Best Blogger TipsSoon

Samstag, 5. März 2011

TZMPAKAAU

Ya Kikwete,Gongo la mboto na Aladawi

WAKATI tunakaribia kumaliza robo ya kwanza kati ya nne za mwaka huu 2011,Tanzania imeshuhudia matukio kadhaa yanayostahili kujadiliwa kwa kina. Lakini kutokana na ufinyu wa muda na nafasi, makala hii itaangalia matukio mawili makubwa ambayo yanahusiana kwa namna moja au nyingine.
Tukio la kwanza ni milipuko ya mabomu katika kitongoji cha Gongo la Mboto jijini Dar es Salaam. Hadi muda huu ninapoandika makala hii, waathirika wa milipuko hiyo bado wanaendelea kuteseka.
Wengine bado wana majonzi ya kupoteza ndugu na jamaa zao (kwa vifo au kupotea), uharibifu wa mali zao, au kuathirika kiafya. Na athari hizo zinaendelea huku waliozembea kiutendaji na kusababisha milipuko hiyo wakigoma kuwajibika, na huku mwenye dhamana ya kuwawajibisha (Rais Kikwete) akiwa bize na mambo mengine .
Si vema kutumia janga kuwa jukwaa la siasa au kutupiana lawama. Kufanya hivyo ni kuwaongezea maumivu waathirika wa janga husika. Hata hivyo, kuna nyakati tunalazimika kutonesha vidonda ili kusaka tiba ya kudumu. Kwa mfano, kama “kuwakalia kooni” wazembe waliosababisha mabomu hayo kulipuka kutapelekea wajiuzulu na hatimaye kurejesha imani na usalama wa wananchi, basi, ni vema kufanya hivyo.
Ni katika mantiki hiyo inayumkinika kusema bayana kuwa tukio la milipuko ya Gongo la Mboto limetusaidia, kwa mara nyingine, kuonyesha ombwe kubwa linaloukabili uongozi wa Rais Jakaya Kikwete.
Japo ni rahisi kumlaumu Kikwete hasa pale anaposita kufanya maamuzi mepesi; achilia yale magumu, ni vigumu sana kubashiri kwa nini anashindwa kufanya maamuzi hayo.
Alipochelea kuwachukulia hatua za kisheria viongozi waliohusishwa na ufisadi wa Richmond, na hivyo kusababisha sakata tuliyonayo ya Dowans, kulikuwa na “kisingizio” kuwa “hao ni watu wake wa karibu” ambapo baadhi yao walikuwa na ujasiri wa kutamka hadharani kuwa “hawakufahamiana na Kikwete kwa kukutana mtaani” kuashiria kuwa wao na mkuu huyo wa nchi ni “damu damu”.
Kadhalika, Kikwete alipoamua kupuuza tuhuma za ufisadi zilizokuwa zikiwakabili baadhi ya wagombea ubunge kwa tiketi ya CCM (kwenye Uchaguzi Mkuu uliopita) na kuwapigia kampeni hadharani, kulikuwa na “utetezi” kuwa wagombea hao ni watuhumiwa tu.
Lakini utapata wapi utetezi wa uamuzi usio wa busara wa Rais wetu kuweka kando janga lililowakumba wakazi wa Mbagala na kwenda Mauritania kushughulikia mgogoro wa kisiasa nchini Ivory Coast?
Hivi hiyo sio dalili ya wazi ya kiongozi asiyethamini vipaumbele vyake na vya wananchi waliompa dhamana ya kuwaongoza? Amani na usalama huko Ivory Coast ni muhimu, lakini amani na usalama wa Watanzania; hususan waathirika wa milipuko ya mabomu, ni muhimu zaidi.
Hadi siku chache zilizopita, nilikuwa sielewi kwa nini Kikwete anachelea kuwawajibisha Waziri Mwinyi na Jenerali Mwamunyange. Lakini pongezi zimwendee Katibu Mkuu wa CHADEMA Dkt Willibrod Slaa, “aliyelipua bomu” kuwa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) lilishaomba fedha za kuteketeza mabomu yaliyokwisha muda wake lakini Serikali ya Kikwete ikapuuza.
Nasema “ikapuuza” kwa sababu kisingizio kuwa serikali haina fedha hakiendani na hali halisi hasa tunaposikia serikali hiyo hiyo ikiweka bayana dhamira yake ya kulipa fidia ya mabilioni ya shilingi kwa kampuni ya Dowans (rejea kauli za Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja na Mwanasheria Mkuu Fredeeick Werema).
Lakini hata kama Kikwete amejidai kuwageuka watendaji wake hao na kudai “naye ni miongoni mwa wasiotaka Dowans ilipwe, serikali itajitetea vipi kuwa haina hela ya kuteketeza mabomu lakini inamudu kumpatia kila mbunge shilingi milioni 90?
Ukijumlisha kiwango hicho na idadi ya wabunge wetu 323 utabaini  kuwa jumla yake sio tu ingetosha kuteketeza mabomu yaliyokwisha muda wake; bali pia huenda kingemsaidia Kikwete kuanza utekelezaji wa ahadi yake ya kumpatia laptop kila mwanafunzi (kama bado anaikumbuka…au alimaanisha dawati kwa kila mwanafunzi?).
