Best Blogger TipsSoon

Sonntag, 10. Juni 2012

TZMPAKAAU

MAWAZIRI WA CCM WANG'AKA
Chama cha Mapinduzi (CCM), kimetumia mtaji wa mawaziri wake watano kujibu mapigo ya Chama cha Chadema Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema),
kwa kuzitolea ufafanuzi kero mbalimbali zinazilikabili Jiji la Dar es Salaam na taifa na namna ya kuzipatia ufumbuzi.
Ikiwa ni wiki mbili baada ya Chadema kutoka mashambulizi kwa serikali, mawaziri hao wamejitokeza kujibu mapigo katika mkutano wa hadhara ulioandaliwa na CCM kwenye viwanja vya Jangwani jijini Dar es Salaam, eneo ambalo Chadema walilitumia kurusha mashambulizi hayo na kuzindua mpango wao ujulikanao kama Movement for change (M4C).
Waziri wa Usafirishaji na Uchukuzi Dk.Harrison Mwakyembe
Akizungumza kwenye mkutano huo, Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, alisema moja ya kero inayolikabili jiji la Dar es Salaam ni jeuri ya baadhi ya wamiliki na wafanyakazi wa daladala ambao hupandisha nauli bila kufuata utaratibu uliowekwa na serikali.
Dk. Mwakyembe alisema wiki mbili zilizopita, taasisi iliyo chini ya wizara yake, Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (Sumatra) walikamata daladala 19 kwa kuongeza nauli kinyume cha sheria.
“Katika kujiridhisha nikasema siwezi kwenda Bungeni nikaacha hali ya Dar es Salaam ni mbaya kwa upande wa nauli, nikapanda daladala kutoka Mwenge kwenda Tegeta na Tegeta kwenda Bunju, badala ya nauli ya Sh. 500 kutoka Mwenge kwenda Tegeta nikatozwa Sh. 1000, kutoka Tegeta mpaka Bunju nilitozwa sh. 1,500, huku ni kuwaumiza wananchi na kuchezea sheria za nchi,” alisema Dk. Mwakyembe.
Alisema watu wanapandisha nauli utadhani wizara yake haipo, na kuahidi kuwashukia wamiliki wa daladala na kwamba watakosa mahali pa kukimbilia na atalazimika kuchelewa kwenda bungeni ili kuhakikisha kero hii inapatiwa ufumbuzi haraka.
Waziri Mwakyembe alisema hakuna sababu ya watu kupandisha nauli ovyo ovyo kama vile serikali imekwenda likizo wakati upo utaratibu wa kisheria wa kufanya hivyo.
“Na sio huko tu kwenye daladala na wengine wote wanaopandisha nauli ovyo kwa kisingizio cha gharama zimepanda, kuna utaratibu wa kisheria kupandisha gharama, kama una maombi yako peleka Sumatra, Sumatra wataitisha mkutano wa wadau, watajadiliana itarudi kwetu, tutaliangalia kama kweli gharama zimepanda halafu tutatoa bei elekezi, sio kila mtu kujiamulia tu, hii ni serikali,” alisema Dk. Mwakyemba.
Dk. Mwakyembe ambaye alikuwa kivutio kwenye mkutano huo kutokana na msimamo wake, alitumia fursa hiyo kutoa namba yake ya simu ya mkononi ya 0782 242526 akiwataka wananchi wampigie wakati wowote wanapoona daladala inawadhulumu kwa kuwatoza nauli kubwa ambayo haipo kisheria.
Akizungumzia tatizo la msongamano wa magari katika jiji la Dar es Salaam, alisema foleni zilizopo kimsingi zinaua uchumi wa nchi hasa ikizingatiwa kwamba mkoa wa Dar es Salaam ndio tegemeo la kiuchumi nchini.
