- CHADEMA,CCM wapewa onyo
- Mkutano waitishwa kujadili
- Slaa hakubali tena kuibiwa kura
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) imesema hali katika Jimbo la Arumeru, mkoani Arusha siyo shwari na imepanga kukutana leo kujadili vurugu zinazoendelea kujitokeza kwenye kampeni za uchaguzi mdogo wa ubunge katika jimbo hilo.
Kampeni hizo zilizoanza Machi 9, mwaka huu, zimeanza kuingia dosari baada ya kuwepo vitendo vya uvunjifu wa amani huku Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na Chama Cha Mapinduzi (CCM) vikifanyiana vurugu na kushutumiana.
Mwenyekiti wa Nec, Jaji Mstaafu, Damian Lubuva, alitoa kauli
hiyo jana alipotakiwa na NIPASHE kueleza msimamo wa Nec kufuatia matukio ya vurugu hizo ambazo zinazidi kushika kasi katika Jimbo la Arumeru Mashariki.
hiyo jana alipotakiwa na NIPASHE kueleza msimamo wa Nec kufuatia matukio ya vurugu hizo ambazo zinazidi kushika kasi katika Jimbo la Arumeru Mashariki.
“Kesho (leo) tutakaa pamoja na mambo mengine, lakini pia tutaangali suala la vurugu hizo ambazo zimejitokeza huko Arumeru,” alisema.
Jaji Lubuva alisema wiki iliyopita alitoka Arumeru Mashariki, hali ilikuwa shwari, lakini ghafla ilibadilika na sasa kuna matukio mbalimbali yanayoashiria uvunjifu wa amani.
Katika hatua nyingine, Nec imetoa onyo kwa CCM na Chadema, kwa kuchezeana rafu kwenye kampeni za uchaguzi mdogo katika Jimbo la Arumeru Mashariki na kwamba ikiwa vyama hivyo vitaendelea kukiuka maadili ya uchaguzi vitatozwa faini au kusimamishwa kufanya kampeni.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa jana, Msimamizi wa Uchaguzi wa jimbo hilo ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya Maadili ya NEC, Trasias Kagenzi, alisema CCM imepewa onyo baada ya wafuasi wake kubandua picha za mgombea wa Chadema, Joshua Nassari katika viwanja vya Ngarasero, Usa River.
Alisema chama hicho kimepewa onyo kwa kuwa picha hizo zilikuwa zimebandikwa kabla ya uzinduzi wa kampeni hizo, hivyo haikuwa sahihi kwa wafuasi hao kuzing'oa.
Kagenzi alisema CCM inalalamikiwa pia kwa kutumia lugha ya kashfa na matusi kwenye kampeni zake, dhidi ya mgombea wa Chadema pamoja na suala la kumteka kiongozi wa Chadema na kumjeruhi.
Aidha, kuhusu suala la kutekwa na kujeruhiwa kwa Mwenyekiti wa Chadema wa Tawi la Magidrisho, Nuru Maeda, Kagenzi alisema suala hilo linashughulikiwa na Jeshi la Polisi, hivyo watuhumiwa watashughulikiwa kwa mkondo wa sheria.
Kuhusu Chadema, alisema chama hicho kimeonywa kwa kosa la wafuasi wake kuzuia msafara wa mgombea wa CCM, Sioi Sumari, Machi 18, mwaka huu katika eneo la Maji ya Chai, ambao pia walivunja kioo cha gari mojawapo lililokuwa kwenye msafara huo, pamoja na kuwakashifu viongozi wakuu wa CCM.
“Kamati ya Maadili imeandika barua hizi za onyo ambazo zimeridhiwa na wajumbe wote, wakiwemo wanaotoka CCM na Chadema, Tume inawakumbusha kwamba kama watarudia tutawapa karipio kali...baada ya hapo kuna faini ambayo ni Sh. 100,000 na hata kusimamishwa kufanya kampeni,” alisema Kagenzi.
Aliongeza: “Kamati ya Maadili inavikumbusha vyama vyote kuzingatia kanuni na maadili ya uchaguzi na kuwahamasisha wafuasi wake umuhimu wa kuzingatia maadili, tunavikumbusha kwamba kwenye kampeni wanadi sera na siyo kumshambulia mtu binafsi.”
Katibu mkuu wa CHADEMA taifa Dk.Wilboard Slaa
SLAA: 2010 niliibiwa kura
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Wilbroad Slaa, amedai kuwa mwaka 2010 kura zake za urais zilichakachuliwa, lakini aliamua kukaa kimya kuepusha vurugu na damu kumwagika na kuonya kuwa ikiwa CCM itaendea kuwanyanyasa wananchi watafanya maandamano kuanzia Arumeru Mashariki hadi Ikulu.
