ajenda zikiwa
- Kupinga malipo ya serikali kwa Dowans
- Kuishinikiza serikali kudhibiti mfumko wa bei
- Kupinga matokeo yaliyomuweka meya wa Arusha madarakani
Moto uliowashwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) jijini Mwanza juzi, leo utahamia mjini Musoma ambako yatafanyika maandamano makubwa na kufuatiwa na mkutano wa hadhara kuishinikiza serikali isiilipe Kampuni ya Dowans mabilioni ya Shilingi na kupinga kupanda kwa gharama za maisha.
Juzi, Chadema kilifanya maandamano yaliyoliteka Jiji la Mwanza na kuhudhuriwa na maelfu ya wakazi wake kwa madhumuni hayo.
Maandamano ya leo katika Manispaa ya Musoma yataongozwa na viongozi wa juu wa chama hicho na kuhitimishwa na mkutano mkubwa utakaofanyikia katika viwanja vya Shule ya Msingi ya Mukendo.
Maandamano hayo pamoja na kushirikisha karibu wabunge wote wa chama hicho, pia yatawashirikisha Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho, Freeman Mbowe na Katibu Mkuu, Dk. Wilibrod Slaa.
Mkurugenzi wa Idara ya Utafiti na Sera wa Taifa wa chama hicho, ambaye ni mratibu wa maandamano na shughuli zote za mikutano ya Operesheni Sangara mkoani Mara, Mwita Mwikwabe Waitara, aliliambia NIPASHE jana kuwa tayari Jeshi la Polisi limeyabariki maandamano hayo ya amani na mikutano katika maeneo mbalimbali ya mkoa wa Mara.
“Jana (juzi) katika kikao chetu na Kamanda wa Polisi wa Mkoa (RPC), Mkuu wa Polisi wa Wilaya (OCD) na Mkuu wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) mkoa, tulikubaliana njia za kupita maandamano hayo,” alisema Waitara.
Alisema maandamano hayo yataanzia eneo la Bwiri kisha kupita barabara ya Nyerere, Shabani, Mukendo, Kusaga na kurudi barabara ya Nyerere na kuingia uwanja wa Mukendo,” alisema Waitara.
Aidha, Waitara aliwaomba wananchi kuwasili katika eneo la Bweri majira ya saa 3:00 asubuhi na kwamba maandano hayo yanatarajia kuanza saa 5:00 na kufuatiwa na mkutano ambao utahutubiwa viongozi mbalimbali wa chama hicho.
Alisema miongoni mwa ajenda za mkutano huo ni kuhusu kupinga Tanesco kuilipa Dowans Sh. bilioni 94, uchaguzi wa Meya wa Jiji la Arusha ambao ulisababisha kutokea kwa mauji ya watu watatu, kuitaka serikali kudhibiti mfumuko wa bei katika bidhaa mbalimbali nchini na suala la kuandikwa kwa katiba mpya ya nchi.
Hata hivyo, Waitara alisema baada ya mkutano huo wa leo, kesho viongozi wa chama hicho watagawanyika katika makundi sita kwa ajili ya kufanya mikutano kadhaa katika majimbo yote ya uchaguzi ya Mkoa wa Mara.
Alisema awali, Chadema kiliomba pamoja na njia hizo pia kutumia njia za Nyasho, Majita na Uhamiaji, lakini walishauriana na polisi kusitisha njia hizo tatu kutokana na ufinyu wa barabara ili kuondoa msongamano kwa wananchi wengine.
Alisema kuanzia Jumatatu hadi Jumanne, mikutano na maandamano wengine itafanyika mkoani Shinyanga na Machi 3, 2011 timu ya viongozi wa Chadema itakuwa mkoani Kagera na baadaye kutembelea mikoa ya kanda nyingine.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mara, Robet Boaz, alisema Jeshi la Polisi limeruhusu kufanyika kwa maandamano hayo ya amani na mikutano hiyo.
Chanzo:Nipashe
Keine Kommentare:
Kommentar veröffentlichen