BIG SALARIES IS NOT THE PRIMARY ISSUE:MPs
Baadhi ya wabunge wa Bunge, wamesema uongozi wa umma sio fedha pekee na kwamba hawana mpango wa kuachana na siasa kutokana na kulipwa mshahara na posho kidogo.
Walitoa kauli hiyo walipozungumza na NIPASHE, kufuatia kauli ya Spika, Anne Makinda, kuwa nusu ya wabunge hivi sasa wanatamani kuachana na siasa na kwenda kufanya walizosomea kutokana na kulipwa mshahara mdogo pamoja na posho
Mbunge wa Sumve (CCM), Richard Ndasa, alisema wabunge hawakuchaguliwa kwa lengo la kwenda kupata mshahara mnono badala walipewa jukumu hilo ili kuwatumikia wananchi.
Alisema mbunge makini hawezi kutegemea mshahara na posho pekee na badala yake anatakiwa kufanya kazi zingine za ujasiliamali ili kujiingizia kipato.
Mbunge wa Serengeti (CCM), Dk. Kebwe Stephen Kebwe,, alisema hana mpango wowote wa kuachana na siasa kutokana na kipato kidogo na badala yake ataendelea kuwawakilisha wananchi wake kama kawaida.
Alisema alipoomba nafasi hiyo mwaka 2010 aliwaambia wananchi wamchague ili awawakilishe bungeni, lakini sio wamchague ili akapate utajiri kupitia mishahara na posho nono
Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Margareth Sitta, alisema kuna haja ya kumuuliza Spika Makinda ili aeleze alikopata takwimu kwamba nusu ya wabunge wanatamani kuachana na nafasi zao na kwenda kufanya kazi walizosomea.
“Mimi sina takwimu manake isije ikawa Spika alizungumza na wabunge wawili halafu akasema nusu ya wabunge wanatamani kuachana na ubunge kutokana na posho na mshahara mdogo,” alisema.
Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (Chadema), alisema hana uhakika kama kweli wabunge wametaka kujiuzulu kutokana na kulipwa kidogo.
Alisema kama kuna watu wanawaza hivyo hao sio wabunge na kwamba walipaswa kujiondoa muda mrefu kwa kuwa hawafai kuwawakilisha wananchi.
Vyanzo:TZMPAKAAU,Ippmedia na Globalpublishers
Keine Kommentare:
Kommentar veröffentlichen