Alitoa kauli hiyo kufuatia madai ya Mwenyekiti wa Chadema Kata ya Maroroni, Paul Cyprian kukamatwa na kuteswa na viongozi wa CCM na kuongeza kuwa machafuko yaliyotokea Tunisia pia yalianza hivyo.
Aidha, Dk. Slaa aliwatahadharisha viongozi wa dini kuwa makini na wanasiasa wanaokimbilia makanisani kuficha maovu yao na kujisafisha, badala yake wawakemee ili kudumisha amani iliyopo.
Alitoa tahadhari hiyo jana wakati alipokuwa katika kijiji cha Migandini kwenye kata ya Maroroni, wilayani Arumeru, akimnadi mgombea wa chama hicho Joshua Nassari.
Alisema kumekuwapo na desturi za mafisadi kukimbilia makanisani kujisafisha, jambo linalonajisi makanisa hivyo akawataka viongozi wa dini kuwa waangalifu kwa kukemea.
“Natoa tahadhari kwa viongozi wa dini zote, sababu kazi yenu ya kwanza ni kukemea maovu na kutakasa nchi na siyo kuwasafisha mafisadi, watuhumiwa wa ufisadi wananajisi kanisa la Mungu, tambueni kwamba manufaa ya fedha wanazotoa ni ya muda mfupi,” alisema.
Dk. Slaa alisema haiwezekani mwanasiasa akatoa Sh. milioni 100 kwa ajili ya kanisa bila kuwa na uchungu nazo wala kufahamu atazirudisha vipi.CCM, CHADEMA WAPIGANA VIJEMBE
Vijembe na kashfa vinazidi kutawala kampeni hizo baada ya CCM jana kudai kuwa Chadema kinatembeza bakuli kwenye mikutano ya hadhara baada ya wafadhili wake kuwanyima fedha kutokana na serikali kukataa kukubali kuwepo kwa ndoa za jinsia moja.
Katikati ni Mwingulu NChemba katibu itikadi na uenezi CCM.
NCHEMBA: CHADEMA WAMEFULIA
Meneja wa kampeni za CCM, Lameck Nchemba, alidai kuwa mfadhili wa chama hicho ni Chama cha Conservative kinachoongoza serikali ya Uingereza.
Alidai kuwa serikali ya inayoongozwa na chama hicho katika siku za karibuni kilitaka nchi wanachama wa Jumuiya ya Madola kukubali ndoa za jinsia moja kama sharti la kupata misaada kutoka nchini humo.
Alisema kuwa tangu Chadema kianzishwe hakijawahi kutembeza bakuli na kuwakamua wanachama wake kwenye mikutano ya hadhara na kwamba kinachowalazimisha kufanya hivyo ni ukata, baada ya serikali kukataa masharti ya Waingereza.
Nchemba ambaye ni Mbunge wa Iramba Magharibi na Katibu wa Uchumi wa Halmashauri Kuu ya Taifa (Nec) ya CCM, aliendelea kudai kuwa katika uchaguzi mdogo wa Jimbo la Igunga, mkoani Tabora mwaka jana, Chadema kilikuwa na fedha nyingi kilizopewa kama msaada kutoka nje.
“Hiyo ndiyo sababu waliweza kusumbua, lakini safari hii wamenyimwa ndio maana hata viongozi wao wa kitaifa hawashiriki wote kwenye kampeni hizi,” alidai na kuongeza kuwa kukosekana kwa fedha hizo ndiyo maana mbwembwe walizokuwa wakizifanya Igunga hazionekani Arumeru.
Aliwaambia wananchi kuwa wapinzani wameshindwa kueleza sera na matokeo yake wanaeneza propaganda za uongo, lugha za matusi na chuki miongoni mwa wananchi.
Aliwataka wananchi hao kumchagua mgombea wa CCM ili waweze kupata maendeleo. “Itakuwa juu yenu Wanaarumeru kuamua juu ya mustakabali wa maendeleo ya Meru, CCM ndiyo jibu,” alisema Nchemba.
BULAYA: CCM SIO CHAMA CHA WAZEE
Naye Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Ester Bulaya, amewataka vijana kumchagua mgombea wa chama hicho kwa kuwa ni kijana msomi na kuwa atasaidiana naye kupigania maslahi ya vijana bungeni.
Bulaya aliyasema hayo katika vijiji vya Ngakisosia na Kidire, Kata ya na kuongeza: “Wapinzani wanadai eti CCM ni chama cha wazee, wanasema uongo mchana kweupe… Hivi mimi hapa ni mzee, waachani waendelee na uongo wao mchagueni mgombea wa chama chenye ilani iinayotekelezwa mpate maendeleo.”
