- Helikopta ya Chadema kunyanyuka kesho
- Mangula kuiongezea nguvu CCM
- Ujio wa Mchungaji Mtikila wa (DP) wasubiriwa kwa hamu
Wakati leo ikiwa ni mwanzo wa wiki ya lala salama katika kampeni za uchaguzi mdogo wa ubunge Jimbo la Igunga, mkoani Tabora, vyama vya siasa vinavyowania ubunge katika jimbo hili vitaanza kutafunana kila kimoja kikitaka kurusha karata yake ya mwisho kwa ajili ya kupata uhalali wa mgombea wake kuchaguliwa.
CHADEMA kesho kitaanza kutumia helikopta (Chopa),Erasto Tumbo aliyasema haya hata kabla ya kuzinduliwa kwa kampeni akizungumza igunga alisema "Kama kawaida yetu tayari helikopta imeandaliwa kwa mashambulizi,lakini hatutaanza nayo tutaanza na vyombo vya ardhini kwanza tukiona kuna ulazima,ndipo tutakaponyanyuka juu kwa juu na kumwaga sumu chini"
Wakati huo huo, Chadema kimemshushia kombora Rostam kuwa ameshindwa kuwapatia huduma ya maji safi na salama wananchi wa Igunga na kuwafanya kutumia maji yenye tope na harufu mbaya.
Uchaguzi huo utafanyika Jumapili ijayo kujaza nafasi iliyoachwa wazi na Rostam Aziz wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) aliyejiuzulu Julai 13, mwaka huu akidai kuchoshwa na siasa uchwara, fitina na kuandamwa ndani ya chama hicho.
MANGULA APANDA JUKWAANI RASMI

Bw. Philip Mangula katibu wa zamani wa CCM
CCM ambacho kimemsimamisha mgombea wake, Dk. Peter Kafumu, kimeongeza nguvu kwa kumpeleka Katibu Mkuu Mstaafu, Philiph Mangula ambaye jana alipanda jukwaani na kuhutubia mkutano wa kampeni katika kijiji cha Mwamasunga A.
Tangu kufika kwa Mangula na kada mwingine, Stephen Masishanga, wamekuwa wakijishughulisha zaidi na mikutano ya ndani.
Kwa upande wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), juzi kiliongeza nguvu kwa kumpeleka Naibu Katibu Mkuu wake, Zitto Kabwe na Mbunge wake wa Ilemela, Highness Kiwia.
Zitto amepelekwa moja kwa moja katika Kata ya Isakamalia ambako ndipo mahali Mkuu wa Wilaya ya Igunga, Fatuma Kimario, alikamatwa na kuwekwa chini ya ulinzi na wafuasi wa Chadema.
Zitto atakuwa katika mchuano na Mbunge wa Tabora Mjini (CCM), Ismail Aden Rage, ambaye chama chake pia kimempangia kufanya kampeni za kumnadi Dk. Kafumu.
Hata hivyo, baada ya Rage kudaiwa kupanda na bastola katika jukwaa la mkutano wa kampeni, Chadema wamemshtaki kwa msimamizi wa uchaguzi wa jimbo hilo, Protace Magayane, wakitaka aondolewe katika kinyang’anyiro hicho kwa kukiuka maadili ya uchaguzi.
CHOPA YA CHADEMA KUANZA KAZI KESHO
Chopa la CHADEMA lililotumiwa kule Busanda
Ujio wa Mch.C.Mtikila wasubiriwa kwa hamu
Mwenyekiti wa Democratic Party(DP) Mch Mtikila
huku Mwenyekiti wa Chama cha Democratic (DP), Mchungaji Christopher Mtikila, anatarajiwa kuwasili kesho na kuhutubia mkutano wa hadhara.
Magari ya matangazo yalikuwa yakipita katika maeneo mbalimbali ya mji wa Igunga kutangazia kuhusiana na ujio wa Mtikila ambaye chama chake kimesimamisha mgombea.
LISSU AMRUSHIA ROSTAM KOMBORA

