Best Blogger TipsSoon

Montag, 21. Februar 2011

TZMPAKAAU

Mbeya Institute of science and Technology(MIST) kuwa chuo kikuu

  •  Mpango kukamilika ndani ya miaka mitano
  • Ni ahadi ya mawaziri wa mawasiliano, sayansi na Teknolojia 


WAZIRI wa Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia na naibu wake, hatimaye, wameamua kupambana na fupa lililowashinda watangulizi wao: Wamewaahidi wananchi wa Mkoa wa Mbeya kwamba Taasisi ya Sayansi na Teknolojia (MIST) iliyopo mkoani humo itakuwa chuo kikuu ndani ya miaka hii mitano.

Akizungumza na uongozi wa Taasisi hiyo ya MIST, hivi karibuni, Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Charles Kitwanga, alijitwisha mzigo huo ikiwa ni baada ya Raia Mwema kumtaka atoe msimamo wa serikali kuhusu uamuzi wake wa miaka mingi wa kuipandisha hadhi taasisi hiyo na kuwa chuo kikuu.

Kiu ya wakazi wa Mbeya inajengeka na imani yao kwamba mazingira ya mkoa huo yana sifa zote zinazohitajika ili kujengwa kwa taasisi kubwa za elimu kama chuo kikuu, hivyo kushangazwa na hatua ya serikali kusuasua katika utekelezaji wa maamuzi yake ya kuigeuza taasisi hiyo kuwa chuo kikuu.

Katika majibu yake, Naibu Waziri huyo, alianza kwa kusema:“Hii bado ni Taasisi ya Sayansi na Teknolojia, mpango mkakati ni kuifanya iwe Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia, tumo kwenye mkakati. Kuna taratibu za kufuata. Kwa mfano, walimu wenye sifa za kufundisha chuo kikuu, kuna mambo ya kisheria, majengo, pesa na muundo wa chuo chenyewe.”

Na alipobanwa kuhusu mkakati kuchukua miaka mingi kiasi cha wananchi kukosa imani, ndipo Waziri Kitwanga alipojibu akisema:“Ndani ya miaka mitano ijayo; yaani kati ya 2010 na 2015, taasisi itakuwa imekamilika kuwa chuo kikuu. Itakapokuwa chuo kikuu, bado mafunzo ya kada zingine yaliyokuwa yakitolewa na taasisi yataendelea kutolewa. Kwa hiyo pamoja na mtazamo huo wa kuifanya taasisi hiyo kuwa chuo kikuu, bado lazima kuangalia soko; kwa maana ya technicians. Lengo ni uwiano wa 1:5.”

Kauli hiyo ya Kitwanga inakuja siku chache tangu bosi wake, Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia Prof. Makame Mbarawa Mnyaa kutoa msimamo huo huo pale alipotembelea taasisi hiyo mara tu baada ya kuteuliwa kushika wadhifa huo mwishoni mwa mwaka jana.

Wakati wa wizara hiyo alisema:“Serikali ina nia ya dhati ya kuifanya Taasisi ya Sayansi na Teknolojia Mbeya kuwa chuo kikuu ndani ya miaka mitano. Na hiki kitakua chuo kikuu pekee cha ‘ICT’ cha Tanzania. Chuo kingine kama hicho kipo nchini Rwanda.”

Katika kuthibitisha dhamira hiyo ya serikali, Waziri Mnyaa aliahidi kutembelea tena taasisi hiyo mwezi Machi mwaka huu wa 2011 ikiwa ni sehemu ya kufuatilia kwa ukaribu zaidi maendeleo ya shughuli hiyo; hii ikiwa ni mbali na kuwatuma watendaji wake pale wizarani wakiwemo Mkurugenzi wa Sayansi na Teknolojia, Prof. Evelyne Mbede na Naibu Waziri wake aliyefanya ziara yake hivi karibuni.

Simulizi za taasisi hiyo, ambayo awali ilijulikana kama Chuo cha Ufundi Mbeya(MTC) na baadae Taasisi ya Sayansi na Teknolojia Mbeya (MIST), kupandishwa hadhi na kuwa chuo kikuu zimekuwepo kwa zaidi ya muongo sasa; huku kila ifikapo wakati wa Uchaguzi Mkuu wananchi wakihakikishiwa kuhusu kukamilika kwa mchakato huo ndani ya kipindi kifupi.

Viongozi mbali mbali waliotembelea mkoa huo wakiwemo wakuu wa nchi wamekutana na swali hilo mara kadhaa, na wote walitoa ahadi ya aina hiyo hiyo yenye matumaini kwa wananchi wa mkoa huo.

Lakini safari hii, ahadi ya Waziri na Naibu wake imekuwa ya matumaini makubwa zaidi kutokana na uwazi wake; kwani wametoa hadi muda wa mchakato huo kukamilika, na hivyo kutoa matumaini kwamba suala la MIST kuwa chuo kikuu laweza likawa historia ndani ya miaka mitano ijayo.

Kwa upande wa Waziri Kitwanga, pamoja na kubeba zigo hilo la watangulizi wake, alitoa pia salamu rasmi kwa taasisi hizo nchini, na kwamba zijielekeze katika kuandaa wataalamu wenye ujuzi na mawazo tofauti.

