Best Blogger TipsSoon

Freitag, 3. Juni 2011

TZMPAKAAU

  Zitto agusa penyewe na sasa wabunge wang´aka
  • Hoja yake ni kufutwa kwa posho za vikao kwa wabunge
Juzi Zitto ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema) na Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho, alisema haoni sababu mbunge kuendelea kulipwa posho nono kwa ajili ya kuhudhuria vikao kwa kuwa hiyo ni sehemu ya kazi yao ya kila siku.

Alisema anataka sheria ya Bunge inayotoa mwanya kwa wabunge kulipwa posho hizo ibadilishwe haraka ili kiasi hicho cha fedha kitumike kwa ajili ya kuwasaidia Watanzania wengine wenye matatizo.

Alisema mkutano wa Bunge la Bajeti unatarajiwa kuanza Juni 7, mwaka huu hadi Agosti 15, mwaka huu, kwa maana hiyo kutakuwa na siku za kazi 48 ambazo zitaigharimu serikali Sh. bilioni 3 kama posho ya vikao kwa wabunge .



Zitto Zuberi Kabwe mbunge wa kigoma kaskazini

Ukitaka kuona sura halisi za wabunge wa Tanzania gusa posho zao, huo ndio msimamo wao wa miaka na miaka na jana ulijidhihirisha kufuatia ushauri wa Waziri Kivuli wa Fedha, Zitto Kabwe, wa kutaka kufutwa kwa posho za vikao kwa wabunge katika bajeti ya serikali ya mwaka 2011/2012.

Jana baadhi ya wabunge hasa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), walipinga kwa nguvu zao zote mapendekezo ya Zitto ya kutaka posho za vikao wanazolipwa ziondolewe.
Mwenyekiti wa CCM bara Kapteni John Chiligati

Wa kwanza kupinga mapendekezo hayo bila hata kutafuna maneno alikuwa ni Mbunge wa Manyoni Mashariki (CCM), John Chiligati, ambaye alisema kama wabunge wa kambi ya upinzani hawataki kuzipokea fedha hizo waziache.Ikumbukwe kuwa huyu jamaa kama mwenyekiti wa CCM tanzania bara,Waziri na Mbunge anapata marupurupu ambayo hawezi hata kuyamaliza.

Mh.Mohammad Chomboh mbunge wa Magomeni Visiwani

Naye Mbunge wa Magomeni visiwani Zanzibar, Mohammad Chomboh (CCM), alisema suala hilo halitekeleziki kwa kuwa Sh. 80,000 anayolipwa mbunge kama posho ni ndogo ikilinganishwa na hali halisi ya maisha ilivyo sasa.

Alisema kulala nyumba ya wageni kwa siku wanapokuwa Dodoma ni Sh. 50,000 hapo bado hawajala hivyo kiasi hicho sio kikubwa kama inavyoelezwa na upinzani.

Mbunge wa Bukoba Vijijini, Jasson Rweikiza (CCM), alisema hoja ya kutaka posho ifutwe ni mawazo ya mtu kwani waliopanga malipo ya posho hiyo nao pia wana sababu zao.

Hata hivyo, alimtaka mbunge yeyote mwenye hoja kama hiyo, aipeleke bungeni ikajadiliwe huko, badala ya kuizungumzia nje ya Bunge.

Mbunge wa Nzega mjini daktari Hamisi Kingwalla

Mbunge wa Nzega (CCM), Dkt. Hamisi Kigwangalla, alisema haungi mkono hoja ya Zitto, kwa vile imejaa unafiki na kujitafutia umaarufu.

“Kama kweli tuna dhamira ya msingi ya kutumikia Watanzania kuna vitu vingi vilipaswa viondolewe na si posho peke yake. Kwa mfano, mashangingi yangefutwa kwa sababu yana gharama kubwa kuendesha.
Lakini yanahitajika kwa wabunge kutumia kuwafikia wananchi vijijini,” alisema Dk. Kigwangalla.
Alisema posho za vikao, ambazo Zitto anataka zifutwe, ni ndogo kulinganisha na majukumu yanayomkabili mbunge.

Dk. Kigwangalla alisema hata shida binafsi za wananchi, wanategemea zitatuliwe na mbunge, hivyo ni vigumu mbunge kufanya kazi bila kulipwa posho.
“Vinginevyo wanataka mbunge arudi mitaani kuganga njaa. Kwa hiyo, hiyo ni kauli ya unafiki, ya wanasiasa wanaotafuta umaarufu, mimi siwezi kuiunga mkono,” alisema Dk. Kigwangalla.

Akitoa maoni yake, Ali Khamis Seif mbunge wa jimbo la Mkoani (CUF), alisema hoja ya kutaka posho ziondolewe ni nzuri lakini kwa sasa bado sio wakati wake.

Alisema mbunge ana kazi nyingi za kuwasaidia wananchi hivyo ikiwa ataondolewa posho watashindwa kutatua kero mbalimbali za wananchi.

Hata hivyo alisema ikiwa fedha hizo zitaondolewa kwa mbunge ziingizwe kwenye mfuko wa jimbo ili zisaidie kusukuma mbele maendeleo ya wananchi.