Mbunge wa Singida mashariki na mwanasheria wa chama cha CHADEMA bw.Tundu Lissu
Akimnadi mgombea wa Chadema, Joseph Kashindye, katika Kata ya Bukoko, Mkurugenzi wa Sheria na Haki za Binadamu, Tundu Lissu, alisema Katibu Mkuu wa CCM, Wilison Mukama, amekuwa akitamba kuwa Rostam katika kipindi chake cha miaka 18, aliwezesha kuiletea maendeleo Wilaya ya Igunga kwa kuitoa ya mwisho kuwa ya kwanza katika Mkoa wa Tabora, lakini katika hali ya uhalisia halifanani.

Mbunge aliyejiuzulu baada ya kugubikwa na kashwa nzito nzito bw. Rostam Aziz
”Nilipokuwa ninasikia Mukama akimsifia Rostam kuwa ameleta maendeleo na kuifanya Igunga kuwa wilaya ya kwanza, nilifikiria kuwa itakuwa tofauti kimaendeleo. Nimekuja hapa wiki mbili zilizopita, nimesikitishwa sana na huduma ya maji inayotolewa katika jimbo hili,” alisema Lissu.
Alisema amefikia katika hoteli nzuri iliyopo mjini Igunga, lakini maji yanayotoka bombani ni tope na yananuka, hali inayowafanya kushindwa kuyatumia hata kupigia mswaki.
Alisema ukitaka kuyaoga maji hayo unalazimika kuyaweka ili yachujike kabla ya kuyatumia na kuwataka wananchi kumchagua Kashindye akatatue tatizo hilo pamoja na matatizo mengine yanayolikabili Jimbo la Igunga.
”Maendeleo ambayo tunaambiwa Rostam Aziz amegeuza kuwa wilaya ya kwanza mbona hatuyaoni?” alihoji.
Aidha, Lissu alisema Sh milioni 818 zilizokuwa zimetengwa na Bunge la Jamuhuri katika bajeti ya mwaka jana kwa ajili ya matumizi ya maendeleo ya Wilaya ya Igunga, zimetumika kinyume na maelekezo ya serikali.
Alisema kwa mujibu wa ripoti ya Mkaguzi na Mthibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kwa kipindi cha miaka miwili inaonyesha kuwa fedha zinazopelekwa kwa ajili ya matumizi ya maendeleo kwenye wilaya hiyo kwa muda wa miaka miwili maendeleo yake hayaridhishi.
Alisema fedha hizo zimekuwa zikienda katika matumizi binafsi na hivyo kuishia kuwataka wananchi kutoa michango kwa ajili ya maendeleo yao.
KASHINDYE AAHIDI MAENDELEO

Kwa upande wake, Kashinye, alisema mambo yaliyomsukuma kugombea ubunge katika jimbo hilo ni pamoja na kutoona jamii inashirikishwa katika suala la kugawa maeneo ya uchimbaji kwa wawekezaji.
Alisema iwapo watamchagua, atafuta mpango mzima wa kuwagawia wawekezaji maeneo ya uchimbaji na kuanza upya mchakato wa ugawaji wa maeneo hayo kwa kuwashirikisha wananchi wenye ardhi.
Alisema pia jambo jingine lilomsukuma ni huduma ya maji safi na salama ambayo alisema haipatikani na mahali pachache inapopatikana maji yake si safi wala salama.
Alifafanua kuwa fedha kwa ajili ya maendeleo zipo na kwamba kinachotakiwa ni kiongozi safi atakayeweza kusimamia miradi ya maji, barabara na mengine vyema.
Alisema iwapo wananchi wataridhia Jumapili ijayo na kumchagua, maisha yake yote ya ubunge yatakuwa Igunga.
Vyanzo:Ippmedia,TZMPAKAAU
Keine Kommentare:
Kommentar veröffentlichen