Best Blogger TipsSoon

Samstag, 23. April 2011

TZMPAKAAU

VIONGOZI WA DINI WANENA
Kasi ya viongozi kujilimbikizia mali na kusahau watu maskini inatisha na isipodhibitiwa inaweza kuliingiza taifa mahali pabaya.
Hayo yalisemwa jana na Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Kanisa Kuu la mjini Iringa, Enock Mlyuka, wakati akihubiri katika Ibada ya Ijumaa Kuu.
Alisema viongozi hao wamesahau hali ngumu ya maisha inayowakabili wananchi na ameshauri watawala watafute ufumbuzi wa kuondoa tofauti ya matabaka kati ya walionacho na wasionacho.
Alisema mgawanyiko baina ya wenye nacho na wasio nacho kama hautaangaliwa mapema utaligawa taifa kutokana na viongozi kushindwa kutekeleza majukumu yao na wao kujikita katika maslahi binafsi.
Mchungaji Enock ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Tumaini kilichopo mkoani Iringa anayeshughulikia kitengo cha Theolojia.
Alisema mmomonyoko wa maadili kwa baadhi ya viongozi waliopewa madaraka, kutojali wajibu wao, ndivyo vimelitumbukiza taifa mahali pabaya.
Akizungumzia mabadiliko ya kisiasa hapa nchini, mchungaji huyo alisema kuwa hata kama zitatangazwa kauli mbiu za kujivua gamba, kama viongozi waliopewa dhamana ya kuwatumikia wananchi wataongozwa na mtindo wa chukua chako mapema mambo yatakwenda kama zamani na hakuna mabadiliko yatakayotokea.
Akizungumzia machafuko ya kisiasa na migogoro inayoendelea barani Afrika kwa sasa, Mchungaji Enock alisema kuwa sababu kubwa ni ufa unaotokana na waliopata nafasi kutowajali watu wa chini.
Alisema viongozi wa umma kujali zaidi maslahi yao kuliko kuwatumikia wananchi ni mbegu ya hatari inayopandwa.
Alitaka viongozi hao kuzingatia misingi ya haki sambamba na kuhakikisha kuwa raslimali za taifa zilizopo zinalenga kuwanufaisha wananchi ambao, ndio waliowaajiri kuwaongoza.
Mkoani Mbeya, viongozi wa kisiasa hususan wabunge, wametakiwa kutoyakimbia majimbo yao baada ya kupata ubunge na kwenda kukaa katika miji mikubwa, badala yake wakae kwenye maeneo yao ili kutambua kero za wananchi.
Wito huo ulitolewa na Paroko wa Kanisa Katoliki la Mwanjelwa Jijini Mbeya, Padri Mwakasita, wakati wa mahubiri kwenye Ibada ya Ijumaa Kuu ambapo waumini wa Kikristo walikumbuka mateso ya Yesu Kristo.
Alisema viongozi hao wanapaswa kuwaheshimu wananchi waliowapa dhamana ya kuwaongoza na kujitoa kuwatumikia kwa moyo mmoja badala ya kuwaacha na kwenda kuishi katika miji mikubwa.
Aidha, Paroko Mwakasita aliwataka viongozi hao wasitumie nafasi zao kuwanyanyasa wananchi waliowapa dhamana na badala yake wafuate maadili ya uongozi.
Paroko Mwakasita pia aliwageukia viongozi wa juu serikalini na kuwataka kutumia maliasili za nchi vizuri ili zitumike kwa manufaa ya nchi na Watanzania kwa ujumla badala ya viongozi kuzitumia kujinufaisha wao wanyewe na hatimaye kufilisi nchi.
"Hivi karibuni kumekuwa na kashfa nyingi kuhusiana na wimbi la ufisadi ambalo ni matokeo ya tamaa za viongozi wetu kujilimbikizia mali nyingi ," alisema Padri Mwakasita.