Bulaya alisema propaganda za uongo za wapinzania hazina msingi na kwamba kuna maeneo wananchi wamekwisha kuwafahamu na kuwanyima kura. “Mfano halisi ni Jimbo la Tarime, waliwadanganya wapiga kura kuwa watoto wao wangesomeshwa bure, lakini hawakufanya hivyo na wapiga kura wa Tarime wakaamua kumchagua mgombea wa CCM mwaka 2010,” alisema.
Naye Sioi aliwaahidi wananchi kuwa akishinda atashughulikia kero za wananchi, ukiwemo ukosefu wa umeme.
Meneja wa Kampeni za CHADEMA jimbo la Arumeru na mbunge wa jimbo la Karatu Mchungaji Israel Natse.
NATSE: CCM WANATUMIA UDINIMbunge wa Karatu (Chadema), Mchungaji Israel Natse, amesema CCM kimewakusanya wachungaji wa madhehebu ya Pentekoste zaidi ya 120 na kuwataka wahamasishe waumini wao wakichague chama hicho.
Alisema iwapo wachungaji watakubaliana na matakwa ya CCM wanaweza kuhatarisha amani ya Meru kwa kuwa wataingiza nchi katika vita.
“Jana (juzi) CCM iliwaita viongozi wa Pentekoste ili kuwashawishi waumini wao wamchague Sioi kwa ajili ya kumfuta machozi mjane wa marehemu na yeye kwa sababu ya kufiwa na baba yao, nawasihi wachungaji kwa unyenyekevu mkubwa, msikubaliane na matakwa yao kwa sababu mtaingiza nchi hii katika vita,” alisema jana katika mkutano uliofanyika katika kijiji cha Migandini, Kata ya Maroroni.
Mchungaji Natse alisema CCM wamezoea kutumia udini katika chaguzi ndogondogo, akitolea mfano wa uchaguzi Igunga, kwamba walitumia udini na Waislamu waliambiwa wasipigie Chadema hali wanayotaka kuileta Arumeru Mashariki, kwa kutumia makanisa kisiasa.
“Hawa watu wanakemea udini na kuimba kuwa taifa letu halina udini, lakini wenyewe wamekuwa mstari wa mbele kutumia udini kushawishi watu,” alisema.
Naye mgombea wa chama hicho, Joshua Nassari, alisema haombi ubunge ili aishi nyumba ya kifahari, bali anataka kuwakilisha watu wa jimbo la Arumeru Mashariki.
“Ndugu zangu naombeni msifanye makosa hawa CCM wamepita kunitukana, huku wakipita majumbani kunitukana wanasema sijafunga ndoa, wakati wanafahamu mimi mkristo mzuri ninayefahamu mke mwema, huchaguliwa na Mungu na wakati ukifika nitaoa,” alisema.
Mbunge wa Korogwe Vijijini (CCM) bw.Stephen Ngonyani aka Profesa Maji Marefu
MAJI MAREFU ATEMBELEA CHADEMA
Katika hatua nyingine, Mbunge wa Korogwe Vijijini (CCM), Stephen Ngonyani, ametembelea ngome ya Chadema iliyopo eneo la Usa River na kulakiwa na wabunge wenzake wa kambi ya upinzani, pamoja na mgombea wa Chadema katika jimbo la Arumeru Mashariki, Nassari.
Ngonyani ambaye ni maarufu kwa jina la Profesa Majimarefu, alifika kwenye kambi ya Chadema mapema asubuhi jana ambapo alisalimiana na wabunge wa Chadema Vincent Nyerere (Musoma Mjini) na Mchungaji Msigwa (Iringa Mjini).
Ngonyani alikuwa akizungumza na wabunge wenzake akiwatia moyo kwamba Chadema ina nafasi kubwa ya kushinda katika kinyang'anyiro hicho.
Hata hivyo, kitendo cha Majimarefu kutembelea ngome ya Chadema, kilitafsiriwa vibaya na baadhi ya wafuasi wa chama hicho, ambao walimtaka aondoke eneo hilo kwa kuwa CCM kimekuwa kikiwanyanyasa wafuasi wa Chadema ikiwemo kuwapiga na kuwajeruhi.
Kufuatia kauli ya wafuasi hao, wabunge wa Chadema walimlazimisha Majimarefu kuondoka huku akisindikizwa na Nassari pamoja na viongozi wengine wa chama hicho.
Vyanzo:TZMPAKAAU,Ippmedia,Swahili villa,Kamanda wa Matukio Yasni world na IBN news.
Keine Kommentare:
Kommentar veröffentlichen