“Focus iwe kutayarisha wataalamu watakaolitoa taifa kutoka kwenye kuuza raw products hadi processed, ku-add value ya bidhaa, kilimo cha quality products, kwa mfano chungwa lizalishwe kwa saizi moja kama yale kutoka Afrika Kusini,” anasema Waziri Kitwanga na kuongeza:

“Ufundishaji ulenge kuwafanya wahitimu waweze kujiajiri badala ya mawazo ya kuajiriwa, fursa za ajira binafsi zipo nyingi. Kuajiriwa iwe kwa muda tu, vijana wafundishwe ujasiriamali, wataweza kuwakusanya mafundi walioko mitaani, wataunda vikundi, ajira zitakuwa rasmi; kisha watalipa kodi. Hivi sasa mafundi ni wengi mitaani na hawalipi kodi.”

Pamoja na mzigo wa MIST kuwa chuo kikuu, Waziri Kitwanga alijitwisha mzigo mwingine pale alipotoa changamoto kwa taasisi hizo akiziagiza ziende na wakati, kwa kuingia kwenye teknolojia mpya ili mazingira wanayosomea wanafunzi yalingane na yale watakayofanyia kazi.

“Mazingira mnayosomea hapa hayalingani na mtakayofanyia kazi. Itabidi mkajifunze tena,” anatahadharisha Waziri huyo wakati akizungumza na wanafunzi wa taasisi hiyo.

Wakati Waziri huyo akitoa changamoto hiyo ya taasisi hizo kwenda na wakati, taarifa kutoka kwa uongozi wa MIST pamoja na wanafunzi zinabainisha kuwepo kwa uhaba mkubwa wa vitabu kukidhi matakwa ya mitaala ya mafunzo ya stashahada ya kawaida na shahada ya kwanza, haina jengo maalumu la maktaba, mitambo na vifaa vya karakana na maabara, na kwamba licha ya uchakavu vingi vilivyopo ni vya zamani na vilivyopitwa na wakati.

Mwanafunzi wa mwaka wa tatu wa Shahada ya Uhandisi Ujenzi, Jacob Mambo analizungumzia suala la vifaa kwa uchungu zaidi kwa kusema:

“Maabara zimechakaa, haziendani na mfumo wa sasa. Tunahitaji utekelezaji badala ya ahadi. Hatuna hata intaneti na maktaba ni ndogo sana, na haina vitabu.”

Taasisi ya Sayansi na Teknolojia Mbeya (MIST- Mbeya Institute of Science and Technology) ilianzishwa rasmi mwaka 2004 baada ya kukipandisha hadhi kilichokuwa Chuo cha Ufundi Mbeya (MTC- Mbeya Technical College) ambacho kilianzishwa mwaka 1986.

MTC ilianzishwa chini ya ushirikiano wa Serikali na iliyokuwa Shirikisho la Nchi za Kisovieti la Urusi kikiwa na idara nne za uhandisi ujenzi, uhandisi mitambo, uhandisi umeme na general studies.

Chuo hicho kiliendelea kujipanua kitaaluma kutokana na kuongezeka kwa mahitaji kama ilivyofanyika mwaka 1992 ambapo waliongeza idara ya usanifu majengo.

Hata hivyo, mabadiliko makubwa yalifanyika baada ya kupandishwa hadhi na kuwa taasisi ambapo idara mpya zilianzishwa ikiwemo ya kompyuta, elimu endelevu, utafiti na baadaye idara ya ushauri na utafiti na uchapishaji.

Taasisi hiyo hivi sasa inatoa mafunzo ya stashahada ya kawaida katika fani za usanifu majengo, uhandisi kompyuta, uhandisi mitambo, uhandisi ujenzi, uhandisi umeme, teknolojia ya maabara na uongozi wa biashara.

Shahada ya kwanza katika taasisi hiyo inatolewa katika fani za usanifu majengo, uhandisi wa mitambo, uhandisi wa ujenzi, uhandisi wa umeme na uongozi wa biashara.

Tangu kuanzishwa kwake, taasisi hiyo imefanikiwa katika mambo kadhaa ikiwemo kuboresha mitaala iliyokuwepo, kuandaa mitaala ya shahada ya kwanza na kuongeza udahili wa wanafunzi kutoka wastani wa wanafunzi 600 kwa miaka ya 1986 hadi 2007 na kufikia wanafunzi 1,757 kwa mwaka 2010/2011, utoaji wa mafunzo ya awali kwa wanafunzi wasio na alama za kuridhisha na kutengeza samani kukarabati na kuandaa mabweni.

Mkuu wa taasisi hiyo, Prof Joseph Msambichaka anayataja mafanikio mengine yaliyopatikana kuwa ni pamoja na umaliziaji wa majengo mawili kwa ajili ya kutoa huduma ya malazi kwa wanafunzi, kuongeza idadi ya watumishi, usomeshaji watumishi, uandaaji mpango kabambe wa taasisi, ushirikiano na sekta binafsi, ununuzi wa magari, utoaji huduma za ushauri wa kitaalamu, ushirikiano na vyuo vya ndani pamoja na vile vya nje.

Wananchi wanasubiri kwa hamu kuona utekelezaji wa mpango huo wa kuipandisha hadhi taasisi hiyo, na hivyo jiji la Mbeya kuwa makao ya chuo kikuu cha kwanza nchini cha ICT.

1 Kommentar:

  1. Dah unajua niliishi hapo chuoni miaka fulani na maza akiwa mwalimu.....chuo kipo freshi na wakufunzi wake ni wazuri tuuu ila kabla ya kupandishwa hadhi nadhani waalimu wengi zaidi wanahitajika pamoja na facilities za kisasa

    AntwortenLöschen