Best Blogger TipsSoon

Freitag, 6. Mai 2011

Matembezi ya hisani ya kuchangia chakula mashuleni
  • Matembezi yatafanyika tar 29 Mei  Dodoma
  • Kawambwa:Tangu kuanzishwa kwa mpango huu wanafunzi 700,000 wamenufaika
  • Naye balozi wa WFP nchini asisitiza umuhimu wa Tanzania kuweza kujitegemea kwa chakula


Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa, amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi katika matembezi ya hisani ya uchangiaji wa chakula shuleni kupitia Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP).
Waziri Kawambwa, alitoa rai hiyo wakati akizindua mpango huo jijini Dar es Salaam jana. Matembezi hayo yatafanyika Mei 29, mwaka huu mjini Dodoma.
Alisema serikali imekuwa ikishirikiana kwa karibu na WFP katika matembezi mbalimbali yanayohusu uchangiaji wa chakula kwa takriban miaka 10 sasa.
Alisema tangu kuanzishwa kwa mpango huo, zaidi ya wanafunzi 700,000 kutoka shule 1,167 katika wilaya 16 kwenye mikoa ya Arusha, Manyara, Singida, Shinyanga na Dodoma, wamefaidika na mpango wa utoaji chakula shuleni ambapo ufaulu wa watoto hao umeongezeka.
"Tangu kuanzishwa kwa mpango huu, ufaulu wa wanafunzi umeongezeka kutoka asilimia 14 mwaka 2000 hadi asilimia 57 mwaka 2009," alisema.
Naye Balozi WFP nchini, Reginald Mengi, akimkaribisha mgeni rasmi alisema anafurahishwa na ongezeko la ufaulu wa wanafunzi nchini hasa baada ya mpango wa kutoa chakula mashuleni ambao umesababisha wanafunzi kusoma kwa bidii na kupanua uelewa wao.
"Mwanafunzi anapokuwa shuleni akiwa na njaa, ni vigumu kumsikiliza mwalimu kwa makini kwani muda wote anawaza chakula, hivyo kupoteza umakini katika masomo yake na kiwango chake cha kufaulu kushuka," alisema Mengi.
Aliongeza kuwa taifa ambalo haliwezi kujilisha lenyewe, haliwezi kuwa huru hivyo aliiomba serikali kuhakikisha inajenga mazingira mazuri ya upatikanaji na uhifadhi wa chakula pamoja na kutoa chakula wakati maafa yanapotokea ili kujenga taifa huru lenye watu wenye elimu na afya bora.
Alipoulizwa wana mikakati gani katika kuendeleza mpango huo, Mengi alijibu: "Ni vizuri tufikirie jinsi gani ya kuwa na mipango mizuri ya kuhakikisha tunazalisha chakula cha kutosha ili siku moja tuondokane na tatizo la chakula nchini badala ya kupanga kuwa na matembezi kila mwaka."
Naye Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Betty Mkwasa, alisema matembezi hayo yatafanyika kwa mara ya saba hivyo anafarijika matembezi hayo kufanyikia mkoani kwake. Matembezi hayo yamelenga kuchangia chakula katika shule mbalimbali nchini.

Vyanzo:Ippmedia,TZMPAKAAU

Keine Kommentare:

Kommentar veröffentlichen