Best Blogger TipsSoon

Dienstag, 1. März 2011

TZMPAKAAU



Jamii ya watanzania imeendelea na dhana yake ya mshikamano
  • Hili limedhihirika katika kipindi hichi cha wiki mbili toka kutokea kwa milipuko Gongo la Mboto
Waathirika wa milipuko ya mabomu katika kambi ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kambi ya Gongo la Mboto, jijini Dar es Salaam, jana walimwagiwa misaada zaidi yenye thamani ya mamilioni ya shilingi.
Miongoni mwa waliotoa misaada hiyo, ni pamoja na Mwenyekiti Mtendaji wa IPP, Reginald Mengi, ambaye alimkabidhi Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, msaada wa tani 17 za vyakula mbalimbali kwa ajili ya kuwasaidia waathirika hao.
Mbali na vyakula, Mengi pia alimkabidhi Waziri Mkuu hundi yenye thamani ya Sh. milioni 13.5 kwa ajili ya kuzipa familia 27 zilizofiwa na ndugu kufuatia tukio hilo kwa kila moja kugawiwa Sh. 500,000 katika fedha hizo kama mkono wa pole.
Vyakula vilivyotolewa na Mengi jana katika kituo cha kupokelea misaada cha kamati ya maafa ya mkoa wa Dar es Salaam kilichopo katika ofisi za Kata ya Ukonga, ni pamoja na unga wa sembe, mchele, sukari na maharage.
Akikabidhi msaada huo, Mengi aliwapa pole wafiwa wote kwa kuondokewa na ndugu zao waliokuwa wakiwapenda na pia akamuomba Mwenyezi Mungu awasaidie marehemu kuwaweka mahali pema peponi.
Wengine waliotoa misaada jana, ni Balozi wa Russia nchini, Alexander Aristov Rannikh, aliyetoa Dola za Marekani 100,000 (Sh. milioni 151.7), Kampuni ya Sahel Trading iliyotoa kifaa maalum cha kusaidia kutambua mabomu yaliyozagaa mitaani.
Katika hatua nyingine wasanii wa muziki wa kizazi kipya na filamu waliotoa hundi yenye thamani ya Sh. milioni 72 zilizopatikana baada ya mechi ya mpira wa miguu baina yao,pia wasanii hawa wametoa magunia 200 sukari na magunia 200 ya mchele; na Serengeti Breweries Limited (SBL) (mabati 300, mifuko ya saruji 300, mashuka 200 na vyandarua 200).
Wengine ni Hiland Estate (tani 10 za mchele) Seuma Group (kilo 150 za unga, kilo 30 za maharage na sabuni), Zakaria Group of Company/Murza Oil Group (mifuko 1,000 ya saruji); Benki ya Baroda (hundi yenye thamani ya Sh. milioni 2); wafanyakazi wa Benki ya Barclays (lita 350 za damu na vyakula vyenye thamani ya Sh. milioni 2.4 na nguo).
Awali, Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Saidi Meck Sadiki, alisema kufikia jana, watu 27 walikuwa wamepoteza maisha na kwamba, iwapo itathibitika kifo cha mtu mmoja aliyefariki dunia juzi kina uhusiano na tukio hilo, atakuwa ametimiza idadi ya watu 28.
Sadiki alisema kati ya watoto 1,069, waliopoteana na ndugu zao, wamekwisha kuchukuliwa, 11 wapo katika kituo cha Ustawi wa Jamii Kurasini na kwamba, wengine zaidi ni watoto wa mitaani na waliokwenda Dar es Salaam kufanya kazi.
Alisema iwapo ndugu zao hawatajitokeza kuwachukua, watawarudisha makwao.
Kaimu Mkuu huyo wa Mkoa alisema nyumba 69 zilizokuwa zikitumiwa na kaya 100 na watu 459, zimeanguka na uharibifu mkubwa ulitokea kwenye shule 10 (za msingi na sekondari) pamoja na zahanati moja.
Alisema wathamini wamekadiria kuwa ili kuzirejesha shule hizo katika hali nzuri na watoto kuendelea kusoma, zinahitajika Sh. milioni 120.
Hata hivyo, alisema wanakabiliwa na changamoto kadhaa, ikiwamo ukubwa wa kazi ya kuwafikishia waathirika misaada kutokana na kuwapo mtandao mpana wa kuwafikia waliko, na pia mabomu kuzagaa maeneo mengi.
Alisema pamoja na kuwapo timu tisa za uhakiki wa nyumba zilizoathirika, kazi ya kuzihakiki imekuwa kubwa kinyume cha walivyotarajia na kusema:
“Nadhani tunaweza kuongeza siku mbili zaidi ili kukamilisha kazi hiyo.”
Naye Pinda alisema mabomu yaliyolipuka ni mengi na gharama yake ni kubwa, hivyo akasema lazima serikali ilitazame jambo hilo kuona namna itakavyoweza kulirejeshea jeshi uwezo ili kuhakikisha kwamba, Watanzania wanaendelea kulindwa muda wote kadiri inavyotakiwa.
Alisema kutokana na ugumu wa kazi iliyopo, inaweza kuchukua muda mrefu kuyaona na kuyaondoa mabomu yaliyozagaa mitaani.
Alisema serikali imepokea salamu nyingi za pole kutoka nje ya nchi, lakini akataka shukrani za pekee ziende kwa Serikali ya Msumbiji chini ya Rais wake wa sasa, Armando Guebuza, kwa kutuma timu nchini kuja kubadilishana uzoefu na serikali ya Tanzania, walioupata wakati nchi yao (Msumbiji) ilipopatwa na janga kama hilo mwaka 2007.
Aliitaka kamati ya maafa kusimamia na kuigawa vizuri misaada iliyopatikana na akatumia fursa hiyo kumshukuru Balozi Aristov, Mengi, wasanii na wasamaria wema wengine wote kwa misaada waliyoitoa kwa waathirika.
Pinda pia alitumia fursa ya jana, kuwatembelea waathirika katika eneo la Majohe na katika ghala la kuhifadhi misaada mbalimbali lililoko Shule ya Sekondari Pugu.

1 Kommentar: