Best Blogger TipsSoon

Freitag, 4. November 2011

TZMPAKAAU

MAWAZIRI :USHOGA HAUKUBALIKI
MINISTERS: NO TO HOMOSEXUALITY 
Serikali ya Tanzania imesema haitakubali kutambua haki za watu wa ndoa za jinsia moja na imesema iko tayari kuvunja uhusiano na Uingereza kama itatoa misaada kwa masharti ya kutambua ndoa hizo ambazo ni kinyume cha utamaduni wa Kitanzania.
Msimamo huo wa serikali kupinga kutambua haki za mashoga ulitolewa jana kwa nyakati tofauti na mawaziri wanne.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, aliwaambia waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuwa Tanzania iko tayari kuvunja uhusiano na Uingereza na kusisitiza kuwa ipo tayari kubaki na umasikini wake kuliko kukubaliana na masharti ambayo yanakiuka utamaduni wa nchi ambao unaongozwa na familia.
Membe aliwaambia waandishi wa habari kuwa tamko lililotolewa na Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameroon, ni hatarishi na linaweza kuvunja Jumuiya ya Madola.
Bendera za nchi za madola
Alisema kuwa endapo likitokea jambo hilo waziri huyo atatakiwa kuwajibika kwani Jumuiya hiyo imeunganishwa na nchi 54 ambapo nchi 13 zimeridhia masuala ya ushoga na nchi 41 zimepinga suala hilo.
Membe alisema Tanzania haiwezi kuyumbishwa wala kupindisha sheria kwa sababu ya msaada wa nchi moja. ”Tuko tayari kwa lolote na hata ikiwezekana kuvunjika kwa mahusiano kwa masharti ya kishenzi kama ni hela zao basi wabaki nazo,” alisema.
Aliongeza kuwa sheria ya mwaka 1971 iko wazi kuwa Tanzania inakataza ndoa za jinsia moja hivyo Uingereza isitake kuilazimisha kuivunja kwa kuwa hatua hiyo inaweza kuleta mifarakano.
Membe alisema katika kuthibitisha kuwa Tanzania haikubalianani na masharti ya Uingereza, mwanzoni mwa mwaka huu alipokea barua kutoka nchi moja ambayo hakuitaja jina ikimtaka ampokee balozi ambaye amefunga ndoa na mwanaume mwenzake.
Alisema kitendo hicho kilimshtua sana na ndipo alipoamua kuwasiliana na Rais Jakaya Kikwete, ambaye alijibu neno moja tu la “Tobaa”.
“Kauli hiyo ya Rais ilinishtua sana na kujiuliza maswali mengi, ndipo alipowasiliana na huyo balozi ambaye alikuwa anamaliza muda wake na kumuambia kuwa haitawezekana kumpokea balozi huyo kutokana sheria ya Tanzania kukataza ndoa za jinsia moja,” alisema Waziri Membe.
 
Viongozi wa mataifa mbalimbali katika mkutano wa mwaka 2011 wa nchi jumuiya. 
Membe alisema katika mkutano wa wakuu wa nchi za Jumuiya ya Madola uliofanyika Oktoba 29 hadi 30, mwaka huu nchini Australia, ushoga haikuwa ajenda ya mkutano huo na kwamba Cameroon alitoa tamko hilo nje ya mkutano.
“Hii ni staili mpya ya kuunganisha msaada na ushoga na hatupo tayari kwani hayo masharti ni magumu,” alisema Membe.
KOMBANI: SI UTAMADUNI WETU
Akizungumza na NIPASHE jana, Waziri wa Katiba na Sheria, Celina Kombani, alisema suala hilo si utamaduni wa Watanzania na kwamba kamwe halikubaliki.
“Kwa utamaduni wetu hilo halipo na haiwezekani tukawa na sheria ya namna hiyo, sheria zote za nchi yetu zinatungwa na Watanzania wenyewe na mimi kama Waziri wa Katiba na Sheria nimesema hatuna mpango wa kuwa na sheria ya kutambua mashoga wala hatufikirii kuwa nayo kwa sababu sio utamaduni wetu,” alisema Kombani.
Alisisitiza: “Nasema haiwezekani tukawa na sheria ya namna hiyo.”
SOPHIA SIMBA: SI LAZIMA UINGEREZA ITUSAIDIE
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Sophia Simba, alisema mjini Arusha jana, kuwa Tanzania haikubaliani na suala hilo.
“Sikubaliani na suala la Waziri Mkuu wa Uingereza kuhusu kuitambua haki hiyo, sisi hatufungamani na sheria zao na zaidi tunayo maadili ya kwetu,” alisema.
Alisema Tanzania inaweza kujiendesha bila hata misaada ya kwao na haiwezi kukubali kutambua ndoa za jinsia moja kama moja ya haki za msingi za binadamu.
Alisema Uingereza na washirika wake wana tamaduni zao zinazoruhusu ndoa za aina hiyo, lakini sio utamaduni wa hapa kwetu na nchi nyingine za Afrika.
Alisema Tanzania haitakubali kuendekeza misaada yenye masharti kama hayo kwani inaweza kujiendesha bila kupokea fedha zenye masharti kama hayo.
Alisema Tanzania ina changamoto nyingi ambazo zinahitaji kutafutiwa ufumbuzi, lakini suala la ndoa za njisia moja si sehemu ya changamoto zinazolikabili taifa.
Msimamo wa serikali ya Tanzania umekuja siku chache baada ya Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron, kutangaza kuwa kuwa nchi zinazopata misaada kutoka kwao, zitapimwa kama zinakubali haki za mashoga kama zinataka kuendelea kunufaika na misaada hiyo.
Cameron alisema moja ya masharti ya ufadhili kutoka Uingereza ni nchi husika kutambua ndoa za jinsia moja na kwamba sera hiyo imeanza kutekelezwa kwa baadhi ya nchi.
Vyanzo:TZMPAKAAU na IPPMEDIA

Keine Kommentare:

Kommentar veröffentlichen