Alisema katika kukabiliana na kero hiyo, wizara yake imejipanga katika mwezi mmoja ujao kuanzisha usafiri wa treni wa Tazara kutoka Mwakanga hadi Kurasini kila asubuhi na kutoka Ubungo Maziwa hadi Stesheni, ambapo wataalamu wake wamemuambia huduma hizo zitabeba zaidi ya abiria 9,600 kwa mkupuo.
Aidha alisema wakati anaingia wizarani alikuta wawekezaji wanaotaka kuendesha huduma ya treni, lakini amewapiga ‘stop’ na kwamba kazi hiyo itafanywa na Watanzania wenyewe kupitia serikali yao.
Makao makuu ya bandari ya Dar Es Salaam 
Kuhusu Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), alisema haja ridhika kabisa na utendaji kazi wa mamlaka hiyo na amewapa muda wajiandae kabla hajafanya ziara rasmi kwani anazo taarifa kuwa wafanyakazi wake wamegeuka wafanyakazi wa ‘super market’ ya kuuza 'spare parts' ya magari kutoka nje.
Dk.Mwakyembe alisema watendaji wote wanaofanya biashara hiyo atawashughulikia kwa kuwang’oa hata kama wanajiona ni wakubwa kuliko mti wa Mbuyu.
“Nawakumbusha wenzangu wa bandari ya Dar es Salaam ambayo inatakiwa kuwa sifa na kioo cha Tanzania, mimi sijaridhika nayo kabisa na nimefanya makusudi sijaenda kuwatembelea pale, nataka wajipange sawasawa wasije wakanilaumu mbele ya safari,” alisema huku akishangiliwa na umati wa mashabiki na wanachama wa CCM.
Alisema Tanzania haiwezi kuwa nchi iliyopewa fursa na Mungu kuweza kuwa na lango kuu la nchi sita zinazohitaji huduma hapa lakini nchi hizo zinaikimbia Tanzania kwa sababu ya upuuzi unaofanywa na baadhi ya watendaji wa bandari hiyo.
Dk.Mwakyembe aliwaomba wananchi katika kipindi atakachokuwa katika wizara hiyo hatua atakazokuwa anazichukua dhidi ya watendaji wasiowaaminifu wasiwe wanalalamika na kwamba atatumia miezi mitatu kusafisha uozo uliopo katika wizara na taasisi zake.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Steven Wasira
Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mahusiano na Uratibu, Steven Wasira, alianza kwa kuwashangaa watu wanaosema kuwa serikali ya CCM haijafanya kitu kwa Watanzania tangu wakati wa uhuru.
Alisema suala la kupanda kwa bei za vitu kama mafuta, si la CCM kwani linaanzia nchi za Uarabuni ambako mafuta hutoka huko na kulifanya tatizo hilo la kidunia zaidi.
“Wapo watu wanasema hili tatizo la ugumu wa maisha ndiyo sera ya CCM lakini tujiulize kwani mafuta yakipanda bei Uarabuni, je! CCM iko Uarabuni? Alihoji Wasira na kuongeza kuwa serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali katika kukabiliana na hali hiyo.
Alisema wanaolalamikia suala la ugumu wa maisha ni kwasababu tu hawajui kwani Tanzania huwezi ukalinganisha na nchi ambazo zipo katika kundi la G8 ambazo uchumi wake upo juu.
Wasira alisema hata hivyo zipo hatua kadhaa zinazochukuliwa na serikali ambapo miongoni mwa hatua hizo ni kuwekeza kwenye kilimo cha mabonde ya Kilombero ambako hekta 100,000 zimetengwa kwa ajili ya kilimo cha mpunga.
Kuhusu kukabiliana na tatizo la kupanda kwa bei ya sukari nchini, alisema katika bajeti ya mwaka huu serikalini imeainisha mabonde ya Kilombero, Rufiji, Wami, Maragarasi na Kagera kwa ajili ya kujenga viwanda vya kuzalisha sukari.
