Best Blogger TipsSoon

Donnerstag, 17. Februar 2011

TZMPAKAAU

Milipuko ya mabomu gongo la mboto Dar.
      




   
Watoto wa waathirika wa milipuko ya mabomu huko gongo la mboto kama walivyokutwa na mpiga picha
ndani ya hema



waathirika waliofurika mpaka nje ya hospitali
  •  Yaasababisha vifo vya watu 20
  • Majeruhi zaidi ya 300
  • Uharibifu mkubwa makazi na wa mali za watu
  • Waziri mwinyi na mkuu wa majeshi wagoma kujiuzulu
Maelfu ya wakazi wa Ukonga Gongo la Mboto na maeneo mengine ya jirani, juzi walilazimika kuhama makazi yao kufuatia milipuko hiyo.
Maandamano ya watu hao ya kuhama eneo hilo, yalihusisha makundi mbalimbali wakiwemo wanawake, wanaume, wazee na watoto ambao baadhi walionekana wakielekea eneo la Uwanja wa Taifa na Buguruni.
Baadhi ya wanawake na wanaume walionekana wakiwa wamebeba watoto wao huku kichwani wakiwa na mizigo ya mabegi na vitu mbalimbali.
Aidha, pikipiki, baiskeli, magari makubwa na madogo yakiwemo ya kubebea takataka yalionekana yakiwa yamesheheni wakazi hao ambao walikuwa wakitokea Gongo la Mboto kuelekea maeneo ya mjini na wengine wakitoka eneo hilo kuelekea mkoa wa Pwani, Kisarawe.
Baadhi ya magari yalionekana yakiwa na bendera za Chama cha Wananchi (CUF) ambayo yalijitokeza kutoa msaada kwa kuwachukua waathirika hao na kuwapeleka maeneo ambayo ni salama.
Tafrani hiyo ilisababisha foleni kubwa kwenye barabara hiyo ambayo ni nyembamba huku baadhi ya madereva wakionekana kuvunja sheria na kupita maeneo ya watembea kwa miguu, hali iliyosababisha gari moja aina ya Toyota DCM daladala lenye namba za usajili T 989 ALR kupinduka eneo la Banana.
Katika ajali hiyo, zaidi ya watu 40 walijeruhiwa na kukimbizwa hospitalini kwa matibabu.
Licha ya msururu huo wa watu uliokuwa ukielekea mjini, baadhi waliohojiwa na NIPASHE walisema kuwa hawajui wanaelekea wapi.
Amina Abdallah (40) mkazi wa Gongo la Mboto Gerezani, aliyekutwa akiwa na watoto watatu wa mwisho akiwa na umri wa miezi miwili, alisema kuwa amelazimika kuungana na msururu huo ili kujinusuru na mabomu hayo.
Amina ambaye alikutwa akiwa amebeba begi moja la nguo kichwani na mtoto wake akiwa mgongoni huku wengine wakiwa nyuma yake wakimfuata polepole, alisema amefikia uamuzi ili kuyanusuru maisha yake na familia yake.
Alisema hadi muda huo alipokuwa akizungumza saa 6:45 mchana alikuwa hajala chochote na familia yake zaidi ya maji.
MABOMU YAZAGAA
Katika hatua nyingine, NIPASHE ilishuhudia baadhi ya maeneo yakiwa na mabaki ya mabomu mengine yakiwa pembezoni mwa barabara na mengine kwenye makazi ya watu.
Pia kuna mabaki ya bomu ambalo lilikutwa nje ya Shule ya Msingi Pugu ambapo baadhi ya askari walionekana kuyazungushia alama zinazoashiria kuna hatari.
Kadhalika, nyumba kadhaa zimeezuliwa mabati na nyingine kubomoka baada ya mabomu yaliyokuwa yakiruka kutoka kwenye kambi hiyo kuangukia huko.
Baadhi ya majeruhi waliozungumza na gazeti hili, walisema kuwa kwanza wanamshukuru Mungu kwa kupigania uhai wao.
Majeruhi wa mguu, Lina Ngosingosi (40), mkazi wa Pugu Chanzi, ambaye amelazwa hospitali ya Wilaya ya Kisarawe, akisimulia jinsi alivyojinusuru na mabomu hayo alisema alikimbia zaidi ya kilomita 10 na kufanikiwa kujificha nyuma ya kichuguu kirefu kilichopo katika pori la Mbalige.
Lina alisema kabla ya kufika kwenye kichuguu hicho, wakati bomu la kwanza likilipuka alikuwa nyumbani kwake na kaka zake wakila chakula cha usiku.
Alisema baada ya mlipuko huo, walidharau wakidhani ni hitilafu ya umeme iliyosababishwa na jenereta kubwa lililopo jirani na eneo analoishi.
“Sikutilia maanani, sijawahi kufikiria kama siku moja mabomu yangelipuka eneo hili, lakini mlipuko wa pili ambao ulikuwa na kishindo kikubwa sana ulisababisha nikimbie huku mtoto wangu mdogo wa miaka miwili akiwa mgongoni sikuwa najua ninakoelekea kuna usalama au la,” alisema na kuongeza:
“Nikiwa naendelea kukimbia nilisikia kitu kimepita juu yetu, mwanangu mwingine aliniambia mama bomu linatufuata nyuma, niliwaambia wanangu tunakufa, lakini kitu kile kilipitiliza na kuangukia kwenye nyumba iliyokuwa mbele yetu ya kulala wageni ijulikanayo kama 'Kikubwa Roho' iliyopo eneo la Chanzi, bomu lilibomoa sehemu ya mbele na kutokea nyuma ya nyumba hiyo,” alisema.
Alisema licha ya kuona bomu hilo likiwa kwenye uwelekeo wao, waliendelea kukimbilia huko na kujikuta wakiwa kwenye pori hilo ambalo kwa wakati huo lilikuwa limezingirwa na askari kadhaa wenye silaha.
JESHI LA POLISI LAONYA
Majira ya mchana jana Jeshi la Polisi liliwaonya wale wote wanaopotosha jamii kwa taarifa zisizo rasmi zinazohamasisha wakazi wa maeneo ya Gongo la Mboto kuhama makazi yao kwa kuhofia milipuko itakayoendelea kutokea.
Akizungumza na waandishi wa habari, Msemaji Mkuu wa Jeshi la Polisi, Advera Senso, alisema kumekuwa na taarifa zinazofikia jamii ambazo hazina ukweli wowote na kusababisha wananchi kuwa na wasiwasi juu ya maisha yao na mali zao.
“Tunawasisitiza wananchi kuwa watulivu na waendelee na kazi zao kama kawaida kwa sababu hali hiyo imedhibitiwa kwa sasa hakuna milipuko inayoendelea,” alisema.
“Tunaomba wananchi wajitokeze katika vituo ambavyo waathirika wamehifadhiwa kuja kuwatambua ndugu jamaa na marafiki ikiwemo watoto waliopotezana na wazazi wao wakati wa milipuko,” alisema.
Jeshi hilo limewataka wananchi kutoa ushirikiano ikiwemo kutokugusa wala kuruhusu watoto kuchezea vyuma ambavyo wanavitilia shaka na badala yake wakiviona watoe taarifa kwa kupiga simu namba 0782 114 515; 0783 260 334; 0774 039 029 na 0755 756 410 kwa msaada zaidi.
Alisema wote waliopotelewa na watoto wao waende vituo vya polisi Ukonga, Buguruni, Tazara, Uwanja wa Uhuru na Sabasaba.
CHUO CHA UGAVI CHAFUNGWA
Huko Chanika Chuo cha Ugavi (IPS), kilifungwa kwa muda na wanafunzi wote wameamriwa kuondoka chuoni hapo hadi siku ya Jumatatu kama hali itakuwa imetulia.
Mmoja wa wanafunzi wa chuo hicho, ambaye hakutaja jina lake aliliambia NIPASHE kuwa watu wengi wa Gombo la Mboto mwisho wa lami kukimbilia Chanika wakidhani kule ni salama.