Padri Mwakasika pia aliwaonya viongozi kuwa makini na mikataba mikubwa ambayo nchi inaingia na wawekezaji mbalimbali ambayo inaweza kuwatia matatani na kuwachafua wenyewe pamoja na maadili ya kazi yao.
Alisisitiza kuwa viongozi hawapaswi kukimbilia kuishi kwenye miji mikubwa wakati wote wa uongozi wao na kisha kujisogeza tena kwa wananchi unapofika wakati wa uchaguzi.
Mkoani Mwanza Wakristo wametakiwa kusimamia ukweli na haki ili kutimiza mapenzi ya Mungu kama alivyofanya Yesu Kristo.
Hayo yalisemwa jana na Mhashamu Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Mwanza, Yuda Thadeus Rw’aichi, katika ibada ya Ijumaa Kuu iliyofanyika katika Kanisa Kuu la Epafania `Toleo la Bwana’.
Alisema watu wengi wameshindwa kusimama katika ukweli na uwajibikaji badala yake wamekuwa wakifanya maamuzi kwa kufuata matakwa ya baadhi ya watu.
Alisema Yesu Kristo alikuwa mkweli na mwajibikaji na ndio maana alipoulizwa na Wayahudi wewe ndiye Yesu wa Nazarethi? Hakusita kujibu kuwa yeye ndiye Kristo bila kuogopa atafanywa nini.
Akilinganisha na ulimwengu wa leo, Rw’aichi alisema siku hizi viongozi wanafanya mambo kwa ajili ya kufurahisha marafiki au ndugu zao na sio kutenda haki.
“Mambo siku hizi yamebadilika watu wengi tunapofanya makosa lawama tunawatupia wenzetu ili kunusuru roho zetu na nafsi zetu,” alisema askofu huyo katika ibada hiyo iliyohudhuriwa na waumini wengi wa Kanisa Katoliki jijini hapa.
Jijini Dar es Salaam, Wakristo wote wametakiwa kudumisha upendo na kusameheana katika kipindi hiki cha kukumbuka mateso na kifo cha Yesu Kristo na kuelekea maadhimisho ya kufufuka kwake.
Rai hiyo ilitolewa jana jijini Dar es Salaam na Waziri Mkuu Mstaafu, John Malecela, katika Ibada ya Ijumaa Kuu iliyofanyika kitaifa katika Kanisa la Presbitarian la jijini.
Malecela alisema siku hiyo ni muhimu kwa Wakristo wote na kwamba wanatakiwa kuacha chuki na kujenga utamaduni wa kusamehe ili kuepusha chuki katika jamii ya Kitanzania na kwingineko duniani kwa kigezo cha udini.
“Nawasihi Watanzania kuacha chuki za udini ili kudumisha amani tuliyonayo katika nchi yetu… hayati Baba wa Taita, Julius Nyerere alisisitiza wananchi kuwa na amani na utulivu, alipinga ukabila, rangi wala itikadi,” alisema Malecela.
Katibu Mkuu wa Baraza la Kikristo Tanzania, (CCT), kutoka mkoani Dodoma, Leonard Mtaita, aliwataka Wakristo kukumbuka namna ya utii katika kipindi hiki kuelekea maadhimisho ya kufufuka kwa Yesu Kristo.
Naye Mkurugenzi wa Msimbazi Center, Padri Novatus Mbaula, aliwataka Wakristo wote kuboresha mienendo yao ikiwemo kuepukana na mazingira yasiyofaa wakati huu.
Padri Mbaula alitoa rai hiyo kwa waumini wa Kanisa Katoliki la St. Joseph katika ibada ya Ijumaa Kuu jijini Dar es Salaam.
Imeandikwa na Godfrey Mushi, Iringa; Furaha Eliab, Mbeya; Cosmas Mlekani, Mwanza; Hellen Mwango na Mary Geofrey, Dar es Salaam.
Vyanzo:Nipashe,TZMPAKAAU

Keine Kommentare:

Kommentar veröffentlichen