Tatizo la kupanda kwa gharama za umeme, Waziri huyo alisema kuanzia mwezi Julai mwaka huu kutajengwa bomba la gesi kutoka Mtwara hadi Dare s Salaam ambapo gesi hiyo itatumika kwa ajili ya kuzalisha umeme na hivyo kupunguza gharama ya nishati hiyo kutoka dola senti 42 hadi kufikia dola senti saba za Marekani.
Alisema watu wanaosema kuwa serikali ya CCM haiwajali wananchi wake na haina lolote inachowafanyia, ni sawa na kufuru.
“Nataka kumpa ujumbe Mbowe (Mwenyekiti wa Chadema) anapo sema hatujafanya lolote anamkufuru baba yake mzazi aliyedai uhuru na Mwalimu Nyerere, namsihi asije akapata laana kwa kauli zake hizo,” alisema Waziri.
Waziri wa Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi
Kwa upande wake, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, alikiri kuwepo kwa kero nyingi kwenye sekta ya ardhi na kwamba ufumbuzi wa kero hizo umekuwa ukifanywa kwa kuzingatia sheria za nchi zilizopo.
“Katika sekta ya ardhi tunakwenda kwa sheria, na wahahkikishia wananchi hakuna mtu yoyote atakayeporwa ardhi yake bila kulipwa haki yake,” alisema
Profesa Tibaijuka alisema wananchi ambao waliporwa ardhi zao kwa ubabe aidha na watendaji wa kata au vijiji, wapeleke kero hizo ofisini kwake ili aweze kuzifanyia kazi haraka iwezekanavyo.
Profesa Jumanne Maghembe
Naye Wziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe, alisema wizara yake imejipanga kutatua kero za maji katika jiji la dare s Salaam na maeneo mengine kama Ilani ya CCM inavyoelekeza ifikapo mwaka 2015 upatikanaji wa maji mijini ifikie asilimia 90 kutoka asilimia 65 za sasa na vijijini kutoka asilimia 50 hadi asilimia 65.
Kuhusu upanuzi wa mtambo wa Ruvu Chini, alisema kuwa wanaupanua kutoka chujio moja hadi matano ambapo gharama zake zitakuwa ni dola milioni 37 na ujenzi huo unatarajiwa kukamilika Machi mwakani hali kadjhalika na ule wa Ruvu Juu.
Alisema katika mwaka wa fedha 2012/13 serikali imetenga sh. bilioni 16 kujenga bomba kubwa lenye upana wa mita 1.8 umbali wa kilomita 58 kutoka Ruvu Chini hadi matenki ya yaliyopo Chuo Kikuu cha dare s Salaam.
Profesa Maghembe alisema katika mwaka huu wa fedha serikali imetenga sh. bilioni 15 kujenga visima eneo la Kimbiji na Nampera hali kadhalika inatarajia kujenga bwawa kubwa la Kidunga mkoani Morogoro lengo likiwa ni kuongeza upatikanaji wa maji katika jiji la dare s Salaam.
Waziri wa Ujenzi 
Naye Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, alisema kuwa nchi nzima kuna miradi ya barabara yenye urefu wa kilomita 11,154 inayoendelea kujengwa kwa kiwango cha lami na kwamba otakapo kamilika hata Chadema wataendeleza maandamano yao kupitia barabara za lami.
Alisema miradi yote hiyo inagharimu kiasi cha shilingi trilioni sita ambapo nusu yake zimetolewa na serikali ya Tanzania.
“Nawapongeza wapinzani, waendelee kuandamana katika barabara za lami maana natambua kuwa shukurani ya punda ni mateke, na wasione vyaelea vimeundwa, pia unaweza kumbeba mtu mgongoni kumvusha mtoni na unapofika ng’ambo na kumshusha anakuambia kwanza mgongo wake ulikuwa 
Vyanzo:TZMPAKAAU,Ippmedia,Kamanda wa Matukio na theHabari

Keine Kommentare:

Kommentar veröffentlichen