- Serikali kigugumizi
- Tanesco kigugumizi
Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini, wakiongozwa na Mwenyekiti wao, Januari Makamba (wa kwanza kushoto), wakiwa kwenye kikao na maafisa wa Wizara ya Nishati na Madini chini ya uongozi wa Waziri wa wizara hiyo, William Ngeleja (wa 2 kulia), kwenye ofisi ndogo za Bunge jijini Dar es Salaam jana.
Dowans ni kizungumkuti. Si serikali wala Shirika la Umeme nchini (Tanesco) ambao wako tayari kuzungumzia mambo mawili kuhusu kampuni hiyo.
Moja, kuhusu kuwashwa kwa mitambo ya Kampuni ya Dowans Limited ya kufua umeme kwa kutumia gesi asilia, na mbili, kuhusu kuwasili nchini kwa mtu anayejiita mmiliki wa kampuni hiyo, Brigedia Jenerali Mstaafu Sulaiman Mohammed Yahya Al Adawi.
Wakati kuna taarifa kwamba mitambo ya Dowans imewashwa kwa ajili ya kuzalisha umeme wakati bado kuna mgogoro wa kisheria kati ya Dowans na Tanesco, si viongozi wakuu wa Tanesco wala Wizara ya Nishati na Madini waliokuwa tayari kuzungumzia suala hilo.
Aidha, mamlaka hizo zimekataa kutoa ufafanuzi kuhusu ziara ya Al Adawi mfanyabiashara anayedaiwa kuwa ndiye mmiliki wa Dowans ambaye aliwasili nchini mwishoni mwa wiki.
Jana Tanesco ilishindwa kutoa taarifa kuhusu kinachoendelea mpaka sasa. Mwandishi wetu aliyekuwa katika mkutano wa 13 wa Shirika la Ubia wa Umeme katika eneo la Ukanda wa Afrika Mashariki (EAPP) uliofanyika jijini Dar es Salaam, aliomba kupata ufafanuzi kutoka kwa maofisa waandamizi wa Tanesco, lakini juhudi zake ziligonga mwamba. Meneja uzalishaji wa Tanesco, Stephen Kabadi, aliyemwakilisha Mkurugenzi Mtendaji, alipoulizwa, aliwaelekeza waandishi kuzungumza na Meneja wa Mawasiliano wa Tanesco, Badra Masoud. Naye Badra alisema: “Ni kweli tulikuwa tumeahidi kutoa maelezo ya suala hilo kuanzia leo (Jana), lakini kwa leo (jana) tuna huu mkutano ambao sisi ndio wenyeji, hivyo haitawezekana kutoa maelezo, lakini tutatoa siku nyingine.”
TANESCO WATHIBITISHA BARUA YA DOWANS
Wakati watendaji wa Tanesco wakisita kuzungumzia Dowans, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imethibitisha kuwa Tanesco imepokea barua rasmi kutoka Dowans inayotaka kukubali wafanye mazungumzo yenye lengo la kulifutia deni la Sh. bilioni 94 kutokana na kuvunja nayo mkataba.
Hayo yalibainishwa jana jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa kamati hiyo, January Makamba, kufuatia taarifa ya Tanesco iliyowasilishwa kwa kamati hiyo.
Makamba akizungumza na waandishi wa habari baada ya kumalizika kwa kikao hicho, alisema Tanesco imewaambia kwamba Dowans wamekubali kufuta deni lililotokana na riba.
Hata hivyo, alisema katika baraua yake Dowans imesema itaendelea kuidai Tanesco fedha za kuwauzia umeme kwa kuwa hiyo ilikuwa ni sehemu ya biashara, kwani ilitumia gharama kuzalisha nishati hiyo.
Makamba alisema licha ya kukutana na Tanesco, lakini pia kamati yake ilikutana na Waziri wa Nishari na Madini, William Ngeleja, na maofisa wa wizara yake na kuwataka waieleze kamati hiyo mikakati waliyonayo katika kukabiliana na tatizo la umeme.
Alisema Ngeleja alitoa maelezo ya kina kuhusu mipango yake na kwamba kamati ilimshauri kuharakisha jitihada hizo ili kuwezesha ukodishaji wa mitambo ya dharura ili kukabiliana na tatizo hilo. Mitambo inayotarajiwa kukodishwa itazalisha megawati 260 ambapo kati ya hizo megawati 160 zitazalishwa kwa kutumia mafuta na nyingine 100 kwa kutumia gesi.
MKURUGENZI TANESCO AZIDI KUMRUKA AL ADAWI
Kuhusu serikali kumualika Al Adawi, Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, William Mhando, alisema hawakuwa na taarifa zake na kwamba walisoma habari zake kupitia vyombo vya habari.
“Sisi Tanesco hatumjui mtu huyo wala hatukumualika huyo anayejiita mmiliki wa Dowans hivyo inakuwa vigumu kukomenti (kusema) chochote juu ya suala hilo,” alisema.
NGELEJA AKATAA KUMZUNGUMZIA AL ADAWI
Kwa upande wake, Ngeleja akizungumza na waandishi wa habari jana, alikataa kusema kama serikali ilijua ujio wa Al Adawi nchini kwa madi kwamba suala hilo lipo mahakamani.
HATUJAWASHA MITAMBO
Katika hatua nyingine, Mhando alikanusha madai kwamba Tanesco imewasha mitambo ya Tanesco ili kusaidia kuzalisha umeme ili kukabiliana na mgawo unaoendelea. Hata hivyo, alisema Tanesco iko tayari kufanya mazungumzo na Dowans ili kutumia mitambo yao kwa sharti la kuweka mbele sheria.
Wakati Mhando akikanusha kuwashwa kwa mitambo hiyo, uchunguzi uliofanywa na gazeti hili, umebaini kuwa mashine mbili zilizo katika mtambo wa Dowans eneo la Ubungo jijini Dar es Salaam, ziliwashwa tangu juzi. NIPASHE ilifika jana jioni katika ofisi za Tanesco jirani na ulipo mtambo huo, lakini hakuna mfanyakazi aliye kuwa tayari kuthibitisha kama mitambo hiyo imewashwa kwa maelezo kuwa wao si wasemaji.
Hata hivyo, habari kutoka ndani ya eneo iliyopo mitambo hiyo zilithibitisha kuwashwa kwa mashine mbili toka juzi na mwandishi wetu alisikia zikinguruma. Aidha, chanzo chetu kilieleza kuwa Bodi ya Tanesco ilikutana jana katika kikao kilichomalizika majira ya jioni. Hata hivyo, haikujulikana mara mambo yaliyojadiliwa.
source:Nipashe
Keine Kommentare:
Kommentar veröffentlichen