Best Blogger TipsSoon

Mittwoch, 27. April 2011

TZMPAKAAU

HAKUNA KHERI PASIPO MUUNGANO


Inasemekana  Baba wa Taifa hapa alikuwa akichanganya udongo ule wa
kutoka Tanganyika na ule wa kutoka Zanzibar kama ishara ya kuasisiwa kwa
Jamhuri ya Muungano Tanzania


Viongozi mbalimbali pamoja na wanasiasa wamesema endapo Watanzania wataamua kuvunja Muungano wa Tanganyika na Zanzibar watajuta maisha yao, kwa vile umesaidia kujenga misingi ya udugu, umoja wa kitaifa na amani kwa wananchi wake.

Wakizungumza katika maadhimisho ya miaka 47 ya Muungano jana, Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Prof. Ibrahim Lipumba, alisema ni jambo la hatari kwa Watanzania kufikiria kuuvunja muungano bila ya kuangalia faida na changamoto zake.
Mwenyekiti wa CUF Ibrahim Lipumba

“Watanzania watajuta maisha, iwapo wataamua kuvunja muungano bila ya kuangalia faida zilizopatikana tangu kuasisiwa kwake, ni jambo lililo wazi asilimia 75 ya Watanzania wamezaliwa baada ya kuundwa kwa muungano, hivyo ni wajibu wao kuulea na kuudumisha” alisema Prof. Lipumba.
Aidha, alisema kwamba zaidi ya Wazanzibari 400,000 wanaishi Tanzania Bara, kama ilivyo kwa wananchi wa Tanzania Bara wanaoishi Zanzibar na kutaka wananchi kutumia mjadala wa katiba mpya ili uwe msingi wa kuimarisha muungano badala ya kuuvunja.

Naye Muasisi wa Mapinduzi ya Zanzibar na Mjumbe wa Baraza la kwanza la mapinduzi hayo, Hamid Ameir, alisema wanaopinga muungano hawafahamu msingi wake kwa vile idadi kubwa ni vijana ambao hawakushuhudia maisha ya Waafrika kabla ya ukombozi uliomaliza utawala wa kikoloni.

Mama Fatma Karume akisalimiana na Jenerali Davis

Kwa upande wake, Mke wa Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Mama Fatma Karume, alisema Muungano wa Tanganyika na Zanzibar umeleta faida kubwa kwa pande zote mbili, kwa vile shabaha iliyolengwa na waasisi wake imefanikisha kujenga udugu, umoja na kudumisha amani na usalama wa nchi.

Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa DK.H.Mwinyi

Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk.Hussein Mwinyi, alisema hakuna muungano usiokuwa na kasoro, na jambo la msingi kwa wananchi kudumisha muungano wakati serikali zikiendelea na mchakato wa kutatua kasoro zilizopo kupitia taratibu maalum zilizopo.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano), Samia Suluhu Hassan, alisema kwamba hana uhakika kama kuna mambo yaliingizwa kinyemela katika orodha ya mambo ya muungano kama inavyodaiwa na baadhi ya wanasiasa wa Zanzibar.
Balozi Ali Abeid Karume

Naye Balozi wa Tanzania nchini Italy, Ali Abeid Karume, alisema endapo Wazanzibari na Watanzania Bara wangekuwa hawautaki muungano kama inavyodaiwa na baadhi ya watu, usingefikia miaka 47 tangu ulipoasisiwa mwaka 1964.

Mwisho ni Hotuba fupi ya Mwalimu Nyerere kuhusu Muungano
  •  What he said  applies for people of mainland same wise to those of islands he said this in his long speech but bad luck i didnot find the whole stuff




Vyanzo:TZMPAKAAU,Nipashe

Keine Kommentare:

Kommentar veröffentlichen