Best Blogger TipsSoon

Sonntag, 1. Juli 2012

TZMPAKAAU

Dkt Stephen Ulimboka  apelekwa nje ya nchi(Dkt Stephen Ulimboka who was badly wounded last week has been transferred abroad for further treatmet)
Hatimaye Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari nchini, Dk. Steven Ulimboka amesafirishwa jana, kwenda
nchini Afrika Kusini kwa matibabu zaidi baada ya baadhi ya vipimo kukosekana nchini.
Dk. Ulimboka alisafirishwa jana kwa ndege ambayo haikuwekwa bayana ni ya shirika gani iliyoondoka saa 10:30 jioni kwenye uwanja wa Kimataifa wa Julius Nyerere, chini ya ulinzi mkali wa madaktari .
Atakapowasili kwenye hospitali aliyopangiwa, miongoni mwa vipimo atakavyofanyiwa ni "Toxicology" ambacho hutumika kuangalia sumu mwilini.
Dk. Ulimboka aliondoka jana saa 6:15 mchana kutoka wodi ya Taasisi ya Mifupa Muhimbili (Moi) na gari la kubeba wagonjwa la hospitali binafsi ya AAR lenye namba za usajili T 151 AVD na kupelekwa kwenye jengo la watoto lililopo Muhimbili kwa ajili ya kuwekewa mashine ya 'Dialisis' ambayo hutoa ama kuchuja taka/sumu mwilini. Kwa kawaida kazi hii hufanywa na figo.
Wakati anaondolewa wodini na kuingizwa kwenye gari hilo, milango mikuu ya kuingilia Moi ilifungwa na kutoruhusu mtu yeyote isipokuwa madaktari.
Pamoja na kuwepo kwa mazingira ya kulinda usalama wa Dk. Ulimboka dhidi ya wabaya wake, waandishi wa habari waliokuwa wamekaa nje ya lango hilo baada ya kuzuiwa kuingia walifanikiwa kupiga picha gari la wagonjwa bila kujua kama ndilo lililombeba au la.
Dakika kumi baada ya gari hilo kutoka, jopo la madaktari waliokuwa wakimshughulikia lilitoka bila kuzungumza chochote na waandishi na kuelekea eneo lililopo jengo la kuhifadhia maiti ndani ya hospitali hiyo.
Kutokana na hali hiyo waandishi wa habari waliendelea kukaa eneo hilo huku wakiwa wametegesha kamera zao wakisubiri mgonjwa huyo atolewe kutoka kwenye gari huku gari lingine la wagonjwa kubaki ndani ya jengo hilo.
Lakini daktari mmoja alifika hapo na kuwataarifu waandishi kuwa, tayari mgonjwa ameshatolewa na wakati huo alikuwa jengo la watoto kwa ajili ya kuwekewa mashine hiyo kwa ajili ya kuanza safari ya kuelekea Uwanja wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere kwa safari.
Hata hivyo, magari ya waandishi wa habari, ndugu wa Dk Ulimboka pamoja na costa mbili za madaktari zilizokuwa zimekodishwa kwa ajili ya kumsindikiza mwenzao uwanja wa ndege, yalikwama kwenye foleni kubwa iliyokuwa barabara ya Mandela na kusababisha kukaa hapo kwa muda wa saa nzima na kushindwa kumuona daktari huyo wakati akiondoka.
Kutokana na hali hiyo, madaktari hao waliungana na wanaharakati waliokuwa wamefika eneo hilo kubeba mabango yaliyokuwa na ujumbe tofauti kwa serikali na kuanza kuimba nyimbo zilizokuwa na ujumbe wa kuunga mkono juhudi za Dk. Ulimboka.
Wanaharakati hao ni pamoja na Mkurugenzi wa Chama cha Wanahabari Wanawake nchini (Tamwa), Ananilea Nkya na Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Haki za Binadamu, Dk Hellen Kidjo -Bisimba.
Baadhi ya mabango hayo yalisomeka "Serikali kama Muhimbili kungekuwa na dawa Dk. Ulimboka angetibiwa na madaktari wenzake".
"Madaktari wamegoma kwa sababu hospitali za serikali hazina vitendea kazi, wananchi wanapoteza maisha bila huruma".
"Rais Kikwete ahadi yako ya mgomo wa madaktari kuwa historia hapa Tanzania imeishia wapi tekeleza ahadi yako", "Hata mkituua utetezi utaendelea", "bilioni 200 za kuagiza madaktari nje ya nchi zinatosha kuboresha huduma za afya na kumaliza mgomo wa madaktari" na "Tunadai bajeti ya afya ifikie asilimia 15 kama utekelezaji wa azimio la Abuja".
Akizungumza na waandishi wa habari nje ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere, Katibu wa Jumuiya ya Madaktari nchini, Dk. Edwin Chitage, alisema kwamba sababu kubwa ya kumpeleka mgonjwa wao nje ya nchi imetokana na vipimo anavyotakiwa kufanyiwa kukosekana nchini.
Aliongeza kuwa, hali ya Dk. Ulimbona ilibadilika toka juzi na kwamba, figo zake hazifanyi kazi vizuri.
“Kuna aina ya vipimo anatapaswa kufanyiwa na hospitali zetu zote hazina vipimo hivyo, kwa kweli mwenzetu yupo katika hali mbaya anaumwa sana, kundi aliloondoka nalo leo ni pamoja na madaktari bingwa,” alisema.
Kuhusu nini kinafuata baada ya mwenzao kwenda nje kwa matibabu, Dk. Chitage alisema kuwa, wakati wowote kuanzia sasa watatoa tamko lao na kueleza kuwa mgomo bado unaendelea.
Aliitaka serikali itoe tamko dhidi ya hofu waliyonayo kuhusu maisha ya madaktari hasa kutokana na unyama aliofanyiwa mwenzao.
Hata hivyo, hakuwa tayari kutaja nchi anayopelekwa Dk. Ulimboka na kueleza kuwa, familia yake ndiyo itakayoeleza hilo ambapo hata ndugu zake walipoulizwa hawakuwa tayari kuitaja kwa madai kuwa ni kwa ajili ya usalama wa ndugu yao.
Alishukuru mwitikio mkubwa wa watu waliojitokeza kutoa michango yao ili kumwezesha mwenzao kwenda nje ya nchi na kueleza kuwa, taarifa za fedha hizo zitatolewa ili kuwepo na uwazi.
Miongoni mwa waliofika asubuhi kumjulia hali Dk. Ulimboka kabla ya kusafirishwa ni pamoja na Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Wilson Mkama na Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheli Tanzania (KKKT), Dk. Alex Malasusa.
Vyanzo:Ippmedia na TZMPAKAAU 

Keine Kommentare:

Kommentar veröffentlichen