Hali ya ya kisiasa katika Jiji la Mwanza imechafuka kufuatia wabunge wawili wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kujeruhiwa vibaya kwa kucharangwa mapanga na watu wanaosadikiwa kuwa walikodiwa kutekeleza mauaji dhidi ya wabunge hao kwa sababu za kisiasa.
Wabunge hao waliojeruhiwa sehemu mbalimbali za miili yao ni Highness Kiwia wa Ilemela na Salvatory Machemuli wa Ukerewe.
Akiwa katika uwanja wa ndege wa Mwanza tayari kwa safari ya kuelekea jijini Dar es Salaam kwa ajili ya matibabu zaidi, Kiwia ameliambia NIPASHE kwamba,
Alisema kwamba baada ya kuhitimisha kampeni za uchaguzi mdogo wa udiwani katika Kata ya Kirumba juzi jioni, baadhi ya wanachama wa Chadema akiwemo yeye (Kiwia) waliendelea na vikao vya ndani katika eneo la Ibanda Kata ya Kirumba.
Mbunge wa Ilemela Samson Higness Kiwia(CHADEMA).
Alisema kwamba ilipofika saa sita usiku aliondoka kueleka nyumbani kwake akiwa ndani ya gari ambalo alikuwa ameliazima.
Alifafanua kuwa akiwa njiani, ghafla magari mawili yalimzuia moja mbele, na lingine nyuma hivyo akashindwa kuendelea na safari.
Alibainisha kuwa vijana kadhaa waliteremka kutoka kwenye magari hayo na kumtaka atoke nje ili wamuue kwa sababu wamemtafuta tangu siku nyingi.
Aliendelea kusimulia kwamba hali hiyo ilimfanya ampigie simu OC CID wa Wilaya ya Ilemela ambaye hata hivyo hakuweza kufika mapema eneo la tukio.
Aidha, alisema aliamua pia kumpigia simu Mbunge wa Ukerewe (Machemuli) aliyekuwepo jijini Mwanza kumfahamisha hatari iliyokuwa inamkabili ambaye alifika eneo la tukio muda mfupi baadaye.
Hata hivyo, Kiwia alisema kwamba, baada ya Machemuli kuwasili eneo hilo, vijana wale walimvamia na kuanza kumshambulia hadi akazimia, ndipo wakamgeukia yeye (Kiwia) na kuanza kumshambulia kwa mapanga sehemu mbalimbali za mwili wake.
Mbunge wa Jimbo la Ilemela, Highness Kiwia (kushoto) na Mbunge wa jimbo la Ukerewe, Salvatory Machemli (kulia) wakiendelea na matibabu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) .
Alisema kuwa baada ya hapo hakujua kilichoendelea hadi alipojikuta akiwa katika Hospitali ya Mkoa wa Mwanza Sekou Toure ambako yeye na Machemuli walipatiwa huduma ya kwanza kabla ya kukimbizwa Hospitali ya Rufaa Bugando kwa matibabu zaidi.
Hata hivyo, jana mchana wabunge hao walilazimika kusafiri kwenda Dar es Salaam kwa ajili ya kupata matibabu zaidi kwa vile Kiwia alitakiwa kufanyiwa kipimo cha T-Scan ambacho hakipo Bugando.
Kiwia alisema taarifa za kuwindwa ni kwa sababu za kisiasa na kuwa alishazisikia kitambo, hivyo tukio la kukatwa mapanga limethibitisha kile alichokuwa ameambiwa huko nyuma.
Aliongeza kwamba watu waliomvamia na kumkata mapanga baadhi anawatambua na amekwisha kutoa taarifa polisi, hivyo ni jukumu la Jeshi hilo kuchukua hatua dhidi ya wahusika.
WATATU CHADEMA WAJERUHIWA KIWIRA
Eneo la kiwira Mkoani Mbeya.
Wanachama watatu akiwemo Katibu wa Vijana wa Chadema Mkoa wa Mbeya, Jacob Kaluwa, wamejeruhiwa vibaya kwa kukatwakatwa mapanga na shoka, baada ya kuvamiwa na watu wanaosadikiwa kuwa ni wafuasi wa CCM katika vurugu zilizojitokeza kwenye uchaguzi mdogo wa udiwani Kata ya Kiwira wilayani Rungwe mkoani Mbeya.
Tukio hilo limetokea jana saa 5:00 asubuhi eneo la Ilundo wakati wanachama hao wa Chadema walipokuwa katika harakati za kukagua vituo vya kupigia kura katika vijiji cha Ilunda na ndipo walipovamiwa na watu hao.
Muuguzi wa zamu katika Hospitali ya Wilaya, Grace Kapungu, alisema mbali na Katibu wa Vijana Chadema mkoa wa Mbeya, wengine waliofikishwa katika hospitali hiyo ni John Andengenye na Daudi Hamis.
Alisema Kalua amejeruhiwa mkononi na kichwani na ameshonwa nyuzi 11, Hamisi ameshonwa nyuzi tatu mkononi na nyuzi tatu nyingine kichwani wakati Andengenye ameshonwa nyuzi mbili mdomoni.
Kapungu alisema hali za majeruhi hao zinaendelea vizuri na kwamba baada ya kupata matibabu ilipofika majira ya saa 11:00 jioni waliruhusiwa toka hospitalini hapo.
Kalua alisema walivamiwa na kundi la watu 10 ambapo eneo la Ilundo.
Alisema walipofika eneo hilo wavamiaji hao waliwaeleza kuwa hapa hakuna njia ya kupita kwenda katika Shule ya Msingi Ilundo ambako kuna kituo cha kupigia kura ambapo kulitokea mabishano na ndipo walipoanza kuwashambulia.
Alisema wakati wakiendelea kushambuliwa na watu hao, ghafla lilitokea gari la polisi na ndipo watuhumiwa walikamatwa na kupeleka katika kituo kidogo cha polisi Kiwira.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Advocate Nyombi, alithibitisha kuwa watu 10 wamekamatwa kuhusiana na tukio hilo.
Keine Kommentare:
Kommentar veröffentlichen