Mh.Diana Chilolo

Akizungumzia hoja hiyo, mbunge wa viti maalum (CCM), Diana Chilolo, alisema Zitto ana mtazamo finyu juu ya hoja hiyo ya kutaka posho ya vikao iondolewe. Alisema fedha anayoipata mbunge sio ya kwake pekee bali inawasaidia wananchi wengine wakiwemo yatima, walemavu, wajane katika kupata mahitaji yao.

Kila anapokuwa mbunge wananchi wake wanamuona kama nguzo na kimbilio lao, hivyo posho hizo zinasaidia kutatua matatizo madogo madogo kama hayo.

Alitoa mfano kuwa kuna wabunge wengine wanatumia fedha hizo kuwasaidia wapiga kura wao kupata elimu pamoja na kupata matibabu kazi ambayo ingepaswa kufanywa na serikali.

Huyu jamaa ni Felix Mkosamali miaka 25 lakini hoja zake zina nguvu kama atomic bombs


Mbunge wa Muhambwe (NCCR-Mageuzi), Felix Mkosamali, aliunga mkono hoja ya Zitto ya kutaka wabunge wasiwe wanalipwa posho za vikao.

Mkosamali alisema si posho tu, bali anataka pia mishahara wanayolipwa wabunge pia ipungue na kuwa chini ya ile wanayolipwa hivi sasa kwani hatua hiyo itasaidia kudhibiti mafisadi kuwania ubunge.

“Hatuhitaji watu wagombee kwa ajili ya kupata posho, maana kuna watu huwa wanagombea kwa lengo la kutafuta maslahi binafsi na si kuwawakilisha Watanzania, hivyo posho ikiondolewa na mishahara ikapunguzwa waroho wa madaraka watapungua” alisema Mkosamali.

Aliongeza: “Kwa hiyo, naunga mkono hoja ya kufutwa posho. Lakini mishahara ya wabunge pia ipungue, maana haiwezekani posho zipungue wakati mishahara iko palepale,” alisema. Mkosamali alisema kufutwa kwa posho kwa wabunge ni hatua muhimu kwani kuna maeneo mengi ya kijamii, kama vile hospitali, fedha hizo zinaweza kupelekwa kusaidia.

Alisema pia kupunguzwa kwa mishahara ya wabunge, ni muhimu kwani kutasaidia kuwafanya wanaotaka kuwania ubunge, kufanya hivyo kwa lengo la kuwawakilisha wananchi kwa dhati.

Kulia ni mbunge wa kigoma kusini  kwa tiketi ya NCCR Mageuzi David Kafulila

Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila, naye pia aliunga mkono kufutwa kwa posho za vikao kwa wabunge, lakini alishauri posho hizo zibaki kwa vikao vya watumishi wasio na mishahara, kama vile wenyeviti wa vijiji.

“Mtumishi yeyote alipwe posho ya vikao, ambavyo sio sehemu ya majukumu yake,” alisema Kafulila.
Hata hivyo, alisema malipo ya posho za vikao, yasiishie tu kufutwa kwa wabunge, bali yafutwe serikalini na kwenye mahakama pia.

“Hatupaswi kulipwa kwa kukaa. Pesa nyingi inavuja. Mfumo wa sitting allowance (posho za vikao) must end (ikomeshwe),” alisema Kafulila.
Alisema pia posho nyingine zote zinapaswa kutozwa kodi na suala hilo liwe ni utaratibu na sera kwa mihimili yote ya dola; Bunge, Serikali na Mahakama.

Mbunge wa kilwa Kaskazini Murtaza Mangungu

Mbunge wa Kilwa Kaskazini (CCM), Murtaza Mangungu, aliunga mkono si kufutwa tu kwa posho za vikao kwa wabunge, bali hata mishahara nayo pia ifutwe akisema kazi ya ubunge haitakiwi malipo.
“Mimi maoni yangu ni kwamba, kwa kazi ya ubunge, wabunge hawapaswi kabisa kulipwa hata mshahara, ikifanyika hivyo itawafanya watu kujikita zaidi katika kuwatumikia wananchi,” alisema Mangungu.

Mh.Said Amour Arfi mbunge wa Mpanda Mjini

Kwa upande wake, mbunge wa Mpanda mjini (Chadema), Said Arfi aliunga mkono hoja hiyo ya Zitto na kusema kuwa umefika wakati wabunge kuwajali wananchi wenzao kwa kukubali kuachia posho zao ili ziweze kuwasaidia.
Aliwataka viongozi kupunguza anasa ili fedha hizo zisaidie watu wenye mahitaji ya lazima ikiwemo kuwapatia maendeleo.
Alisema mfumo unaotumiwa na Bunge wa kusema “ndiyoooo au hapanaaa” katika kupitisha hoja mbalimbali haufai kwa kuwa huo ni mfumo wa kijima.
Aliongeza kuwa hoja hiyo ya kutaka posho hizo ziondolewe inaweza kukwamishwa kwa kutumia mfumo huo wa upigaji kura kwa kusema ndiyo au hapana.

Vyanzo:Ippmedia,TZMPAKAAU

Keine Kommentare:

Kommentar veröffentlichen