCM ni kutoka TLP na Chadema.
Viongozi hao ni Katibu Mwenezi wa TLP Wilaya ya Arumeru, Agustino Kiungay na mhamasishaji wa Chadema wa Kata ya Sing’isi, Anna Sillas na wanachama 20 wa vyama hivyo.
WANNE WASHIKILIWA
Jeshi la Polisi linawashikilia vijana wanne wanaodaiwa kuwa wafuasi wa Chadema kwa madai ya kufanya vurugu katika mikutano ya CCM.
Kijana mmoja alikamatwa kwa madai ya kushambulia kwa mawe msafara wa mgombea wa CCM, Sioi, wakati ukielekea Kata ya Seela Sing’isi.
Vijana watatu ambao walikuwa wamevaa beji za Chadema waliupopoa kwa mawe msafara huo mita chache kutoka eneo la mkutano kabla ya mmoja wapo kushikiliwa kwa madai ya kuushambulia msafara huo kwa mawe ambayo yalikuwa yamehifadhiwa katika mfuko wa rambo.
Tukio hilo lilitokea jana saa 6:30 mchana ambapo wakati msafara huo ukielekea eneo la mkutano ghafla walijitokeza mbele ya msafara huo na kuanza kushambulia magari yaliyokuwa yametangulia mbele.
Tukio hilo lilizua purukushani wakati wa kushikiliwa kwa kijana huyo na baadaye wenzake wawili kukimbilia maeneo yasiyojulikana.
Mara baada ya kushikiliwa na vijana wa ulinzi wa CCM walimkabidhi kwa Polisi na kishakupandishwa ndani ya gari la polisi lenye namba PT 2065.
Mbunge wa Simanjiro (CCM), Christopher Ole Sendeka, alilaani kitendo hicho na kusema kwamba chama kilichowatuma kufanya kitendo hicho kimeishiwa sera za kuwaeleza wakazi wa jimbo hilo.
Katika tukio lingine, vijana watatu ambao walikuwa wakinyoosha alama ya vidole viwili inayotumia na Chadema walishikiliwa wakati mkutano wa kumnadi mgombea wa CCM ukiendelea katika uwanja wa Chama eneo la Seela Sing’isi.
Vijana hao waliokuwa wamesimama nyuma ya eneo la mkutano walishikiliwa na askari wa Jeshi la Polisi baada ya Medeye kutamka ya kwamba wanaoiunga mkono CCM wanyooshe mikono juu na ndipo wafuasi hao wakanyoosha alama ya vidole viwili.
Kamanda wa Polisi mkoani Arusha, Thobias Andengenye, alisema ofisi yake haijapokea taarifa kuhusiana na matukio hayo na kuhaidi kufuatilia.
Vyanzo:Ippmedia na TZMPAKAAU
Keine Kommentare:
Kommentar veröffentlichen