UWANJA WA UHURU WAFURIKA
Alisema hadi kufikia jana asubuhi, kulikuwa na wananchi takribani 4,000 katika uwanja wa Uhuru ambao wamehifadhiwa wakati kazi hiyo inaendelea kufanyika.
Alisema yako mabomu ambayo yanasadikika kuwa yameanguka katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere na kwamba wataalam walitoa ushauri wa aina mbili.
Alifafanua kuwa ushauri huo ni kutahadharisha ndege ambazo zilitakiwa kutua juzi usiku kutokufanya hivyo kwa sababu za kiusalama.
“Lakini walichukua hatua nyingine ya uwanja ule kufungwa kwa muda hadi pale wahandisi watakavyofanya ukaguzi na kuwa na uhakika kwamba hakuna bomu ambalo liko pale,” alisema Pinda na kuongeza:
“Mheshimiwa Rais aliarifiwa jana (juzi) usiku na Mkuu wa Majeshi na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Dar es Salaam kuwa walianza kazi jana (juzi) usiku, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ilielekeza jitihada zake zote katika kuona hatua stahiki zinazoweza kuchukuliwa,”alisema.
Alisema Jeshi nalo litaunda baraza la kuchunguza kwa mujibu wa Sheria ya Ulinzi ili kubaini hasa chanzo ni nini na hatua stahiki ziweze kuchukuliwa.

4 Kommentare:

  1. Hello ppo this is new blog just everyone is welcomed to be part of it

    AntwortenLöschen
  2. Hello ppo if y hv any idea of what should be put inside this site i real want ideas

    AntwortenLöschen
  3. Daaah kweli hii serikali sijajua kama inawajali wananchi wake kiasi cha kutosha yaani serikali gani inawalipua wananchi wake kwa mabomu

    AntwortenLöschen
  4. Dieser Kommentar wurde vom Autor entfernt.

    AntwortenLöschen