Best Blogger TipsSoon

Donnerstag, 24. März 2011

TZMAPAKAAU

                                Damu nyingine yamwagika

  • Ni ajali nyengine tena morogoro ndani ya kipindi cha siku tatu


Eneo ambalo ajali ya iliyowahusisha 5stars ilipotokea
                                  Picha ya gari la wasanii wa 5 Stars
Wakati Watanzania na tasnia ya usanii nchini wakiendelea kuomboleza vifo vya wanamuziki 13 wa bendi ya Muziki wa Taarab ya Five Star waliofariki dunia kwa ajali ya barabarani, ajali nyingine imeua watu watatu na kujeruhi wengine saba katika barabara kuu ya Morogoro-Iringa.
Ajali hiyo iliyotokea jana ililihusisha basi la abiria mali ya Kampuni ya Upendo ambalo liligongana uso kwa uso na Mitsubishi Canter na watu watatu kufariki dunia papo hapo na wengine saba kujeruhiwa.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Adolphina Chialo, alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo majira ya saa 5:30 asubuhi katika eneo la N’gapa, mpakani mwa mikoa ya Morogoro na Iringa.
Chialo alisema ajali hiyo ilihusisha basi la kampuni ya Upendo lenye namba T 400 APM aina ya Scania lililokuwa likitoka Mbeya kwenda jijini Dar es Salaam ambalo lilibeba askari Magereza waliokuwa wakitokea Chuo cha Magereza Kiwira ambalo lilipinduka katika ajali hiyo.
Kamanda Chialo alisema kuwa kabla ya kupinduka, basi hilo liligongana uso kwa uso na Canter hiyo namba IT 0125 iliyokuwa ikitokea jijini Dar es Salaam kwenda Malawi.
Chialo alisema magari hayo yaligongana wakati dereva wa Canter akijaribu kumkwepa mpanda baiskeli, Atilia Kimuli (26), mkazi wa Malolo mkoani Iringa.
Kamanda Chialo alisema watu wote watatu waliokuwa ndani ya Canter walifariki papo hapo katika eneo la ajali.
Watu hao walitambulika kuwa ni Ibrahim Chimvu, Pekile Mariot na mwanamke mmoja ambaye jina wala makazi yake havikutambulika mara moja.
Miili ya marehemu ilipelekwa kituo cha Polisi Mikumi, ikisubiri gari lililotumwa na makao makuu ya Polisi mkoa wa Morogoro kwa ajili ya kuisafirisha kuhifadhiwa katika Hospitali ya Mkoa wa Morogoro.
Kwa mujibu wa Chialo, askari sita wa Magereza waliokuwa ndani ya basi la Upendo walijeruhiwa na kulazwa katika Hospitali ya Misheni ya Mtakatifu Kizito.
Askari waliojeruhiwa ni D.1802 WDR Gervas, D.3062 WDR Emmanuel Shija, WDR Ally Kassim, D 2086 WDR Vincent na Mwasenga Herman Israel, wakazi wa Dar es Salaam.
Kuhusu majeruhi wa ajali iliyoua wasanii 13 katika barabara hiyo, Kamanda Chialo alisema wamehamishiwa katika hospitali za Dar es Saalam na Zanzibar.
Aidha maiti zote za wasanii hao zilipelekwa Dar es Salaam na Kibaha mkoani Pwani kwa mazishi.
Alisema dereva wa gari aina ya Coaster lililokuwa limewabeba wasainii hao na lile lililokuwa limeegeshwa barabarani likiwa na shehena ya mbao bado wanasakwa na polisi.
Katika hatua nyingine, maiti za wasanii watano wa kundi zilizohifadhiwa katika Hospitali ya Temeke jijini Dar es Salaam zimesafirishwa kwenda mikoa ya Pwani na Tanga kwa ajili ya mazishi.
Miili ya marehemu hao iliichukuliwa jana na ndugu zao, ambao pamoja na mambo mengine waliishukuru serikali kwa kuuchukulia msiba huo kama janga la kitaifa.
Katika utataribu uliowekwa na wanafamilia hao, miili ya marehemu Hassan Ngereza na Haji Abdallah `Tall' ilisafirishwa kwenda Tanga kwa ajili ya maziko; Hamisa Mipango na Tizo Mgunda walizikwa maeneo ya Kisemvule na Vikindu Wilaya ya Mkuranga huku Shebe Juma akizikwa katika makaburi ya Mburahati.
Hata hivyo, Issa Kijoto, Nasoro Madenge, Omar hashim `Papa Kisauji', Samir Maulid, Maimuna Makuka walizikwa juzi usiku mara baada ya miili yao kuwasili kutoka Morogoro ikiwa imeharibika vibaya.
Kabla ya kuanza safari Mwenyekiti wa Kamati ya mazishi kutoka Manispaa ya Temeke, Diwani Zena Mgaya, alisema madiwani wa Halmashauri hiyo walitoa Sh. milioni tatu kwa ajili ya kuchangia mazishi ya wasanii hao.
Pamoja na fedha hizo, pia walitoa mchele kilo 50 kwa kila familia ya marehemu.
“Tumeumia sana kama wana Temeke, ikumbukwe Bendi ya Five Stars ilikuwa ndani ya eneo letu na msiba huu kwetu ni mzito sana, hivyo tumeamua kuweka nguvu zetu kuzisaidia familia kwa ajili ya mazishi,” alisema Mgaya.
Alisema, anawashukuru wananchi wa Temeke kwa kuwa wavumilivu wakati wa mapokezi ya marehemu wapendwa wao na kilichobaki kuwazika kwa heshima zote pamoja na kuwaombea kwa Mungu awalaze mahali pema peponi.
Hata hivyo, mume wa marehemu Hamisa, aliyejitambulisha kwa jina la Musa Mipango, alisema anaishukuru Serikali kwa kusaidia kwa kiasi kikubwa katika kuwasafirisha marehemu kutoka Morogoro hadi Dar es Salaam kwa heshima.
Wafiwa waliwapongeza Mbunge wa Jimbo la Morogoro Mjini, Abood Aziz na Mbunge wa Temeke, Abbas Mtemvu, kwa kutoa msaada wa mahitaji ya kufanikisha mazishi.
CHADEMA YATUMA RAMBIRAMBI
Wakati huo huo, Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimetoa rambirambi kuhusiana na vifo vya wasanii hao.
Taarifa ya chama hicho iliyotolewa jana na kusainiwa na Waziri Kivuli wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Joseph Mbilinyi, ilieleza kuwa kimepokea kwa uchungu na majonzi makubwa msiba huo wa kitaifa.
“Ni huzuni kubwa kwangu binafsi kama mmoja wa wasanii hapa nchini, na kama Waziri Kivuli wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo,” alisema Mbilinyi ambaye pia ni Mbunge wa Mbeya Mjini.
Aliwaomba ndugu, marafiki, mashabiki na wapenda muziki wa taarabu pamoja na familia za wafiwa wawe na moyo wa uvumilivu na subira katika kipindi hiki cha huzuni kubwa.
Vyanzo:TZMPAKAAU,Nipashe,picha globlal publishers,dinamarios.blogspot.com.

Keine Kommentare:

Kommentar veröffentlichen