Best Blogger TipsSoon

Dienstag, 15. März 2011

TZMPAKAAU

Babu  wa loliondo azidi kuwa gumzo
  • Ndesamburo  kuwapeleka mamia ya watu kwa babu bure
  • Asema kwa wanaotaka kutumia helkopta yake bei ni dola 1000 za marekani
Picha za kwa babu leo

Unawezajionea foleni hamna tofauti na foleni ya mwenge


Babu akiwajibika kwa moyo mkunjufu kutoa dozi,
 huku ulinzi ukiwa umeimarishwa.

Ili ufike kwa babu kwa urahisi Landrover 109 au 110
ni muhimu, kama huamini jaribu kufika huko na chaser yako

Kwa Babu, shusha!!!......hii ni stendi ya kwa Babu

mmoja kati ya wajasiria mali wengi wanaojishughulisha kwa njia moja au nyengine kuwahudumia wagonjwa waliofika kwa mchungaji Mwaisapile....Hee ila mi sijawezajua hii ni nyama ya nini kwa haraka, ila inavutia kiaina.

Mamia ya wakazi wa Manispaa ya Moshi na vitongoji vyake jana walijitokeza na kujiorodhesha kwenda kupatiwa matibabu kwa Mchungaji mstaafu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Ambilikile Mwasapile, katika kijiji cha Samunge, Loliondo wilayani Ngorongoro, baada ya Mbunge wa Moshi Mjini Philemon Ndesamburo (Chadema), kutoa usafiri wa bure kwenda na kurudi kwa watu wasio na uwezo wa kujigharimia.
Jana umati mkubwa wa watu ulifurika katika ofisi za mbunge huyo zilizopo mjini Moshi wakijihorodhesha majina yao huku wakiwa na vyeti vyao vya hospitali mbalimbali kwa ajili ya kwenda Loliondo kupata tiba ya magonjwa sugu inayotolewa na Mchungaji Mwasapile.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa, Ndesamburo alisema kuwa ameamua kutoa usafiri wa bure kwa wagonjwa wasiokuwa na uwezo wa kujigharimia usafiri wa kwenda na kurudi kwa kutumia magari mawili yatakayokuwa yanabeba watu 73.
“Japo ni siri kujua magonjwa ya mgonjwa, lakini wagonjwa wanatakiwa kujitokeza na vyeti vyao na wapo wengi wamejitokeza tena wakiwa ni mtu na mke wake na saa nyingine wanakuja hadi na watoto wao na wanajiandikisha majina yao kwa madiwani wao hapo nje kwenda kwa ‘Babu’,” alisema Ndesamburo.
Ndesamburo alitoa wito kwa wabunge wengine kujitolea kuwasaidia wananchi wao wasiokuwa na uwezo kwenda kupatiwa dawa ambayo inaelezewa na wananchi wengi kuwa imekuwa msaada mkubwa kwao na kuwa wana imani nayo.
Alisema wananchi watalazimika kujilipia fedha za kujikimu mahitaji yao kama malazi, chakula, vinywaji na Sh. 500 kwa ajili ya sadaka ya kwa Mchungaji Mwaipesile.
Mbunge huyo alisema kuwa watu watakaohitaji kutumia usafiri wa helkopta yake watalazimika kuchangia Dola za Marekani 1,000.

Alisema usafiri wa helkopta utakuwa unatumika mara nne kwa siku na kuwa kituo kikuu cha helkopta hiyo kitakuwa jijini Arusha na kwamba zoezi la usafiri wa magari na helkopta litadumu kwa zaidi ya miezi miwili hadi hapo hali ya barabara itakapokuwa nzuri.
“Kwa muda wa wiki moja sasa usafiri wa helkopta hauna nafasi, zimejaa itabidi wananchi wajiorodheshe mapema wanaotaka kutumia usafiri huo licha ya kwamba wanapaswa kuchangia gharama kidogo,” alisema Ndesamburo.
Alisema wagonjwa wengi wanaojitokeza tena wakiwa na vyeti vyao wengi wanaugua magonjwa ya ukimwi, kisukari na kansa.
Alisema kuna wananchi wanaosumbuliwa na magonjwa sugu wanaoshindwa kutoka ndani na kubaki wakiugulia ndani na kwamba anaandaa utaratibu wa kuwasafirisha wagonjwa hao kwa kuwa hivi sasa hali ya usafiri ni vigumu kumsafirisha mtu asiyeweza kujimudu.
Ndesamburo alisema hali ya hewa inaonyesha kuwa baada ya muda mvua zitaanza kunyesha hivyo magari yatashindwa kufika huko kutokana na ubovu wa barabara.
Hata hivyo, alisema magari aliyotoa yanaweza kumudu hali hiyo na kufika Loliondo na kurejea salama kwa kuwa ni magari maalum kwa ajili ya safari za mbugani.
Wakati huo huo, baadhi ya wananchi waliopatiwa matibabu na Mwaisapile, wamezungumzia maendeleo ya afya zao.
Wakizungumza na NIPASHE wananchi hao ambao baadhi yao walikuwa wanaendelea na shughuli zao kama kawaida, wamesema kadiri muda unavyokwenda kumekuwepo na mabadiliko ya afya zao tofauti na ilivyokuwa kabla ya kutumia dawa hizo.
Hata hivyo wananchi wengi waliotoa ushuhuda wa kuwepo kwa mabadiliko ya afya zao ni wale wanaosumbuliwa na magonjwa ya sukari na shinikizo la damu na wengi wao wametoa maelezo kwa masharti ya kutokuwa tayari kupigwa picha wala kutajwa majina yao, hakuna shuhuda aliyethibitisha kuwa amepona ukimwi.
Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, Elias Wawalali na Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Raymond Mushi, wamesema kadiri siku zinavyokwenda hali ya utoaji huduma imeendelea kuwa nzuri na wameendelea kuwaomba wadau wengine wakiwemo wasafirishaji kusaidia kupunguza changamoto zilizopo.
Mushi alisema kwa sasa hakuna tena msongamano katika eneo hilo na kwamba wagonjwa wote waliofika kwa Mchungaji Mwaisapile jana walikunywa dawa na kuondoka muda huo huo.
Kuhusu suala la uboreshaji wa miundombinu ikiwemo vyoo, Mushi alisema jitihada zinaendelea.
Kuhusu barabara, Mushi alisema suala hilo bado ni gumu.
Vyanzo:Nipashe,issamichuzi.blogspot.com,TZMPAKAAU

Keine Kommentare:

Kommentar veröffentlichen