Kumbe basi nafsi inamsuta Kikwete kuwatosa Mwinyi na Mwamunyange kwa vile anafahamu fika kuwa uwepo wa viongozi hao unasaidia kutengeneza ngao ya kuzuia lawama kumwangukia yeye.
Hilo, hata hivyo,  haliwafanyi Mwinyi na Mwamunyange kutokuwa na hatia; kwani laiti wangekuwa wazalendo na wenye uchungu na maisha ya Watanzania wenzao, basi, wangeweza hata kuomba wapumzishwe nyadhifa zao ili dhamira zao zisiendelee kuwasuta.
Tuangalie tukio la pili. Hili sio tu linachefua lakini pia linaleta hisia kuwa tusipokuwa makini kuna siku Tanzania itageuka koloni binafsi la mafisadi. Kama tamithilia fulani vile, Kikwete alipoondoka tu kwenda Mauritania tukapata “ugeni wa kitaifa” wa anayeelezwa kuwa mmiliki wa kampuni ya Dowans,  Jenerali (Mstaafu) Sulaiman Mohammed Yahya Al Adawi wa Oman.
Mwarabu huyu tunayeambiwa alikimbia nchi mara baada ya Mapinduzi ya Zanzibar yaliyoung’oa utawala dhalimu wa Sultani, ameacha historia ya vituko. Hakutaka kwa hiari kupigwa picha wala kurekodiwa ingawa baadaye waandishi wa habari waliweza kumpiga picha kikachero wakati akitembelea mitambo hiyo ya Dowans.
Nawashangaa wahariri kwa hatua yao ya awali ya kumkubalia Adawi asipigwe picha. Kwangu mimi, huko ni sawa na “kuuza uhuru wa taaluma yao tukufu” kwa kutekeleza matakwa ya mfanyabiashara huyo. Kwanini wasingemwambia bayana kuwa “haki yako ya kutotaka upigwe picha au urekodiwe sio muhimu zaidi ya wajibu wetu kama wanahabari kuwathibitishia  wasomaji au wasikilizaji wetu kuwa tamko la Adawi ni la kweli na si uzushi”.
Hapa, namaanisha kuwa haki inapaswa kuendana na wajibu. Haki ya Adawi “kujificha” ilipaswa kuendana na wajibu wa waandishi wa habari “kumwonyesha kwa umma”. Wanahabari walikubali “kuuza uhuru wao” na kutojali iwapo umma utaipokea kwa mashaka habari watakayoripoti kuhusu mfanyabiashara huyo; kwani hakuna picha wala sauti kuthibitisha ukweli wa tukio na habari hiyo.
Hivi kama wahariri hao wangeweka msimamo kuwa “bila picha yako tunaondoka” bado Adawi angeendeleza “nyodo” hizo? Alichofanya mfanyabiashara huyo ni udhalilishaji kwa wahariri hao na taaluma ya habari nchini Tanzania.
Natumaini wanahabari walioalikwa kwenye press conference hiyo hawatarudia udhaifu wa aina hiyo na watasimama kidete kupinga kugeuzwa vipaza sauti vya watu wasiothamini wajibu wa wanahabari na haki za umma unaowategemea wanahabari hao.
Na vituko vya Adawi havikuishia hapo.Wakati huko nyuma alikana kuifahamu kampuni ya Dowans-achilia mbali kuimiliki (rejea mahojiano yake na Mwanakijiji wa KLH News).
Lakini katika kile kinachoweza kuashiria kuwa Adawi ni “mtu muhimu” kwa utawala wa Kikwete, iliripotiwa kuwa kabla hajarejea Oman alikwenda Ikulu na kukutana na Makamu wa Rais, Dk. Gharib Bilal (ambapo pia aligoma kupigwa picha). Ikumbukwe kuwa kwa wakati huo Dk. Bilal alikuwa anakaimu urais kutokana na Kikwete kuwa nje ya nchi. Si Makamu wa Rais wala Ikulu waliothibitisha kufanyika kwa kikao hicho wala kueleza kilichozungumzwa.
Nihitimishe kwa kugusia madai ya Adawi kuwa yuko radhi kupunguza fidia anayoidai TANESCO. Dowans ni zao la mkataba wa kifisadi wa Richmond. Kwa Adawi na Dowans yake kudai fidia ni sawa na kibaka kukupora kisha anakupigia ukelele wa “mwizi,mwizi...” na baada ya wananchi wenye hasira kumshushia kipigo aliyeporwa (baada ya kughilibiwa na kelele za kibaka), mwathirika huyo anakejeliwa na kibaka kwa kudaiwa fidia “ya kumpora” na kumdhihaki kuwa yuko radhi kupunguza fidia hiyo kama wataafikiana!
Tahadhari: tusipokuwa makini baadhi ya wawekezaji wa nje wanaoletwa nchini na vibaraka waliofadhiliwa katika malengo yao ya kisiasa na kiuchumi wanaweza kuishia kuigeuza Tanzania kuwa koloni binafsi. Unapoona waliokimbia ukombozi wa wazawa wanakuja kutuhubiria hili na lile, basi, kuna hatari ya watu wa aina hiyo kurejea jumla na kutaka kutuongoza.

Chanzo:Raia mwema
kwamaelezo zaidi Barua pepe: epgc2@yahoo.co.uk
tembelea blog:Chahali.blogspot.com

Keine Kommentare:

Kommentar veröffentlichen